Na Hasani Haufi- Mahakama, Songea
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha amemkabidhi Mkuu wa
Gereza la Wilaya ya Tunduru, Mrakibu wa Magereza Uswege Yoran vifaa vya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) vya kisasa vitakavyotumika kusikiliza
mashauri kwa njia ya mtandao.
Vifaa hivyo vilivyokabidhiwa
hivi karibuni vitawawezesha Mahabusu waliopo gerezani kusikiliza mashauri yao
bila kufika mahakamani moja kwa moja.
Akizungumza wakati
akikabidhi vifaa hivyo, Mhe. Karayemaha alisema kuwa Mahakama ya Tanzania imepiga
hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA na imeangalia changamoto nyingi
zinazosababisha kuchelewa kwa huduma za kimahakama, hivyo ikaanzishe mifumo
mingi inayoenda kutibu changamoto hiyo.
“Ni matarajio yetu kuwa
vifaa hivi vitafanya kazi iliyokusudiwa ya usikilizaji wa mashauri na vitaenda
kutibu kero na visingizio mbalimbali, ikiwemo kukosekana kwa mafuta na gari ya
kupeleka mahabusu na wafungwa mahakamani. Vifaa hivi pia vitasaidia mahabusu wenye
changamoto za kiafya ambazo zinawafanya kushindwa kutoka gerezani na kupelekea
mashauri kuchelewa,’’ alisema.
Mhe. Karayemaha alisema
kuwa, vifaa hivyo vilivyokabidhiwa kwa gereza hilo vitaenda kuongeza kasi ya
upatikanaji wa haki kwa haraka na kupunguza au kuondoa kabisa malalamiko kwa
mahabusu na wafungwa, kwani mashauri yanapokaa kwa muda mrefu ndivyo haki ya
mahabusu waliopo gerezani inachelewa.
Kwa upande wake, Mkuu wa
Gereza la Wilaya ya Tunduru ameushukuru uongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania
Kanda ya Songea kwa kusikia kilio cha muda mrefu na mwishowe kuwakabidhi vifaa
hivyo vya kisasa kwa ajili ya kusiliza mashauri kwa njia ya mtandao, hivyo kuwapunguzia
gharama ya kubeba mahabusu hao.
“Tuna furaha isiyo na kifani
kwani tunapitia changamoto kubwa, ambazo tunashindwa kuzitatua kwa vile zipo nje
ya uwezo wetu, hivyo vifaa hivi tutavitumia kwa matumizi yaliyokusudiwa kwa
lengo la kupunguza gharama za usafiri na muda pia,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya
hiyo, Mhe. Julius Mtatiro kwa ujumla aliipongeza Mahakama ya Tanzania
inayoongozwa na Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahimu Juma, kwa kupiga hatua kubwa
katika upande wa TEHAMA na kuwa mfano bora wa kuigwa kwa taasisi zingine za
kiserikali.
Alisema kuwa miongoni mwa
malengo ya Mahakama ni kutoa haki kwa wakati, hivyo vifaa vilivyotolewa vitaenda
kutibu matatizo ya mahabusu na akaahidi kuwa msimamizi katika vifaa hivyo.
“Mahakama ya Tananzania
imekuwa ikikimbia katika upande wa utoaji haki kwa njia ya TEHAMA na kuwa ni
sehemu moja wapo ya taasisi zingine za kiserikali kuiga kitu kizuri kama hicho siyo
vibaya. Kutokana na jitihada hizi ninaahidi nikiwa kama Mkuu wa Ulinzi
nitahakikisha vifaa vinakuwa salama siku zote kwa manufaa ya taifa letu,’’
alisema.
Katika tukio jingine, Jaji
wa Mahakama Kuu katika Kanda hiyo, Mhe. Upendo Madeha naye amekabidhi vifaa
kama hivyo juzi tarehe 06 Novemba, 2023 katika Gereza la Wilaya Mbinga. Alisema
kuwa vifaa hivyo ni moja ya mageuzi ya kitaasisi katika kukamilisha na
kuboresha mfumo wa uendeshaji wa mashauri mtandao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza
la Wilaya Mbinga, Mrakimu Mwandamizi wa Magereza Aloyce Mbongo ameushukuru
uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea kwa kuwarahisishia huduma na
kuwapunguzia gharama ya usafiri na muda.
“Zipo sababau nyingi,
lakini kimsingi Mahakama imefanya maboresho na mageuzi makubwa sana ya kitaasisi
ikiwemo mifumo kama JSDS, TANZLII, TAMS na mfumo wa kusikiliza mashauri kwa
njia ya mtandao,” alisema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya
Mbinga, Mhe. Aziza Mangosongo ameushukuru uongozi wa Mahakama kwa jitihada
wanazozifanya za kuboresha huduma za Mahakama katika maeneo mbalimbali, ikiwa
lengo ni kuhakikisha huduma za Mahakama zinapatikana kwa urahisi.
Aliomba wataalam wa mifumo wa Mahakama kutembelea na kutoa elimu ya matumizi ya vifaa hivyo mara kwa mara ili kuhakikisha changamoto za mifumo zinatotatuliwa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha (kulia mwenye suti ya
bluu) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Julius Mtatiro.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha akitetea jambo na Mkuu wa Wilaya
ya Tunduru, Julius Mtatiro (wa kwanza kutoka kulia).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha na wenzake kwenye luninga baada
ya Afisa TEHAMA, Bi. Catherine Okumu kukamilisha zoezi la kufunga vifaa hivyo.
Jaji wa Mahakama Kuu
Kanda ya Songea, Mhe. Upendo Madeha akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya
Mkuu wa Wilaya Mbinga.
Jaji wa Mahakama Kuu
Kanda ya Songea, Mhe. Upendo Madeha (wa pili kulia) akimkabidhi vifaa vya TEHAMA,
Mkuu wa Gereza la Mahabusu Mbinga Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Aloyce Mbongo.
Jaji wa Mahakama Kuu
Kanda ya Songea, Mhe. Upendo Madeha (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya
pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mhe. Aziza Mangosongo (kulia) na kushoto
kwake ni Mkuu wa Gereza la Mbinga, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Aloyce Mbogo pamoja
na wadau wengine wa Mahakama.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni