· Mahakama Sports yawachapa mbili kwa karai
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Iringa
Timu ya Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) Mpira wa Miguu leo tarehe Octoba, 2023 imeikung’uta
Ardhi mabao 2:0 na kutinga robo fainali kwenye Mashindano ya Shirikisho la
Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika mkoani hapa.
Ardhi waliokuwa wanang’ang’ania
kucheza na Mahakama Sports licha ya kuondolewa kwenye mashindano kwa kuchezesha
mamluki imekiona cha mtema kuni baada ya kufungashiwa vilago kwenye mashindano hayo
baada ya kupokea kichapo hicho.
Awali, Mahakama Sports
ilikuwa icheze kabumbu hilo na TARURA jana tarehe 6 Octoba, 2023, lakini
mtanange huo uliahirishwa kutokana na fujo zilizoletwa na Ardhi na kukataa
kutoka uwanjani, huku Viongozi wao wakidai hawakuwa na barua kutoka SHIMIWI
inayowatoa kwenye mashindano.
Kabumbu la leo
lililochezwa majira ya saa 2:00 asubuhi kwenye Viwanja vya Mkwawa lilianza kwa timu
zote kushambuliana kwa zamu, huku Mahakama Sports ikilisakama lango la
wapinzani mara kwa mara.
Iliwachukua dakika ya
kwanza ya mchezo Mahakama Sports kuukwamisha mpira kwenye nyavu kupitia kwa
mshambuliaji wake hatari Martin Mpanduzi. Hata hivyo, mshika kibendera namba mbili
alilikataa bao hilo kwa madai ya mfungaji kuwa aliotea, kitendo kilichozua zomea
zomea kwa mashabiki kwa kukataa bao hilo halali.
Kukataliwa kwa bao hilo
kuliwaamsha Mahakama Sports na kuzidisha mashambulizi. Katika dakika ya 11, beki
wa kushoto Gisbert Chentro aliachia shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Ardhi
na kujaa kwenye wavu, hivyo kuiandikia timu yake bao la kwanza.
Baada ya kuingia kwa bao
hilo, Ardhi walionekana kuzidiwa hasa katika eneo la katikati, huku vijana wa
Mahakama Sports wakisakata kandanda safi na kuutawala mchezo. Ilipofika katika
dakika ya 24, Mpanduzi aliwatoka walinzi wa Ardhi na kupachika bao la pili na
la ushindi kwa timu yake.
Hadi timu zinaenda kwenye
mapumziko, Mahakama Sports ilikuwa mbele kwa mabao 2:0. Katika kipindi cha
pili, timu zote zilikuwa zinashambulia kwa kuviziana, lakini mabeki walikaa
imara hadi mwisho wa mchezo hakuna timu iliyoweza kuliona lango la mwenzake.
Akizungumza baada ya mchezo
huo kukamilika, Mwalimu Spear Mbwembe amewapongeza vijana wake kwa kucheza kwa
tahadhari kubwa na kupata matokeo kwa kuzingatia ubora wa timu pinzani.
“Hawa jamaa (Ardhi) ni
wazuri sana, lakini nashukuru vijana wangu wamezingatia maelekezo yangu na kuweza
kuwadhibiti. Mchezo huu waliouonesha, itafungwa timu yoyote itakayokuja mbele
yetu,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa
Mahakama Sports Wilson Dede amesema anauhakika timu yake itachukua kombe mwaka
huu kutokana na ubora wa vijana alionao na hakuna yeyote atakayewazuia kwenye
hatua zinazofuata.
“Hawa Ardhi ni wazuri
sana. Ingawa kulikuwepo na mkanganyiko namna walivyorudishwa kwenye mashindano,
sisi tulikubali kupambana nao na bahati nzuri wamekiona cha moto. Sasa
tunaangalia mbele na tutaendelea kupambana hadi ushindi upatikane,” amesema.
Wachezaji wa Mahakama
Sports waliosakata kambumbu ni Fahamu Kibona, Nasoro Mwampamba, Gisbert Chentro,
Rashid Mbwana, Akida Mzee, Kelvin Muhagama, Frank Obadia, Seleman Magawa,
Martin Mpanduzi, Seif Shamte na Abdi Sasamaro.
Walioanzia kuchoma
mahindi ni Michael Turuka, Emmanuel Mwamole, Juma Mbega, Davis Munubi, Timoth
Mwakisamba, Gabriel Tabana na Ramadhan Seif. Benchi la ufundi liliongozwa na
Kocha Mkuu Spear Mbwembe na Kocha Msaidizi Said Albea.
Alikuwepo pia Timu Meneja
Shaibu Kanyachole, Meneja wa Vifaa Eliya Ngule na Daktari Janeth Mapunda.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni