Na. Innocent Kansha – Mahakama, Lushoto
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewakumbusha Majaji wa Mahakama
ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania walioapishwa Septemba 14, 2023, kuwa
wananchi watapima uwezo wao kwa kutenda haki na siyo vyeo walivyotunukiwa.
Akizungumza
katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo elekezi ya Majaji hao 24, ikiwemo wanne (4)
wa Mahakama Rufani na 20 wa Mahakama Kuu , leo tarehe 2 Oktoba, 2023 katika
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto mkoani Tanga ambapo mafuzo hayo yatafanyika
kwa muda wa wiki tatu, Jaji Mkuu Mhe. Prof. Juma amesema, mwananchi hatajali
Jaji husika ana uwezo gani wa elimu ama ana utaalam wa kiwango gani isipokuwa
uwezo wako utapimwa kwa kiasi gani utaweza kutatua changamoto zao
zinazowakabili wanapotafuta haki.
“Baadhi
yenu mmesoma sana wengine shahada za uzamili, shahada za uzamivu kwa mwananchi
anayetafuta haki hataangalia hizo shahada, yeye atafika kutafuta huduma tu,
haangalii kama wewe ulikuwa ni profesa wa sheria, una udaktari wa sheria, haangalii kama kwenye hukumu yako utaandika we ni daktari au nani, yeye anachotaka
tu ni hukumu inapotoka aisome aone kama inampa haki ili afanye uamuzi unaofuata”,
amesema Jaji Mkuu.
Mhe.
Prof. Juma amesema, uwezo wa Jaji utapimwa kwa kiasi gani amejifunza katika
mafunzo hayo elekezi, na namna gani atakavyokuwa anajitayarisha kila siku
kusikiliza shauri lililo mbele yake, uwezo wa utoaji wa huduma wa Jaji utapimwa
kila siku utakapokuwa unaingia mahakamani na kwa kila jalada utakalo kabidhiwa
litatumika kukupima. Vilevile hata makarani utakaofanya nao kazi watakupima
wakiona unaanza kulegalega huo ndiyo utakuwa ubuyu utakaokuwa unazungumzwa kwenye
mabaraza na vijiweni
Mhe.
Prof. Juma amewaambia Majaji hao kuwa wajitayarishe kufundiswa kazi na makarani,
wao wote walifundishwa kazi na makarani hata maafisa wa jeshi wanafundishwa na
wanajeshi wenye vyeo vya kawaida, sasa wale watu wa chini ndiyo wanafahamu
taratibu zote za kila siku za mahakamani kuna mambo mengi sana mtajifunza
kutoka kwao.
Kuhusu
matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Jaji Mkuu amesema,
maboresho mengi ya muda mrefu hasa katika matumizi ya tehama. Mahakama inatumia
sana mifumo ya tehama kuwajibishana, kupima utendaji na kuangalia kila hatua
zinazofanywa na Maafisa wa Mahakama.
“Mimi
siku zote huwa nawambia Majaji wapya kwamba, hakuna shimo unaloweza kijificha
unapofanya kazi za kimahakama kwa sababu mifumo ya mtandao inaangalia mzigo
wako wa mashauri kila siku, kama unaweka mashauri ya mlundikano utajulikana,
kama wewe Jaji kazi yako ni kuhairisha mashauri utajulikana, kama wewe ni Jaji
unayemaliza kusikiliza mashauri na husomi hukumu au unasoma hukumu hutoi nakala
utajulikana na utafuatiliwa na ndiyo maana katika salamu zetu za Mahakama
tunatumia sana uadilifu, weledi na uwajibikaji kwa sababu mfumo wetu mzima
unahakikisha uwajibikaji”, amesisitiza Mhe. Prof. Juma.
Jaji
Mkuu amesema, mfumo mpya wa kieletroniki wa kusajili, kusimamia na kuratibu
mashauri ‘Advanced Case Management’ utaanza kufanyiwa majaribio leo tarehe 2 Oktoba,
2023 kwa kipindi cha mwezi mzima na utaziduliwa tarehe 1 novemba, 2023. Hivyo
Mahakama inahama kutoka katika mfumo iliyokuwa ikiutumia kwa miaka kadhaa na
kuanza kutumia mfumo wa kieletroniki wa kusajili na kusimamia mashauri ikiwa ni
mfumo mama utakao tumika kuwafuatilia Maafisa wa Mahakama.
“Mfumo
huu unatusaidia sisi kuhakikisha kwamba haki ambayo Katiba imewaahidi wananchi
inapatikana ndani ya wakati, zama za matumizi ya majalada magumu, zama za
majalada kupotea, zama za hukumu ambayo inasomwa lakini lakala hazipatikani itaisha
kuanzia mfumo huu utakapo anza kufanya kazi”, ameongeza Jaji Mkuu
Kuhusu
Maadili, Mhe. Prof. Juma amesema, ukisoma Kanuni za Maadili za Maafisa wa
Mahakama ‘Code of Conduct for Judicial Officers’ zinasisitiza uwezo na ujuzi,
kanuni hizo zinasema kwamba, uwezo ambao umewawezesha kuteuliwa kuwa Majaji au
kuaminiwa kuwa Majaji wa Rufani na Majaji wa Mahakama Kuu, kanuni zinabainisha
dkuendelea kuwa na uwezo huo huo bila kupungua.
“Kwa
sababu uwezo ukipungua kanuni zinasema ni kigezo cha kuwaondoa kutoka katika
kazi ya ujaji, kanuni hizo zimetamka kwamba hasa kanuni ya nne inaelekeza uwezo
na umakini ‘Competence & Diligence’ uwezo mlionao mnapaswa kuendeleza”,
amewambia Majaji hao.
Awali,
Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Mhe
Paul Kihwelo amesema, mafunzo kama hayo yanayoanza kutolewa kwa Majaji hao ni
ya kundi la nane (8) na kwa upande wa Mahakama ya Rufani hilo ni kundi la nne
(4) yakitolewa katika nyakati tofauti mara tu Mhe. Rais anapoteua kuwaapisha Majaji
wapya toka kuanzia mwaka 2014 hadi sasa.
“Mhe.
Jaji Mkuu ninaomba nikuhakikishie wewe binafsi pamoja na washiriki kwamba kama
Chuo kwa kutumia uzoefu wa mafunzo yaliyotangulia tumejipanga vizuri uchaguzi
wa wakufunzi pamoja na mada zitakazo tolewa zitakidhi kiu ya washiriki pamoja
na kutimiza lengo la Mahakama na la Taifa, siku zote tunaamini Mahakama mafunzo
yanatakiwa kujibu changamoto zilizopo na za baadaye”, amesema Jaji Kihwelo.
Mhe.
Kihwelo amesema, mafunzo hayo yanalenga kuwajenga Wahe. Majaji kwa ajili ya Mahakama
ya leo na Mahakama ya kesho. Mafunzo kwa yatakayo tolewa kwa washiriki wa
Mahakama Kuu yatajumisha jumla ya mada 38 na wawezeshaji 41 watashiriki zoezi
hilo kwa muda wa wiki tatu (3). Kwa upande wa washriki wa Mahakama ya Rufani
kutatolewa mada tisa (9) na wawezeshaji sita (6) kwa muda wa wiki moja.
“Siku
zote mafunzo ya Mahakama yanajikita katika maeneo matatu yaani mtazamo ama
huluka, ujuzi na maarifa ‘ASK Attitude, Skills and knowledge’ ndiyo lengo la
wawezeshaji wote waliopo na watakao kuja watagusa maeneo hayo”, amesema Jaji Kihwelo.
Naye,
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani akitoa
neno la shukrani, amemshukuru Jaji Mkuu kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na
kufungua mafunzo hayo elekezi kwa Majaji hao.
“Mafunzo
haya ya awamu hii ni ya kwanza na ya aina ya kipekee kwani kwa mara ya kwanza yamewajumuisha
kwa pamoja Majaji wote wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu.”, amesema Mhe. Siyani.
Mhe.
Siyani amesema mafunzo hayo yanaakisi sera ya mafunzo ya Mahakama na mpango wa
utekelezaji wake na hivyo kuwa utamaduni kwa Chuo na Uongozi wa Mahakama kutoa
mafunzo elekezi kwa watumishi wa kada mbalimbali ikiwemo Majaji wa ngazi zote.
“”Bila
shaka uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani ni imani kubwa
ambayo mamlaka ya uteuzi imeweka kwenu kwa niaba ya watanzania wapatao
takribani milioni 61”, ameongeza Jaji Kiongozi.
Mhe.
Siyani akatoa maelekezo kwa Majaji wa Mahakama kuu walioanza mafunzo elekezi
mwaka 2021 jumla ya Majaji 21 walipatiwa mafunzo na wakapewa nafasi ya mafunzo
kwa vitendo ambapo walipangiwa jumla ya mashauri 342 kati ya hayo mashauri 309
yalimalizika na ikumbukwe kuwa yale sio majaribio ya haki za watu, mtapaswa
kwenda kutoa haki. Kiwango cha umalizaji mashauri kwa kwa mwaka huo ilikuwa
asilimia 90.3 ufanisi huo ulitokana na kujengewa uwezo wa mafunzo kutokea
Lushoto.
Mhe.
Siyani ameongeza kuwa, mwaka 2022 kulikuwa na Majaji 22 wa Mahakama Kuu
walioshiriki mafunzo elekezi na jumla ya mashauri 430 yalipangwa kwa Majaji hao
na mashauri 402 sawa na asilimia 93 yalimalizika na asilimia 79 ya maamuzi hayo
yalipandishwa kwenye Mfumo wa kielektroniki wa TanzLII
“Mwaka
huu 2023 tumeandaa wastani wa mashauri mengine 400 yanayowasubiri Majaji wa
Mahakama Kuu mara watakapo maliza mafunzo elekezi tuasubiri kuona kama
mafanikio yaliyofikiwa na makundi yaliyopita yataendelezwa na Kundi hili lakini
ni vema mkatambua baada ya kujengewa uwezo kuna matarajio ya matokeo makubwa
mtakwenda kwenye vituo mtakavyopangiwa mkiwa mnakimbia kama askari wapya wenye
nguvu”, amesisitiza Jaji Kiongozi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni