Jumamosi, 4 Novemba 2023

MAGEREZA KANDA YA SHINYANGA ZAUNGANISHWA KIDIGITALI

Na Emmanuel oguda na Naumi Shekilindi, Mahakama Shinyanga

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe Frank Mahimbali amemkabidhi Mkuu wa Gereza la Wilaya Kahama Mrakibu SP Hamza Abdallah vifaa vya TEHAMA vya kisasa vitakavyotumika kusikiliza mashauri kwa njia ya ‘Video Conferencing’ vitakavyowezesha usikilizwaji wa mashauri wakati Mahabusu akiwa gerezani bila kupelekwa Mahakamani.

Akizungumza wakati akikabidhi vifaa hivyo, tarehe 02 Novemba, 2023, Mhe .Mahimbali alisema kuwa, kwa sasa Mahakama ya Tanzania imehamia katika TEHAMA hivyo shughuli nyingi sasa zinafanyika kwa kutumia Mifumo mbalimbali iliyoanzishwa kwa lengo la kuharakisha utoaji haki kwa wananchi. 

“Ni matarajio yetu vifaa hivi vitafanya kazi iliyokusuidiwa ya usikilizwaji wa mashauri na sasa gharama za kusafiri kutoka Kahama kwenda mahakamani Mbogwe au Bukombe zitapungua sana na ndugu zetu wa Magereza wataondokana na gharama za usafiri zilizokuwa zikiwakabili kwa kuwa sasa kesi inaweza kusikilizwa Mfungwa akiwa gerezani bila kusafiri kwenda Mahakamani,’’ alisema Mhe. Mahimbali.

Mhe. Mahimbali alisema kuwa, vifaa hivyo vilivyokabidhiwa kwa Magereza vitawezesha usikilizwaji wa mashauri kwa haraka na pia kupunguza gharama za usafiri pamoja na muda.

Kwa upande wake Mkuu wa Gereza la Wilaya Kahama, Mrakibu wa Magereza SP Hamza Abdallah, ameushukuru Uongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga kwa kuwakabidhi vifaa hivyo kwa ajili ya usikilizwaji wa mashauri kidigitali na kwamba kama Magereza umewaondolea changamoto ya usafiri hasa kwa Mahabusu wenye mashauri Wilaya za Mbogwe na Bukombe.

‘’Tunayo furaha tumepokea vifaa vya kisasa kabisa kutoka Mahakama ya Tanzania kwa ajili ya usikilizwaji wa Mashauri, kwa kweli tumefurahi kwa sababu kuwa na vifaa hivi kwetu Magereza itatuondolea gharama za kusafirisha Mahabusu kwenda Wilaya za Bukombe na Mbogwe,’’ alisema SP Abdallah.

Wakati huo huo, Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita aliyeambatana na Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mh. Caroline Kiliwa wamekabidhi vifaa kama hivyo kwa niaba ya Jaji Mfawidhi Kanda ya Shinyanga katika Gereza la Wilaya Bariadi. 

Akikabidhi vifaa hivyo, Bw. Kanyairita amesema kuwa Mahakama ya Tanzania imejipanga kikamilifu katika kuhakikisha mashauri yanamalizika kwa wakati, pia kuhakikisha inatekeleza nguzo ya Tatu ya mpango Mkakati inayohusu Kurejesha imani ya wananchi na Ushirikishwaji wa Wadau.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Gereza la Bariadi, Mkaribu wa Magereza SP Yona Magage ameishukuru Mahakama kwa kuwapatia vifaa vya kisasa vya kusikiliza mashauri kwa njia ya video ambavyo vitaiondolea magereza gharama za usafiri, kuokoa muda hali kadhalika kuimarisha usalama wa Mahabusu kwani sasa hawatasafiri umbali mrefu kufuata Mahakama.

Kwa upande mwingine, Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Maswa, Mhe. Aziz Khamis amekabidhi vifaa kama hivyo katika gereza la Wilaya ya Maswa.

Mahakama ya Tanzania katika jitihada zake kuelekea Mahakama Mtandao e-Judiciary’ imetoa pia Televisheni za kisasa inchi 65 kwa Magereza Kahama, Bariadi na Maswa kwa ajili ya usikilizwaji wa Mashauri kwa njia ya ‘’Video Conferencing’’ katika kuhakikisha lengo la utoaji haki kwa wakati linafikiwa kwa wakati.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali (wa pili kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Gereza Wilaya Kahama, SP Hamza Abdallah vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya Video. Kushoto ni Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Bi. Mavis Miti na wengine ni Maafisa wa Magereza wakishuhudia zoezi la makabidhiano.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali (kushoto) akizungumza jambo na Maafisa Magereza. Katikati ni Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Bi. Mavis Miti.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga Mhe. Frank Mahimbali na wenzake wakionekana kwenye Video baada zoezi  la kufunga vifaa hivyo katika gereza la Wilaya Kahama.
Mkaguzi Msaidizi wa Gereza la Wilaya Kahama, Mrakibu Anthony Kusekwa akifanya majaribio ya kuandika katika kifaa kilichokabidhiwa katika Magereza hiyo kwa ajili ya usikilizwaji wa mashauri.
Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita (kulia) akikabidhi Televisheni ya kisasa kwa Kaimu Mkuu wa Gereza la Bariadi, SP Yona Magage.
Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Maswa, Mhe. Aziz Khamis (kushoto) akikabidhi Televisheni ya kisasa kwa  Mkuu wa Gereza la Wilaya Maswa, SP Omary Mbwambo.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni