Jumanne, 10 Oktoba 2023

MAAFISA WA MAHAKAMA WAPIGWA MSASA KUHUSU UPELELEZI

Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro

Majaji, Mahakimu, waendesha mashtaka wa Serikali  na wapelelezi wameendelea kupigwa msasa wa masuala mazima ya upelelezi wa kesi.

Ni katika mafunzo yanayoendelea kutolewa kupitia Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na shirika lisilo la Kiserikali la pams foundation.

Akitoa somo leo tarehe 10 Oktoba, 2023 mwezeshaji Bw. Colman Lubisi Afisa Upelelezi toka Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU alisisitiza kuwa wanapotekeleza majukumu yao wafanye kwa kuzingatia taaruma inavyowataka.

Bw. Lubisi aliendelea kuelezea kuwa ni vyema shahidi akaandaliwa mapema ili kuhakikisha mshatakiwa anapatiwa haki yake kwakuwa kesi nyingi hasa za ujangili huondolewa mahakamani kutokana na kuwa ushahidi haujakamilika.

Akichangia mada wakati wa kipindi cha majadiliano, Jaji wa Mahakama Kuu Mhe. Dkt. Deo Nangela alisema kuwa ni muhimu kumuandaa shahidi mapema kabla ya kuingia naye mahakamani.

“Simaanishi umfundishe shahidi akaseme nini isipokuwa kama mwendesha mashtaka unatakiwa kujua shahidi anaenda kusema nini mahakamani na endepo ana kumbukumbu ya anachoenda kutolea ushahidi,” alifafanua Mhe. Nangela.

Kuhusu suala la usalama kwa mashahidi, Mhe. Nangela alishauri wapelelezi kutumia utambulisho wa mashahidi zaidi tofauti na kumleta shahidi mbele ya Mahakama kwa kuwa utambulisho huo utakuwa unafahamika kimahakama, hii ni katika mashauri ambayo shahidi anahofia usalama wa maisha yake.

Ikumbukwe kuwa mafunzo haya yamejikita katika mashauri ya makosa ya wanayamapori na maliasili ambayo yatatolewa hapa na yanatarajiwa kuhitimishwa mnamo tarehe 13 Oktoba,2023.

Lengo likiwa ni kuwajengea ujuzi na kubadilishana uzoefu kwakuwa washiriki toka maeneo mbalimbali wakiwemo Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu, Waendesha Mashataka na wapelelezi wamekutana pamoja.


Muwezeshaji wa mafunzo, Bw. Colman Lubisi, Afisa Mwandamizi wa Upelelezi toka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) akitoa somo kwa washiriki wa mafunzo (hawapo pichani).

Mwezeshaji (juu na chini) akiendelea kutoa mafunzo kwa washiriki.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt Deo Nangela akichangia mada wakati wa mafunzo.

Washiriki wa mafunzo wakifuatilia mada toka kwa muwezeshaji (hayupo pichani).

Darasa likiendelea.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania (kushoto) Mhe. Rose Ebrahim ambaye ni miongoni mwa washiriki wa mafunzo akifuatilia kwa makini.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa (wa kwanza kulia) pamoja na washiri wakifuatilia mafunzo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Iringa)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni