Alhamisi, 12 Oktoba 2023

MAHAKAMA SPORTS NETIBOLI YAWEKA HISTORIA SHIMIWI

·Yashika nafasi ya nne

·Mpira wa miguu waachia ndugu zao Sheria mshindi wa tatu

Na Faustine Kapama-Mahakama, Iringa 

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Netiboli imeweka historia mpya kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika mkoani hapa baada ya kushika nafasi ya nne katika mchezo huo.

Mahakama Sports imefika katika hatua hiyo baada ya kutolewa na Hazina, ambayo imeshika nafasi ya tatu kufuatia mchezo mgumu uliochezwa kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha leo tarehe 12 Octoba, 2023 kuanzia saa 10:00 jioni.

Pamoja na kucheza pungufu mchezaji mmoja katika kipindi cha pili, Mahakama Sports iliweza kumudu vyema mchezo huo ambao ulikuwa piga nikupige kwani timu moja inapotumbukiza kikapu, timu nyingine nayo inajibu mapigo.

Mchezaji mmoja wa Mahakama Sports alitolewa nje kufuatia figisufigisu za waamuzi, hivyo kuwafanya wachezaji wa Hazina wawe wengi zaidi uwanjani na kuwawezesha kuutawala mchezo.

Hadi mchezo unamalizika, Hazina walifanikiwa kutumbukiza vikapu 39, huku Mahakama Sports ikawa imevuna vikapu 30, jambo lililotafasiliwa na watazamaji kuwa matokeo yasingekuwa hivyo kama timu zote zingekuwa na wachezaji sawa.

Kitendo cha Mahakama Sports kushika nafasi hiyo kinaifanya kuweka historia mpya SHIMIWI kwani mwaka jana kwenye mashindano hayo yaliyofanyika jijini Tanga iliishia katika hatua ya 16 bora.

Katika hatua nyingine, Mahakama Sports mpira wa miguu imewaachia ndugu zao Sheria kushika nafasi ya tatu kwenye mashindano hayo baada ya kumalizika kwa mchezo kabambe uliozikutanisha timu hizo.

Mchezo huo iliochezwa katika uwanja wa Samora kuanzia saa 10:00 jioni ulikuwa wa kuvutia kwani timu hizo ndugu zilicheza kiistarabu na hapakuwepo na purukushani za hapa na pale kwa wachezaji.

Ilikuwa Mahakama Sports iliyokuwa ya kwanza kuliona lango la ndugu zao kabla nao kujipu mapigo na kusawazisha kutokana na mpira wa adhabu ulioelekezwa langoni na kumpita mlinga mlango alipokuwa anajaribu kuokoa hatari hiyo.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, timu zote zilienda kwenye mapumziko zikiwa na nguvu sawa. Katika kipindi cha pili, Mahakama Sports waliweza kumiliki mpira na kushambulia lango la wapinzani mara kwa mara.

Hata hivyo, bahati ya kupachika mabao haikuwa yao, jambo lililowapa faida Sheria na kutumia moja ya nafasi chache walizozipata kupata bao la pili na la kuongoza kutokana na adhabu ndogo iliyoelekezwa kwenye lango lao.

Hadi mwamuzi anapuliza kipenga kuashiria kumalizika kwa mtanange huo, Sheria wakaibuka washindi wa bao 2:1.

Kufuatia matokeao hayo, Mahakama Sports inashika nafasi ya nne kwenye mchezo huo na Sheria inakamata nafasi ya tatu. Fainali za mpambano huo zinatarajiwa kufanyika kesho tarehe 13 Octoba, 2023 kuzikutanisha Hazina na Mifugo.

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Netiboli iliyoiwakilisha vyema Mahakama kwenye mashindano ya SHIMIWI Iringa.
Moja ya pasi iliyozaa kikapu ilianzia hapa kwa mkata umeme Shan Ally.
Mkata umeme akageuka nyuma akamkuta mshambuliaji wa kati Nyangi Kisangeta.
Kisangenta akaitupa kwa winga Upendo Gustaf, naye akaitumbukiza kwa mtupiaji kinara Tatu Mawazo (picha chini).
Tatu Mawazo akageuka na kuitumbukiza kwenye wavu (picha chini).

Mpira huooo unatumbukia kwenye kamba.
Wachezaji wa Mahakama Sports Mpira wa Miguu wakiwania mpira.

Wachezaji wa Mahakama Sports Mpira wa Miguu wakilisakama lango la Sheria (juu na chini).





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni