Jumanne, 3 Oktoba 2023

MAJI YAKATIKA SHIMIWI IRINGA

  • Yapokonywa pointi kwa kuchezesha mamluki

Na Faustine Kapama-Mahakama, Iringa 

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) imeshinda rufaa yake kupinga ushindi ambao timu ya Maji iliupata katika mchezo wa mpira wa miguu kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika mkoani hapa.

Uamuzi huo umetolewa na Kamati ya Rufaa ya SHIMIWI baada ya Mahakama Sports kuthibitisha pasipo na shaka kuwa timu ya Maji ilichezesha mamluki, yaani watu wasio na sifa ya kushiriki mashindano hayo.

Kwa mujibu wa Kanuni SHIMIWI, wanaotakiwa kushiriki kwenye mashindano ni watumishi kutoka katika Wizara na Idara za Serikali pekee na siyo mtu mwingine yoyote.

Mchezo uliolalamikiwa ulichezwa katika uwanja wa Samora kuzikutanisha Mahakama Sports Mpira wa Miguu na Maji. Katika mchezo huo Maji walitoka kifua mbele kwa ushindi mwembamba wa gori 2:1 na ilipata ushindi huo kwa taaabu sana. 

Hata hivyo, baada ya mchezo huo, viongozi wa Mahakama Sports walifanya uchunguzi na kubaini mmoja katika timu ya Maji hakuwa mtumishi na hakustahiki kushiriki katika mashindano. 

Baada ya kubaini kasoro hiyo, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede aliiagiza Kamati ya Rufaa ya Mahakama inayoongozwa na Hakimu Mkazi Martin Mushi na Hakimu Mkazi Kennedy Chando pamoja na wanasheria nguli waliobobea katika fani hizo, kwa kushirikiana na Viongozi wengine wa Mahakama Sports, kuwasilisha rufaa katika mamlaka husika.

Viongozi wengine wa Mahakama Sports walioshirikiana na Kamati hiyo, ambayo ilikuwa na sababu moja inayohusu timu pinzani kuchezesha mamluki, ni Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende na Naibu Katibu Mkuu Theodosia Mwangoka.

Kamati ya Rufaa ya SHIMIWI ilisikiliza rufaa hiyo kwa pande zote mbili kupewa nafasi ya kusikilizwa. Katika utetezi wake, Maji waliwasilisha barua ya mkataba wa kibarua wa mchezaji aliyelalamikiwa pamoja na leseni ya uchezaji.

Baada ya kubanwa mbavu na wataalam wa Mahakama, Maji walishindwa kuwasilisha nyaraka zingine muhimu zinazomtambulisha mtumishi kama kadi ya bima ya afya, kitambulisho cha taifa, salary slip na kitambulisho cha kazi.

Baada ya kuzingatia uzito wa ushahidi uliotolewa, Kamati ya Rufaa ya SHIMIWI iliikubali rufaa iliyowasilishwa na Mahakama Sports na kuwatia hatiani Maji kwa kukiuka Kanuni za Shirikisho. Maji wamepokonywa pointi tatu na magori matatu kwa mujibu wa taratibu za michezo kufuatia ushindi walioupata kwenye mchezo huo.

Kufuatia uamuzi huo na kama Kamati ya Rufaa ya SHIMIWI itatoa ushindi kwa mrufani, timu ya Mahakama Sports itachumpa hadi kileleni mwa kundi A na kujihakikishia nafasi ya kutinga katika 16 bora.

Mahakama Sports inashiriki katika michezo mbalimbali mwaka huu, ikiwemo Kamba Wanaume na Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata, Tufe, Riadha na Baiskeli.

Katika mashindano ya SHIMIWI yaliyofanyika mwaka jana jijini Tanga, timu ya Mahakama ya Tanzania ilizoa makombe saba baada ya kuibuka washindi katika michezo mbalimbali.

Michezo ambayo Mahakama Sports ilipata medali na makombe ni Kamba Wanawake walioibuka mshindi wa kwanza, Riadha Wanawake mita 3,000 mshindi wa kwanza, Tufe Wanawake mshindi wa kwanza, Kamba Wanaume walioshika nafasi ya pili, Mpira wa Miguu Wanaume walioshika nafasi ya pili na Bao Wanaume mshindi wa tatu.

Hakimu Mkazi Martin Mushi, Gwiji la Sheria linaloongoza Kamati ya Rufaa ya Mahakama Sports.
Hakimu Mkazi Kennedy Chando, Gwiji jingine la Sheria. Utaumia ukikutana na sura hii kwenye masuala ya sheria. Waulize Uchukuzi SHIMIWI Tanga yaliyowakuta.
Sehemu ya Viongozi wa Mahakama Sports, wapo macho kuhakikisha haki inatendeka kwenye mashindano wakati wote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni