Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Katika jitihada za
kulinda na kuhifadhi rasilimali za wanyamapori nchini Tanzania, Chuo cha Uongozi
wa Mahakama Lushoto (IJA), kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la
PAMS, kimetoa mafunzo kwa Maafisa wa Mahakama ya namna ya kushughulikia
mashauri ya kesi za wanayamapori na maliasili kwa ufanisi zaidi.
Mafunzo hayo
yaliyofunguliwa jana tarehe 9 Oktoba, 2023 mjini Morogoro yamelengwa kuwafikia
maafisa 157.
Akifungua mafunzo hayo
kwa niaba ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapha Mohamed Siyani,
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa
Mansoor alisema kuwa Mahakama imeweka jitihada za kuhakikisha Majaji na
Mahakimu wanaondokana na makosa ya kiufundi yanayopelekea majangili kuachiwa
huru au kutopewa adhabu stahiki.
Alisema Mahakama imekuwa
ikiwashughulikia majangili wakiwemo majangili wa meno ya tembo na nyara za
serikali ambao mara wanapofikishwa Mahakamani na kupatikana na kosa adhabu yake
huwa ni kuhukumiwa na kifungo chake huwa ni miaka 20 na fidia kwa Serikali.
“Lakini kuna baadhi ya
kesi ambazo hazijapelelezwa, vizuri hivyo unakuta jangili anatoka kwa ajili tu
kuna makosa ya kiufundi katika upelelezi, sasa hilo ndio tunalipatia mwarobaini
kupitia mafunzo haya” alisema Mhe. Mansoor.
Kadhalika alisema mafunzo
hayo yatawapa uelewa wa kutosha na kufanya ustawi wa wanyamapori na misitu
kushamiri huku Wafadhili Pams Foundation na Chuo cha uongozi wa mahakama (IJA)
wakijitahidi kupeleka elimu kwa watendaji wanaotakiwa kulinda wanyamapori,
misitu na mazingira waliyorithi kutoka kwa mababu zao.
Alisema kuna juhudi kubwa
zinafanywa na Shirika la uhifadhi Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya usimamizi wa
wanyamapori Tanzania (TAWA) kuhifadhi aina za wanyamapori zilizopo kwenye
hatari ya kupotea ikiwemo Nyati.
Naye Mkurugenzi wa
mafunzo ya kimahakama kutoka Chuo cha Uongozo wa mahakama Lushoto (IJA) Mhe.
Patricia Kisinda alisema wanatarajia kutoa mafunzo hayo kwa maafisa wa mahakama
zaidi ya 757 kutoka mikoa mbalimbali nchini ambapo wameanza na mikoa mitano
ukiwemo Morogoro, Mtwara, Lindi, Dar es salaam na Pwani.
Kisinda alisema wameamua
kugusa wanyamapori na maliasili sababu ni eneo nyeti katika uchumi wa nchi
sambamba na kuwepo kwa changamoto nyingi katika uendeshaji wa mashauri ya
wanyamapori mahakamani na baada ya tathmini ya mafunzo yaliyopita wameona kuna
tija.
Naye Mkurugenzi wa
Shirika lisilo la kiserikali la PAMS Foundation Samson Kasala alisema katika
kushirikiana na serikali na wananchi kuhamasisha kuelewa umuhimu wa maliasili
wanafanya kazi kwa Pamoja kuhakikisha kwamba majangili, waporaji, wanaohusika
katika kutenda makosa ya jinai wanashughulikiwa na mkono wa sheria.
Naye Wakili wa Serikali
ofisi ya mashtaka taifa mkoa wa Pwani Clarence Mhoja anasema mafunzo hayo
yatawasaidia kufikia hatua nzuri ya kupeleka jalada mahakamani pale wenzao wa
ukamataji na upelelezi wanapotekeleza kazi zao kwa mujibu wa sheria.
Mafunzo hayo
yaliyozinduliwa leo tarehe 9 Oktoba, 2023 yanatarajia kuhitimishwa tarehe 13
Oktoba, 2023 yamewashirikisha wahe. Majaji wa Mahakama kuu, Mahakimu, waendesha
mashataka na wapelelezi ambao kwa Pamoja watajengewa uelewa wa namna ya
kushughulikia mashauri hayo hii ikiwa ni kundi la awamu ya kwanza linalotegemea
kuwafikia maafisa 157.
Meza kuu ikiongozwa na Mgeni rasmi Mhe. Latifa Mansoor (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya Pamoja na waendesha mashtaka wa Tanapa ambao pia ni washiriki wa mafunzo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni