Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro
Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi
ya Mahakama kutumia vyema nyenzo walizokabidhiwa ili kuondoa hoja za ukaguzi
ndani ya Mhimili huo.
Prof. Ole Gabriel alitoa
wito huo jana tarehe 6 Oktoba, 2023 wakati akifunga mafunzo ya Kamati ya
Ukaguzi ya Mahakama ya Tanzania ambayo yaliendeshwa katika ukumbi wa Kituo Jumuishi cha
Utoaji Haki Morogoro.
Alisema kuwa amefarijika mafunzo
hayo kuwa shirikishi kwa wakuu wa idara na vitengo ambao sio wajumbe wa
kamati ya ukaguzi.
“Nimefahamishwa mmekabidhiwa
nyenzo zitakazowasaidia kutekeleza majukumu yenu vyema. Kupewa nyenzo ni jambo
moja lakini kusoma, kuelewa na kutumia ni jambo jingine ambalo ni binafsi. Ombi
langu kubwa kwenu ni kuhakikisha tunatumia nyenzo hizo vizuri ili kuleta
mabadiliko chanya,” alisisitiza.
Kadhalika, Mtendaji Mkuu
alitilia mkazo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuondoa
hoja za ukaguzi, “TEHAMA inatusaidia kufanya tracking na kupata kile tunachotaraji...
“...Tukiweza kuzuia hoja
za ukaguzi tutakuwa tumefanikiwa, utamaduni wetu baada ya haya mafunzo mazuri
uwe ni kuzuia hoja za kikaguzi, natamani ifike sehemu Mahakama iwe ya mfano kwa
kukosa hoja za ukaguzi,” alisema.
Awali, akisoma taarifa
fupi ya mafunzo hayo, Katibu wa ya Ukaguzi ya Mahakama ya Tanzania, Bi. Agnes Bulyota alisema
kuwa katika kipindi walichokuwa hapo wamefundishwa mambo mbalimbali, ikiwemo
namna ya kuandaa taarifa ya ukaguzi.
“Mafunzo haya adhimu
yametolewa kwa wajumbe wa kamati, wakuu wa idara pamoja na vitengo vyote vya
Mahakama ya Tanzania. Mafunzo haya yametuwezesha kujenga uelewa wa pamoja katika
kumshauri afisa masuhuli na kuiwezesha Mahakama kutimiza malengo yake ya
kimkakati katika utoaji haki kiufanisi,” alisema.
Meza Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa sekretarieti ya mafunzo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Iringa)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni