Jumanne, 10 Oktoba 2023

MAHAKAMA MIONGONI MWA TAASISI ZINAZOSHIRIKI WIKI YA VIJANA KITAIFA

Christopher Msagati – Mahakama, Manyara

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara ni miongoni mwa Taasisi mbalimbali za umma na binafsi zilizoshiriki katika uzinduzi wa Wiki ya Vijana Kitaifa inayoendelea kufanyika mjini Babati mkoani Manyara.

Akizindua rasmi wiki ya maonesho hayo yanayoendelea mjini Babati leo tarehe 10 Oktoba, 2023, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenesta Mhagama kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa. Waziri Mhagama amesema, Taifa linawategemea sana vijana kwani ndiyo nguvu kazi ya leo na kesho.

“Shime vijana Serikali na jamii kwa ujumla inawategemea kuendelea kufanya kazi kwa bidii, hivyo Taifa linawaamini kama chachu ya kusukuma gurudumu la maendeleo, vilevile ili Taifa liendelee linahitaji vijana wanaochapa kazi kwa bidii na nidhamu ya hali ya juu kwa mstakabali wa maendeleo katika Taifa”, alisema Mhe. Mhagama.

Aidha, Mahakama Kuu Kanda ya Manyara imetumia jukwaa hilo kushiriki maonesho hayo ya Wiki ya Vijana kwa ajili ya kuonesha huduma na kutoa elimu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na mhimili huo wa utoaji haki nchini.

Kupita banda hilo wananchi wa Babati wamepata nafasi ya kujifunza juu ya masuala mbalimbali ya kimahakama ikiwa ni pamoja na masuala ya mtambuka ya Mirathi, Ndoa na Talaka, Mifumo ya Kielektroniki inayotumiwa na Mahakama katika kutoa huduma ya utoaji haki kwa wananchi na kuipongeza Mahakama kwa mafanikio ya kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara.

Wiki hii ya Vijana Kitaifa ambayo ilianza tarehe 08/10/2023 na kutarajiwa kuhitimishwa tarehe 14/10/2023 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kumbukizi ya miaka 24 ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere na Kilele cha Mbio za Mwenge yatakayoadhimishwa Kitaifa Babati Mkoani Manyara tarehe 14/10/2023.

Wananchi wa Babati wakiendelea kumiminika katika Banda la Mahakama Kuu Kanda ya Manyara kwa ajili ya kupata elimu na ushauri wa masuala ya Kisheria.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. Bernard Mpepo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi waliokuwa wakitoa Elimu katika Banda la Mahakama Kuu Kanda ya Manyara. Wenggine Afisa Utumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati Bi. Ntezirembo Yassin (kushoto) na Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Thobias Kavishe (kulia). 

  Msaidizi wa sheria Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara  Mhe. Thobias Kavishe  akizungumza na baadhi ya Wananchi waliotembelea banda la Mahakama Kuu Kanda ya Manyara. Wengine waliokati upande wa kushoto ni Afisa Utumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati Bi. Ntezirembo Yassin na (wa kwanza Kulia) ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Babati Mhe. Kandida Kalembo.

 h(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni