·Wabadilishana uzoefu na wenzao wa kituo cha kuchakata taarifa ya kimahakama
Na Tiganya Vincent-Kazakhstan
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel jana tarehe 6 Novemba, 2023 amewaongoza Wataalamu wa Mahakama ya Tanzania katika ziara ya kubadishana uzoefu kuhusu uimarishaji wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuboresha shughuli za kila siku za utoaji wa haki nchini.
Timu hiyo ambayo imeweze kutembelea Mahakama ya Juu ya Upeo (Supreme Court) ya Kazakhastan ambapo ilipata fursa ya kutembelea chumba maalum cha kusimamia, kuendesha na kudhibiti mtandao na kituo cha kuchakata taarifa za kimahakama kwa ajili ya kujifunza.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Prof. Ole Gabriel alimweleza Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Kazakhstan Nail Akhetzakirov kuwa tukio hilo ni mwendelezo wa iliyofanyika mwaka 2018 ambapo watajifunza uendeshaji, usimamizi wa shughuli za Mahakama kwa kutumia TEHAMA.
Alisema Nchi ya Kazakhastan imepiga hatua katika matumizi ya TEHAMA katika shughuli mbalimbali za Mahakama, hivyo nao watabadilishana uzoefu ili kuendeleza mapinduzi makubwa yanayoendelea ya Mahakama mtandao nchini Tanzania ikiwemo kupunguza matumizi ya karatasi katika uendeshaji wa shughuli zake.
Aidha, Prof. Ole Gabriel alimuomba Mtendaji Mkuu mwenzake wa Mahakama ya Kazakhastan kuendelea kushirikiana kwa Maafisa TEHAMA wa pande zote kwa kukubalishana uzoefu kwa ajili ya kuwajengea uwezo ili waweze kuendana na kasi ya mabadiliko ya Teknolojia hiyo yanayobadilika kila wakati duniania.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Kazakhastan aliishukuru timu ya Tanzania kwa ziara hiyo ya kubadilisha uzoefu na kuahidi kuendelea na ushirikiano utakaowezesha pande zote mbili kuimarisha zaidi matumizi ya TEHAMA mahakamani.
Awali, Prof. Ole Elisante na timu yake walipata fursa ya kutembelea Ofisi za Benki ya Dunia na kukutana na Mwakilishi wa Kazakhstan Andrei Mikhnev.
Viongozi wengine waliopo katika ziara hiyo ya mafunzo ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Jenifa Omolo, Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Angelo Rumisha na Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Alesia Mbuya.
Sanamu ya Lady
Justice katika Mahakama ya Upeo wa Juu ya Kazakhstan.
Mwakilishi wa
Benki ya Dunia nchini Kazakhstan Andrei Mikhenew akizungumza na ujumbe wa
Mahakama ya Tanzania ulipomtembelea ofisini kwake tarehe 6 Novemba, 2023.
Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa na ujumbe wa
Mahakama ya Tanzania uliotembelea Mahakama ya Upeo wa Juu ya Kazakhstan kwa
ajili ya kubadilishana uzoefu wa usimamizi na uendeshaji wa mifumo ya
kimahakama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni