·Yaitifua tifutifu Ardhi
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Iringa
Timu ya Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume imekamilisha kibabe michezo yake
katika kundi A kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za
Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika mkoani hapa.
Katika mchezo wake wa
mwisho, Mahakama Sports imeitifua Ardhi, hivyo kukwea kileleni mwa kundi hilo
lililoshirikisha timu zingine nne, ambazo zote zimepokea vichapo vikali.
Mchezo huo ambao
ulichezwa majira ya saa 12.30 asubuhi haukuwa na upinzani wowote kwani Ardhi waliingia
uwanjani wakiwa na hofu, hasa baada ya kuiona mibuyu ya Mahakama ambayo haikuwa
na utani na mtu.
Kabla ya mchezo kuanza,
mashabiki waliofurika uwanjani waliwaombea Ardhi msamahaha kwa Mahakama ili nao
wapate angalau hata pointi moja. Hata hivyo, waamuzi alipoamuru mchezo huo
kuanza, Mahakama haikuwa na utani na mtu.
Ardhi alichezea vichapo
vikali katika mivuto yote miwili, hivyo kuiwezesha Mahakama kuibuka kidedea na
kushika nafasi ya kwanza kwenye kundi hilo. Mahakama imeshinda mechi zake zote
katika kundi A. Mbali na Ardhi, timu nyingine zilizopokea vichapo ni Viwanda na
Biashara, Maji, RAS Kigoma na Kilimo.
Akizunguza baada ya
mchezo huo, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amewapongeza wanamichezo
wote kwa kuwezesha timu zote nne, yaani Kamba Wanaume, Kamba Wanawake, Netiboli
na Mpira wa Miguu, ambayo ina mechi moja mkononi, kwa kutinga hatua ya 16 bora.
"Kwa
sasa macho na nguvu yetu tunazielekeza kwenye hatua inayofuata. Tutahakikisha
tunapambana ili timu zetu zote zifanye vizuri kwenye michezo inayofuata.
Ninachoomba tuendeleze ushirikiano na kudumisha nidhamu wakati wote ili lengo
letu litimie,"amesema.
Mahakama Sports inashiriki katika michezo mbalimbali mwaka huu,
ikiwemo Kamba Wanaume na Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao,
Karata, Tufe, Riadha na Baiskeli.
Katika mashindano ya SHIMIWI yaliyofanyika mwaka jana jijini
Tanga, timu ya Mahakama ya Tanzania ilizoa makombe saba baada ya kuibuka
washindi katika michezo mbalimbali.
Michezo ambayo Mahakama Sports ilipata medali na makombe ni Kamba Wanawake walioibuka mshindi wa kwanza, Riadha Wanawake mita 3,000 mshindi wa kwanza, Tufe Wanawake mshindi wa kwanza, Kamba Wanaume walioshika nafasi ya pili, Mpira wa Miguu Wanaume walioshika nafasi ya pili na Bao Wanaume mshindi wa tatu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni