Na Faustine Kapama-Mahakama, Iringa
Timu ya Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) Mpira wa Miguu imechaguliwa kucheza mechi ya
ufunguzi wa Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI)
yanayofanyika mkoani hapa.
Taarifa hiyo njema
imetolewa na Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede katika kikao cha
wanamichezo wa Mahakama kuwa ufunguzi rasmi wa mashindano hayo utafanyika kesho
tarehe 4 Octoba, 2023 katika Uwanja wa Samora.
"Viongozi wa SHIMIWI
wameipendekeza timu yetu kucheza mechi ya ufunguzi rasmi wa mashindano haya.
Tutacheza na timu ya Kilimo majira ya mchana. Hii ni heshima kubwa kwetu na
sisi Viongozi tumeipokea kwa mikono miwili," amesema.
Mwenyekiti amefafanua
kuwa kuchaguliwa kwa Mahakama kucheza mechi hiyo kunatokana na nidhamu ya hali
ya juu waliyoionesha katika michezo iliyopita. Hivyo akahimiza wachezaji
kucheza kwa kuzingatia sheria zote ili watu wote watakaokuwa uwanjani waweze
kufurahia mechi hiyo.
"Kutakuwa na watu
wengi kwenye ufunguzi huu. Wanamichezo wote na watu wengine watakuwa
wanatutazama sisi. Tuilinde heshima hii kwa kucheza vizuri na kuendelea
kuonesha nidhamu...
“Viongozi wa SHIMIWI
wameshaliona hilo na wanatupongeza sana kwa kudumisha nidhamu siyo tu kwenye
kambi, lakini pia mahali pengine. Kadhalika, wametusifia kwa kuujulisha umma wa
Wanairinga na Tanzania nzima uwepo wa mashindano haya," amesema.
Hata hivyo, Dede
amewahimiza vijana wake kwenda kupambana kwenye mchezo huo ili kupata ushindi,
hatua itakayowawezesha kujiongezea pointi kwenye mashindano hayo.
Mahakama Sports inashiriki katika michezo mbalimbali mwaka huu,
ikiwemo Kamba Wanaume na Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao,
Karata, Tufe, Riadha na Baiskeli.
Katika mashindano ya SHIMIWI yaliyofanyika mwaka jana jijini
Tanga, timu ya Mahakama ya Tanzania ilizoa makombe saba baada ya kuibuka
washindi katika michezo mbalimbali.
Michezo ambayo Mahakama Sports ilipata medali na makombe ni Kamba
Wanawake walioibuka mshindi wa kwanza, Riadha Wanawake mita 3,000 mshindi wa
kwanza, Tufe Wanawake mshindi wa kwanza, Kamba Wanaume walioshika nafasi ya
pili, Mpira wa Miguu Wanaume walioshika nafasi ya pili na Bao Wanaume mshindi
wa tatu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni