·Yagawa dozi ya vikapu 50 kwa 8
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Iringa
Timu ya Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) ya Netiboli imeendelea kuonyesha makali yake kwenye
Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI)
yanayofanyika mkoani hapa baada ya kuibugiza Ras Mtwara vikapu 50:8.
Matokeo hayo yanaifanya
Mahakama Sports kutinga katika hatua ya 16 bora baada ya kushika nafasi ya pili
kwenye kundi G lenye timu tano. Timu ya Mahakama imekamilisha michezo ya hatuà
ya makundi kwa kushinda michezo mitatu, huku ikipoteza mchezo mmoja kwa taaabu
sana.
Katika mchezo huo, Ardhi
walionufaika na upendeleo wa mwamuzi walishinda kwa ushindi mwembambna wa vikapu
23:21. Mchezo wa mwisho uliofanyika jana tarehe 2 Octoba, 2023 kwenye viwanja
vya Chuo Kikuu cha Kikristo Ruaha dhidi ya Ras Mtwara ulichezwa majira ya saa
11:00 jioni.
Katika mchezo huo,
Mahakama Sports ililisakama mara kwa mara lango la wapinzani na tupia tupia za
hapa na pale, zikiongozwa na Tatu Mawazo na Philomena Haule, ziliihakikishi
timu hiyo kuondoka na ushindi.
Hadi timu zote mbili
zinaenda kwenye mapumziko, Mahakama Sports ilikuwa inaongoza kwa vikapu 22 kwa
5. Katika kipindi cha pili, Mahakama Sports waliendelea kukaza uzi na kumiliki
mpira kwa kiasi kikubwa, hatua iliyowawezesha kwenda kwenye lango la wapinzani
mara wa mara.
Kasi ya utupiaji vikapu
iliongezeka katika kipindi hicho na kuwezesha Mahakama Sports kutumbukiza vikapu
28, huku Ras Mtwara wakiambulia vikapu 3 pekee. Hadi mwamuzi anapuliza kipenga
kumaliza mchezo huo, Mahakama Sports ilikuwa imejizolea vikapu 50 kwa 8
walivyopata Ras Mtwara.
Akizungumza baada ya
mchezo huo, Mwalimu wa Timu Paul Mathias amesema hatua waliyofikia ni nzuri
kwani wameshajihakikishia kufika katika hatua ya 16 bora. Aliwaomba vijana wake
kuendelea kupambana katika hatua inayofuata ili kusonga mbele katika
mashindano.
Naye Katibu wa Mahakama
Sports Robert Tende amesema wameshakamilisha lengo la awali la kuvuka katika
hatua ya 16 bora, hivyo nguvu kubwa kwa sasa wanaielekeza kwenye hatua
inayofuata na anaamini vijana wake wataendeleza vipigo hadi kunyakua kombe.
Wachezaji wanaoiwakilisha
Mahakama katika mchezo huo ni ni Tatu Mawazo, Filomena Haule, Upendo Gustaf,
Nyangi Kisangeta, Veronica Rajab, Eunice Chengo na Sophia Songoro.
Waliokuwa kwenye mbao ndefu ni Nuru Nchimbi, Shani Ally, Rhoida Makassi, Malkia
Nondo na Agnes Joseph.
Mahakama Sports inashiriki katika michezo mbalimbali mwaka huu,
ikiwemo Kamba Wanaume na Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao,
Karata, Tufe, Riadha na Baiskeli.
Katika mashindano ya SHIMIWI yaliyofanyika mwaka jana jijini
Tanga, timu ya Mahakama ya Tanzania ilizoa makombe saba baada ya kuibuka
washindi katika michezo mbalimbali.
Michezo ambayo Mahakama Sports ilipata medali na makombe ni Kamba
Wanawake walioibuka mshindi wa kwanza, Riadha Wanawake mita 3,000 mshindi wa
kwanza, Tufe Wanawake mshindi wa kwanza, Kamba Wanaume walioshika nafasi ya
pili, Mpira wa Miguu Wanaume walioshika nafasi ya pili na Bao Wanaume mshindi
wa tatu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni