Jumatatu, 2 Oktoba 2023

MAHAKAMA SPORTS MPIRA WA MIGUU YAIPIGA VIWANDA NA BIASHARA WIKI

Na Faustine Kapama-Mahakama, Iringa 

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Mpira wa Miguu imekwea kileleni katika kundi A kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayoendelea mkoani hapa baada ya kuikandamiza Viwanda na Biashara magori 7:0 katika mchezo uliojaa ufundi wa kila aina.

Iliwachukua dakika saba tu ya mchezo kwa vijana wa Mhimili wa utoaji haki nchini kupachika bao safi kupitia kwa kiungo bamia Frank Obadia baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Seif Shamte na kuiandikia timu yake bao la kwanza.

Baada ya kwenda kambani, Mahakama Sports iliendelea kulisakama lango la wapinzani na kufanikiwa kupata bao la pili katika dakika ya saba ya mchezo kupitia kwa huyo huyo Frank Obadia baada ya kupokea pasi murua kutoka kwa Seif Shamte kwa mara nyingine.

Kosa kosa za kupachika mabao ziliendelea na ilipofika dakika ya 11 ya mchezo, kiungo hatari aliyeonekana kuwa nyota wa mchezo huo, Selemani Magawa aliachia shuti kali na kujaa wavuni, hivyo kuiandikia timu yake bao la tatu.

Mahakama Sports hawakuishia hapo, kwani walizidisha mashambulizi na ilipofika dakika ya 24 ya mchezo, mshambuliaji hatari Martin Mpanduzi alipokea pasi safi kutoka kwa beki kisiki Nasoro Mwampamba na kuachia shuti lililomshinda mlinda mlango wa Viwanda na Biashara na kujaa kwenye nyavu.

Baada ya kuingia kwa bao hilo, timu ya Viwanda na Biashara ilionekana kuingia kwenye mfumo wa Mahakama Sports na kuchezewa nusu uwanja muda wote. Katika dakika ya 28 ya mchezo, kiungo Seleman Magawa alipachika bao la tano baada ya kupokea pasi kutoka kwa kiungo mwenzake Obadia, ambaye alikuwa mwiba kwa timu pinzani.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Mahakama Sports ilienda kwenye mapumziko ikiwa na magori matano kibindoni. Kipindi cha pili kilitawaliwa na kosa kosa nyingi kwa Mahakama Sports kutokana na upepo mkali uliokuwa unavuma kwenda lango la Kaskazini la Viwanda na Biashara.

Hata hivyo, baada ya kutulia na kuanza kutandaza kandanda safi la kitabuni, dakika ya 47 ya mchezo Nahodha wa Timu aliyeingia kutokea benchi, Devis Munubi alipachika bao na kuipatia timu yake bao la sita.

Baada ya kosa kosa nyingi za hapa na pale, Nahodha Msaidizi Seleman Magawa aliachia shuti kali katika dakika ya 59 ya mchezo na kuweka mpira kwenye kamba, hivyo kuiandikia timu yake bao la saba na la ushindi mnono.

Kuingia kwa bao hilo kulimfanya kiungo huyo tegemezi kuondoka na mpira baada ya kupachika kwenye nyavu jumla ya mabao matatu katika mchezo huo. Hii ni mara ya pili kwa timu ya Mahakama kuondoka na mpita. Mara ya kwanza, mshambuliaji Mpanduji alifunga bao tatu katika kipute kilichopigwa na timu ya Ras Kigoma, ambayo iliogelea jumla ya magori nane kwa nunge.

Matokeo hayo yanaiweka Mahakama Sports katika nafasi nzuri ya kutinga 16 bora baada ya kuzoa pointi tisa ambazo imejikusanyia kufuatia kushinda mechi mbili kwa idadi kubwa ya magori na kupata pointi nyingine tatu baada ya timu ya Maji kupokonywa ushindi walioupata kwa taaabu baada ya kuchezesha mamluki.

Mwalimu wa Timu Spear Mbwembwe amewapongeza vijana wake kwa kucheza vizuri na kumiliki mpira muda wote wa mchezo, hivyo kuwafanya timu pinzani wasipate nafasi yoyote ya kutengeneza mabao.

“Ninawashukuru sana, mmecheza vizuri. Sasa tujipange kwa mechi ya mwisho ili tuendeleze ushindi, hatutaki kupoteza mechi hata moja. Ninawaamini, mtafanya vizuri, kazi iendelee,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amesema hakuna kurudi nyuma mpaka kieleweke. “Hatujamaliza, kazi iendelee. Mwaka huu watatuelewa tu, wakichezesha mamluki tutapambana nao, tunataka mchezo wa haki na haki lazima itawale mashindano haya. Safari hii hatutakubali Bundi azengee mashindano,” amesema.

Wachezaji walioiwakilisha Mahakama ni Micheal Turuka, Nasoro Mwampamba, Akida Mzee, Kelvin Muhagama, Frank Obadia, Gabriel Mwita, Martin Mpanduzi na Seleman Magawa, Abdi Sasamalo, Mbura Minja, Iman Zumbwe, Rashid Hamis, Devis Munubi na Gisbert Chentro.

Wengine walikuwa Seif Shamte, Nkuruma Katagira, Emmanuel Mwamole Fahamu Kibona na Ramadhani Seif. Benchi la ufundi liliongozwa na Kocha Mkuu Spear Mbwembe na Kocha Msaidizi Said Albea, Timu Meneja Shaibu Kanyachole, Meneja wa Vifaa Eliya Ngule na Daktari Janeth Mapunda.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa kuhusu mashindano haya, timu ya Mahakama Mpira wa Miguu imepangwa kundi A na itachuana na Viwanda na Biashara, Maji, RAS Kigoma na Kilimo katika kutafuta nafasi ya kutinga 16 bora.

Mahakama Sports inashiriki katika michezo mbalimbali mwaka huu, ikiwemo Kamba Wanaume na Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata, Tufe, Riadha na Baiskeli.

Katika mashindano ya SHIMIWI yaliyofanyika mwaka jana jijini Tanga, timu ya Mahakama ya Tanzania ilizoa makombe saba baada ya kuibuka washindi katika michezo mbalimbali.

Michezo ambayo Mahakama Sports ilipata medali na makombe ni Kamba Wanawake walioibuka mshindi wa kwanza, Riadha Wanawake mita 3,000 mshindi wa kwanza, Tufe Wanawake mshindi wa kwanza, Kamba Wanaume walioshika nafasi ya pili, Mpira wa Miguu Wanaume walioshika nafasi ya pili na Bao Wanaume mshindi wa tatu.

Hii hapa miamba kutoka Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Mpira wa Miguu iliyotoa kipigo cha magori saba kwa karai.
Nahodha Msaidizi wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Mpira wa Miguu Seleman Magawa (juu) akipokea mpira kutoka kwa mwamuzi baada ya kupachika mabao matatu kwenye mchezo na timu ya Viwanda na Biashara (chini)

Manahodha wa timu zote mbili wakiwa katika picha ya pamoja na waamuzi kabla ya mchezo.
Kipa wa Viwanda na Biashara akilamba nyasi baada ya kukubali kipigo.
Wachezaji wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Mpira wa Miguu (juu na chini) wakimiriki mpira.

Wachezaji wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Mpira wa Miguu wakilisakama lango la wapinzani.
Mwamuzi wa pembeni akinyoosha kibendera kuonyesha mchezaji ameotea.
Mashabiki wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Mpira wa Miguu wakishangilia kwa nguvu wakati kipute kinaendelea.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni