Na Mwanaidi Msekwa-Mahakama, Kazi
Wahenga wanasema, “Elimu ni bahari, Elimu haina
mwisho.” Kamati ya Elimu ya Ndani Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi
imekuwa ikiwapatia watumishi mafunzo mbalimbali ya uhalisia katika mazingira
yote.
Hili limejitokeza hivi karibuni pale Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina alipoongoza
Viongozi na watumishi wa Mahakama hiyo kujifunza namna bora ya uokoaji wa
maisha ya binadamu katika hali hatarishi.
Mtaalamu kutoka Ofisi ya Msalaba Mwekundu, Bw.
Bonaventure Minja alifafanua wakati wa mafunzo hayo maana ya huduma ya kwanza, kuwa
ni msaada wa awali anaopatiwa mtu aliyejeruhiwa au kuugua ghafla na mara nyingi
huduma hiyo hutolewa na mtu wa kawaida kwa mtu aliyepata jeraha au ugonjwa.
Watumishi walijifunza kanuni zinazotumika wakati wa
kutoa huduma ya kwanza huku Bw. Minja akielezea umuhimu wa kutoa huduma ya
kwanza kwa muarithika aliyepatawa na majanga. Kwa msisitizo, aliwaasa wanapotoa
huduma ya kwanza wajiepushe na vitendo vitakavyopelekea kumsababishia mgonjwa
matatizo makubwa.
Akiendelea kutoa mafunzo hayo, Bw. Minja pamoja na Mratibu
wa Mafunzo katika Ofisi ya Msalaba Mwekundu, Bw. Deus Almachius walishirikiana
vema kutoa elimu kwa njia ya vitendo. Jambo hilo liliongeza hamasa kubwa kwa Viongozi
na watumishi waliohudhuria darasa hilo na kutoa shauku ya kuendelea kujifunza
zaidi.
Akiahirisha mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya
Elimu ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt.
Modesta Opiyo aliwashukuru wawezeshaji na kuwaomba kufika mahakamani hapo tena
pale watakapoalikwa.
Naye Jaji Mfawidhi alimpongeza Bw. Bonaventure kwa
umahili wake katika uwasilishaji wa mada. Mafunzo kwa watumishi wa Divisheni ya
Kazi yanatolewa kila siku za Ijumaa kuanzia saa 1:30 hadi 2:45 asubuhi katika
ukumbi wa mikutano wa Mahakama na huwafikia wengi kwa kupitia njia ya mtandao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni