·Utumishi yaoga mabao 2:1
·Bunge Netiboli yabunguliwa vikapu 38:36
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Iringa
Timu za Mahakama Sports
Mpira wa Miguu na Netiboli leo tarehe 8 Octoba, 2023 zimetinga katika hatua ya
nusu fainali katika Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za
Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika mkoani hapa baada ya kuwasurubu Utumishi na
Bunge.
Ulikuwa mchezo wa
Netiboli ulioanza kuchezwa majira ya saa 7:0 katika viwanja vya Chuo Kikuu cha
Kikristo Ruaha ambapo Bunge ndiyo walioanza kulishambulia lango la Mahakama
Sports na kufanikiwa kutupia vikapu vinne vya haraka haraka.
Hata hivyo, vijana wa
Mahakama walitulia na kuanza kuwathibiti wapinzani na kujibu mapigo. Walisimama
imara na kulishabulia lango la wapinzani mara kwa mara. Hadi timu zote zinaenda
kwenye mapumziko, Mahakama Sports ilikuwa mbele kwa vikapu 18 kwa17 walizokuwa
wametupia Bunge.
Kipindi cha pili kilianza
kwa kila timu kumkaba koo mwenzake kutokana na tupia tupia za hapa na pale.
Bunge wakitupia na Mahakama nayo inatupia. Hadi mchezo unamalizika, Mahakama
Sports ilikuwa imeshatupia vikapu 38 kwa 36 walivyotupia Bunge.
Wakati Mahakama Sports
Netiboli ikiwapukutua Bunge, kaka zao timu ya mpira wa miguu imewachakaza
Utumishi kwa mabao 2:1 katika mchezo mgumu uliochezwa kwenye Uwanja wa
Samora.
Ilikuwa Mahakama Sports
walioanza kuliona lango la Utumishi katika dakika ya nne kupitia kwa kiungo punda
Seif Shamte ambaye alipachika bao safi baada ya kumvika kanzu mlinda mlango baada
ya kupokea pasi kutoka kwa Abdi Sasamalo, hivyo kuiandikia timu yake goli la
kuongoza.
Baada ya kuingia kwa bao
hilo, Mahakama Sports walianza kutandaza kabumbu safi kwa kupiga pasi fupi fupi
na kufanikiwa kuumiriki mpira kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, katika dakika za
mwisho za kipindi cha kwanza, Utumishi walipata faulo na kufanikiwa kusawazisha
baada ya mabeki wa Mahakama Sports kushindwa kuelewana.
Katika kipindi cha pili,
Mahakama Sports walizidisha mashambulizi na kuwachezea wapinzani nusu uwanja.
Dakika ya 49, winga wa pembeni Frank Obadia aliachia shuti na mpira ukazama
kwenye nyavu, baada ya kupokea pasi murua kutoka kwa Martin Peter, hivyo
kuiandikia timu yake bao la pili. Hadi mchezo unamalizika, Mahakama Sports
ilitoka kifua mbele na kutinga katika hatua ya nusu fainali.
Michezo yote miwili imeshuhudiwa na Mkurugenzi wa Mipango wa Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni mlezi wa Mahakama Sports, Erasmus Uisso.
Akizungumza baada ya
michezo hiyo, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amewapongeza wachezaji
wote kwa kucheza vizuri, kwa kujituma na hatimaye kuibuka washindi, licha ya
timu pinzani kutoa upinzani mkali.
"Hizi timu za Utumishi na Bunge ni nzuri sana na zimetoa upinzani mkali. Lakini, kama nilivyokwisha kusema, sisi tupo vizuri kwenye kila idara na timu yoyote itakayojipendekeza kwetu itapigwa. Vipigo hivi vitaendelea hadi kuchukua makombe. Hatuna utani na mtu safari hii," amesema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni