Na. Richard Matasha-Mahakama, Mtwara
Mahakama
ya Tanzania Kanda ya Mtwara hivi karibuni imeendesha mafunzo kwa watumishi ili
kuwajengea uelewa kuhusu mfumo wa usimamizi na uendeshaji mashauri.
Mafunzo
hayo yaliyokuwa yanafanyika kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu yalifunguliwa na Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Ebrahim alisema, “Tuhakikishe kila
mmoja wetu anashiriki kwa kufungua akili na mawazo yake, tuwe tayari kujifunza
muda wote na kuwafundisha wananchi.”
Alisema
kuwa matumizi sahihi ya mfumo huo yataboresha huduma za kimahakama, hivyo
akawasihi kutembea na ndoto ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma ili kuhakikisha Mahakama ya Kidijitali inawezekana.
Mafunzo
hayo ni mahsusi kwa ajili ya kujianda na ujio wa mfumo mpya wa kusimamia na
kuendesha mashauri kidijitali ambao unatarajiwa kuanza kutumika mwanzoni mwa
mwezi Novemba, 2023.
Mkufunzi
Mkuu wa mafunzo hayo alikuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara,
Mhe. Fredrick Lukuna akishirikiana na Afisa Tehama wa Kanda hiyo, Bw. Richard
Matasha.
Mahakimu
Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi Mtwara na Lindi, Mahakimu Wakazi
Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya katika Mikoa ya Lindi na Mtwara, baadhi ya Mahakimu
Wakazi na watumishi wengine wa Mahakama walishiriki kwenye mafunzo hayo.
Washiriki
wa mafunzo hayo walipongeza uongozi wa Mahakama kwa hatua kubwa ya maboresho
hayo na wameahidi kujitoa kwa hali na mali ili kuendana na kasi hiyo inayoendelea
kufanyika ndani ya Mahakama ya Tanzania.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi, Mhe. Consolatha Singano (wa kwanza kulia), akiwa na watumishi wenzake wa Mahakama Kanda ya Mtwara katika mafunzo hayo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Iringa)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni