·Yaisasambua kwa vikapu 52 kwa 16
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Iringa
Timu ya Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) Netiboli leo tarehe 6 Octoba, 2023 imeisasambua
Sheria kwa vikapu 52 kwa 16 na kufanikiwa kutinga robo fainali kwenye
Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI)
yanayofanyika mkoani hapa.
Mchezo huo uliofanyika kwenye
viwanja vya Chuo Kikuu cha Kikristo Ruaha majira ya saa 4.00 asubuhi ulianza
kwa Sheria kudhibiti mpira na kutangulia kutupia vikapu viwili vya haraka
haraka katika dakika za mwanzo.
Hata hivyo, Mahakama
Sports ilitulia na kuanza kutupa pasi mpenyezo zilizowachanganya wapinzani wao
na kuanza kulisakama mara kwa mara lango la Sheria.
Baada ya kujibu
mashambulizi, tupia tupia za hapa na pale zilizokuwa zinaongozwa na Tatu Mawazo
na Philomena Haule ziliihakikishi timu hiyo kuondoka na ushindi. Hadi timu zote
mbili zinaenda kwenye mapumziko, Mahakama Sports ilikuwa inaongoza kwa vikapu 27
kwa 8.
Katika kipindi cha pili,
Mahakama Sports waliendelea kulishambulia lango la wapinzani, huku wakitoa pasi
za kuelewana, hatua iliyowawezesha kwenda kwenye lango la wapinzani mara wa
mara.
Kasi ya utupiaji vikapu
iliongezeka katika kipindi hicho na kuwezesha Mahakama Sports kutumbukiza
vikapu 25, huku Sheria wakiambulia vikapu 8 pekee. Hadi mwamuzi anapuliza
kipenga kumaliza mchezo huo, Mahakama Sports ilikuwa imejizolea vikapu 52 kwa 16
walivyotupia Sheria.
Akizungumza baada ya
mchezo huo kumalizika, Mwalimu wa Timu Paul Mathias amesema ameridhishwa na juhudi
zinazofanywa na wachezaji wake na anauhakika wataendeleza wimbi la ushindi
katika hatua inayofuata.
“Tunaingia kwenye hatua muhimu
katika mashindano. Kwetu sisi hatuna kitu kingine zaidi ya ushindi kwa kila
mechi itakayokuja mbele yetu. Yoyote atakayejipendekeza tutashughulika naye,
ninachowaomba vijana wangu waendelee kujituma na kucheza kwa ushirikiano,” amesema.
Naye Katibu wa Mahakama
Sports Robert Tende amesema hatua waliyofikia ya robo fainali ni nzuri kuelekea
kutwaa kombe. “Safari hii tunakwenda kufanya maajabu, hawataamini kitakachowakuta.
Uzuri ni kwamba timu yetu inabadilika kiuchezaji kulingana na mpinzani. Kwa
hiyo, yoyote atakayekuja atapigwa,” amesema.
Wachezaji walioiwakilisha
Mahakama katika mchezo huo ni ni Tatu Mawazo, Filomena Haule, Upendo Gustaf,
Nyangi Kisangeta, Eunice Chengo, Sophia Songoro, Shan Ally na Agness Mwanyika.
Waliokuwa kwenye mbao ndefu
ni Nuru Nchimbi, Malkia Nondo, Talita Kayuli na Ruth Kibona, huku benchi la
ufundi likiongozwa na Mwalimu Paul Mathias na Naibu Katibu Mkuu wa Mahakama
Sports Theodosia Mwangoka.
Katika hatua nyingine,
kabumbu lililokuwa lichezwe leo tarehe 6 Octoba, 2023 katika uwanja wa Mkwawa
kuwakutanisha Mahakama Sports Mpira wa Miguu na TARURA limeahirishwa kutokana
fujo za wachezaji wa timu ya Ardhi ambayo imeondolewa kwenye mashindano kwa
kuchezesha mamluki.
Mechi hiyo ambayo ilikuwa
imepangwa kuchezwa majira ya saa 2:00 asubuhi ilishindwa kuendelea baada ya
wachezaji hao wa Ardhi kukataa kutoka kwenye uwanja, huku Viongozi wao wakidai
kuwa hawajapokea barua kutoka SHIMIWI kuhusu uamuzi wa kuondolewa kwenye mashindano.
Wakati fujo hizo
zinatokea, tayari waamuzi walishafanya ukaguzi wa timu zote mbili ili kuruhusu mtanange
huo ambao ungechezwa ili kumtafuta mshindi atakayetinga katika hatua ya robo
fainali.
Mahakama Sports
inashiriki katika michezo mbalimbali mwaka huu, ikiwemo Kamba Wanaume na
Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata, Tufe, Riadha na
Baiskeli.
Katika mashindano ya
SHIMIWI yaliyofanyika mwaka jana jijini Tanga, timu ya Mahakama ya Tanzania
ilizoa makombe saba baada ya kuibuka washindi katika michezo mbalimbali.
Michezo ambayo Mahakama Sports ilipata medali na makombe ni Kamba Wanawake walioibuka mshindi wa kwanza, Riadha Wanawake mita 3,000 mshindi wa kwanza, Tufe Wanawake mshindi wa kwanza, Kamba Wanaume walioshika nafasi ya pili, Mpira wa Miguu Wanaume walioshika nafasi ya pili na Bao Wanaume mshindi wa tatu.
Mashambuli ya kutupia kikapu huanzia hapa kwa Eunice Chengo.
Eunice anaitupa pasi ya mashambuli kwa Agness Mwanyika.
Agness anaitupa kwa Upendo Gustaf.
Philomena badala ya kutupia anairudisha kati kwa Nyangi Kisangeta, naye anautuliza mpira ili kuwapa nafasi watupiaji kujiweka sawa.
Nyangi anaitupa kwa mtupiaji kinara, Tatu Mawazo.Mtupiaji Tatu anatupia mpira langoni.
Mpira huoooo unatumbukia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni