Jumanne, 3 Oktoba 2023

KAMATI YA UKAGUZI YA MAHAKAMA YAZINDULIWA

Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro 

Kamati ya Ukaguzi ya Mahakama ya Tanzania yazinduliwa rasmi na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba leo tarehe 2 Oktoba, 2023 katika ukumbi wa mkutano ulioko ndani ya Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC)Morogoro.

Uzinduzi huo uliombatana na ufunguaji wa mafunzo elekezi kwa wajumbe wa Kamati hiyo, pamoja na washiriki ambao ni wageni waalikwa, akizungumza wakati wa uzinduzi, Mhe. Chaba ambaye alitoa nasaha zake kwa washiriki wa kikao kwa kusema kuwa wayazingatie mafunzo hayo ambayo ni adhimu na muhimu kwa ustawi wa Mahakama ya Tanzania. 

Aidha Mhe. Chaba ameongeza kuwa Kamati hiyo itaiwezesha Taasisi hiyo kutekeleza malengo ya kimkakati kwa kuzingatia viwango vya juu katika kuleta tija na ufanisi utokanao na matumizi bora ya rasilimali watu na fedha ikiwemo kukupunguza kwa kiwango kikubwa hoja za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. 

“Nimetaarifiwa kwamba dhumuni kuu la mafunzo haya ni kuijengea uwezo Kamati ili iweze kuwa na ujuzi na weledi wa kutosha juu ya masuala mazima ya usimamizi wa viashiria hatarishi katika ngazi za mamlaka zilizo chini ya Mhimili wa Mahakama,” ameeleza Mhe. Chaba na kuongeza kuwa baada ya mafunzo hayo wataisaidia Mahakama kuepuka hasara zitokanazo na kushindwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika Utumishi wa Umma. 

Mhe. Chaba aliitaka Kamati hiyo kuwa na utaratibu wa kutoa taarifa kwa Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kulingana na matokeo ya ukaguzi katika vipindi husika ikiwa ni sambamba na kufanya upelelezi wa kina kuhusu shughuli zenye hisia kubwa ya udanganyifu katika mamlaka zilizoko chini ya Taasisi hiyo, huku akitolea mfano miradi ya ujenzi na ukarabati wa majengo na kutoa ushauri wa kitaalam. 

Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Pius Maneno ameeleza kuwa wajumbe  watakabidhiwa nyenzo ikiwemo flashi ambazo ndani yake kuna Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania, muongozo wa kamati, chata ya ukaguzi na kamati, kanuni za fedha za umma haya yakiwa ni maendeleo ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasilaino(TEHAMA) kwa Mahakama, ikiwa ni tofauti na miaka ya nyuma ambapo wajumbe hao wangekabidhiwa vitabu vikubwa vyenye nyenzo hizo. 

Kamati hiyo inategemewa kujinoa kwa siku tano kuanzia tarehe 2 hadi tarehe 6 Oktoba, 2023 ambayo tofauti na wajumbe kuna wageni waalikwa ambao ni Wakuu wa Idara mbalimbali ndani ya Mahakama ambao kwa pamoja watashiriki. 

  Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba akizungumza na wajumbe wa Kikao cha Kamati ya Ukaguzi ya Mahakama (hawapo pichani) wakati akizindua Kamati hiyo na kufungua mafunzo.

  Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Messe Chaba (kushoto) akimkabidhi mmoja wa wajumbe wa Kamati nyenzo ya kazi(flashi) katikati ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Pius Maneno.

Meza Kuu kutoka kushoto ni KaimuJaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Messe Chaba, kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya Mahakama ya Tanzania, Bw. Pius Maneno wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati hiyo.
Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi ya Mahakama wakifuatilia hotuba ya ufunguzi toka kwa mgeni rasmi Mhe. Messe Chaba (hayupo pichani).

Meza Kuu aliyekaa katikati  ni Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Messe Chaba, ikiwa katika picha ya pamoja na wageni waalikwa katika mafunzo hayo. 
Meza Kuu aliyekaa katikati  ni Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Messe Chaba, ikiwa katika picha ya pamoja na sekretarieti ya mafunzo ya kamati ya ukaguzi ya Mahakama.
Meza Kuu aliyekaa katikati  ni Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Messe Chaba, ikiwa katika picha ya pamoja na wenyeji ambao ni watumishi wa Mahakama Kanda ya Morogoro.
Sekretarieti ya mafunzo ya Kamati ya Ukaguzi ya Mahakama ya Tanzania wakiwa katika kutekeleza majukumu wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.

 Meza Kuu aliyekaa katikati  ni Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Messe Chaba, ikiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa mafunzo ya Kamati ya Ukaguzi ya Mahakama ya Tanzania.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni