Na. Stephen Kapiga-Mahakama Mwanza.
Mahakama
zilizopo katika jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kanda ya Mwanza,
leo tarehe 6 Oktoba, 2023, zimehitimisha wiki ya Huduma kwa Mteja kwa kukutana
na wateja wote Mahakama kwa lengo la kuwaeleza kwa kina shughuli mbalimbali
zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania ikiwemo Mkataba wa Huduma kwa Mteja.
Akizungumza
na wateja pamoja na watumishi wanaofanya kazi katika Mahakama za kituo Jumuishi
cha Utoaji Haki jijini Mwanza, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Mwanza Mhe. Chiganga Tengwa amewashukuru watumishi kwa kutoa huduma nzuri kwa
wateja kwa kipindi cha wiki zima ya kuadhimisha shughuli hiyo, akawataka
kuendelea na ari hiyo ya kutoa huduma bora kwa wateja wote wafikiao katika kituo
hicho kupata huduma za kimahakama.
“Ninawashukuru
kwa namna ambavyo kwa wiki nzima hii mmependeza na kuwa wachangamfu kwa wateja
wetu na kila mmoja amekuwa ni mwenye tabasamu iliyo wavutia wateja na kufurahia
huduma kwa kwa wiki hii. Niwasihi tuendelee na moyo huu hata mara baada ya
kumalizika kwa zoezi la huduma kwa mteja”. Alisema Mhe.Chinganga Tengwa.
Kwa
upande wake Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza Bw. Tutubi
Mangazini amesema kuwa, Mahakama inathamini mchango wa wateja wote kwa kuwa
wawazi hasa pale kulipotekea kutoelewana kimaelekezo na baadhi ya watumishi
waliowapatia huduma na kuwasihi kuwa wasisite kutumia mifumo iliyopo Mahakamani
na kufikisha malalamiko yao.
“Ndugu
zangu, nikiwa kama Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza jukumu langu kubwa
ni kusimamia maswala ya kiutawala na utendaji wa shughuli za watumishi za kila
siku ikiwa ni pamoja na kuwawezesha watumishi hawa waliopendeza kuweza
kuwahudumia nyinyi vizuri, na yule ambaye atakengeuka kumuwajibisha kulingana
na taratibu za kiutumishi. na Naibu Msajili yeye anashughulikia maswala yote ya
mashauri yanayohusu Mahakama Kuu”. amesema Bw. Mangazini.
Kwa
upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza Mhe.
Monica Ndyekobora amesema, mkataba wa
huduma kwa wateja uliopo mahakamani ni kwa ajili ya kusaidia kuainisha wajibu
wa watumishi wa Mahakama kwa wateja na pia kuelezea juu ya wajibu wa mteja kwa
Mahakama anapofika kutafuta huduma.
“Lengo
la mkataba huu ni kuwafahamisha nyinyi wateja huduma zilipo Mahakamani na
viwango vya huduma tunazopaswa kuwapatia na utaraibu mnaopaswa kuufuata endapo
utaona hujapaitiwa huduma inayoridhisha. Hivyo ni vizuri kama mteja ukatambua
wajibu wako pindi unapokuja kupata huduma, mkataba huu unapatika katika tovuti
ya TanzLII hivyo kila mmoja anaweza kuupata na kuusoma”. Alisema Mhe Monica Ndyekobora.
Katika
siku ya kuhitimisha wiki ya huduma kwa wateja, wateja walielimishwa juu ya
mifumo yote inayotumika mahakamani ikiwemo mfumo wa kieletroniki wa kusajili,
kusimamia na kuratibu mashauri, mfumo wa kuendesha mashauri kwa njia ya video
(Video Conference), Mfumo wa kupandisha maamuzi mtandaoni (TanzLII), mfumo wa
malipo ya Serikali, mfumo wa kupokea na kushughulika malalamiko, mfumo wa
ramani ilipo Mahakama(JMAP) na mifumo mingine ambata.
Juma
la huduma kwa mteja lilianza siku ya juamatatu ya tarehe 2 Oktoba, 2023 na kuhitimishwa
rasmi leo tarehe 6 Oktoba, 2023 kwa watumishi wote kukutana na wateja na
kuelezea shughuli na majukumu mbalimbali ya Mahakama ya Tanzania ya kila jambo
ambalo liliwafurahisha wateja.
Naibu Msajili
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza Mhe. Chiganga Tengwa (aliyesimama mbele) akiwashukuru wateja pamoja na watumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Mwanza kwa kuhitimisha salama wiki ya huduma kwa mteja leo tarehe 6 Oktoba, 2023 walipokutana katika kituo hicho.
Mtendaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza Bw. Tutubi Mangazini (aliyesimama mbele) akifafanua jambo kwa wateja na watumishi wa Mahakama waliofika mahakamani katika kilele cha wiki ya
huduma kwa mteja.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, Mhe. Monica Ndyekobora akilelezea juu ya Mkataba wa huduma kwa wateja katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya huduma kwa mteja.
Mteja wa Mahakama wakiwasilisha maoni yake na kutoa shukrani zake kwa Mahakama baada ya kupata elimu katika kilele cha
maadhimisho ya wiki ya huduma kwa mteja.
Sehemu ya
watumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Mwanza wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kwa elimu ya hitimisho ya wiki ya huduma
kwa mteja
Picha ya pamoja kati ya watumishi wa Mahakama Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Mwanza
wakiwa Pamoja na wateja waliofika mahakamani siku ya kilele cha huduma kwa mteja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni