Na Eunice Lugiana, Mahakama Dar es Salaam
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi amewataka Viongozi wa Mahakama zote katika Kanda hiyo kufanya kazi kwa uadilifu na uvumilivu wanapowahudumia watumishi walio chini yao na wateja wa Mahakama.
Mhe. Maghimbi aliyasema hayo jana tarehe 03 Novemba, 2023 katika kikao cha kwanza cha utendaji kazi cha Kanda hiyo kilichofanyika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho Mhe. Maghimbi alisema uongozi ni dhamana hivyo Viongozi wanapaswa kuwa na kauli njema kwa wateja na watumishi wenzao, “uongozi ni dhamana usitegemee kila mtu akupende tarajia kupendwa na wachache lakini pia kuwa mvumilivu fanya maamuzi sahihi.”
Jaji Maghimbi aliwataka Viongozi hao kutowapuuza wateja wanaoleta malalamiko bali wawasikilize na kisha wachuje kabla ya kufanya uamuzi.
Kadhalika, Mhe. Maghimbi aliwataka pia Maafisa Utumishi/Tawala kutekeleza ipasavyo wajibu wao na sio kujifungia ofisini bali wapite katika Ofisi zilizo chini yao kujua kama kazi zinafanyika sawasawa na kama wateja wanaofika mahakamani kupata huduma wanahudumiwa vizuri.
Katika hatua nyingine, Mfawidhi huyo aliwasisitiza na kuwakumbusha Mahakimu Wafawidhi wote wa Kanda hiyo kufikisha taarifa kwa Mahakimu wengine kuwa tarehe 06 Novemba, 2023 Mfumo mpya wa Kuratibu Mashauri mahakamani (e-CMS) utaanza rasmi hivyo kila Hakimu akae mkao wa kujiandaa kisaikolojia kuwa Mfumo mpya unaanza kufanya kazi.
Amewatoa wasiwasi Mahakimu hao na kuwaomba wajitahidi kuujua Mfumo huo na kama kuna changamoto wafanye mawasiliano mapema.
Pia amewataka Mahakimu hao kutokukumbatia majalada ya mashauri badala yake wagawane ili kuondoa mrundikano katika Mahakama zao, na kuongeza kuwa, kama Mahakama husika imezidiwa waombe msaada wa Mahakimu kutoka Mahakama zingine zilizopo ndani ya Kanda hiyo.
Naye, Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Moses Mashaka amesema watumishi 53 wamebadilishwa vituo vya kazi ndani ya Kanda hiyo ili kuleta ufanisi wa kazi na pia kuhusu suala la kuimarisha maadili Mtendaji huyo amewasihi watumishi hao kuwa maadili yawe nguzo mojawapo katika utendaji kazi.
Akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho, kwa upande wake Naibu Msajili Mkuu Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Sundi Fimbo amewaomba wajumbe wote wakatekeleze maazimio ya kikao kazi hicho ambayo ni pamoja na kupata taarifa ya ukaguzi wa ndani, ifikapo tarehe 30 Desemba, 2023, kutokuwa na mrundikano wa mashauri, kufanya vikao vya utendaji kazi mara moja kwa wiki.
Katika kusimamia maadili na kuona maadili yanapewa kipaumbele Kamati ya malezi imeundwa ili kusikiliza changamoto za watumishi Mahakimu na wasio Mahakimu, Kamati hiyo inaongozwa na Mwenyekiti Mhe. Elizabeth Mkwizu, Naibu Msajili wa Kanda hiyo, Mhe. Joseph Lwambano Naibu ambaye ni Katibu na Bi. Athanasia Kabuyanja, Mtendaji Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam- Kisutu kama Katibu ikiwa suala linalojadiliwa na Kamati linamhusu Mtumishi asiye Hakimu (Non Judicial officer).
Wajumbe wa Kamati hiyo ni Mhe. Joyce Mkhoi Hakimu Mkazi Mfawidhi Pwani, Mhe. Veneranda Kaseko, Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Kisarawe na Bw. Brown Mtimba msaidizi wa kumbukumbu Mwandamizi kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (aliyeketi mbele katikati) akiongoza kikao cha Watumishi Kanda ya Dar es Salaam kilichofanyika jana tarehe 03 Novemba, 2023 katika ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni.
Wajumbe wakimfuatilia yalikuwa yakijiri katika kikao.
Jaji Mfawidhi Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (katikati), Naibu Msajili Mkuu wa Kanda hiyo, Mhe. Sundi Fimbo (kushoto) na Mtendaji wa Kanda hiyo, Bw. Moses Mashaka (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Wakaguzi Wa Ndani, Wahasibu Na Wakuu Wa Masjala walioshiriki katika kikao jana tarehe 03 Novemba, 2023.
(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni