Na. Innocent Kansha- Mahakama.
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es salaam imetimiza
ahadi yake iliyoitoa ili kuhakikisha inatatua changamoto zinazowakabili
wafungwa na mahabusu walioko magerezani kwa kuandaa na kutekeleza mpango maalum
wa kuwawezesha Mawakili wa utetezi kupata muda wa kutosha wa kutembelea magerezani
na kuzungumza na wateja wao kabla ya kuanza kwa usikilizwaji wa mashauri
mbalimbali yanayowakabili.
Akizungumza kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Dar-es-salaam, Mhe. Salma Maghimbi. Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Dar es salaam Mhe. Butamo Phillip aliwahakikishia wadau kuwa zoezi la kuwatembelea Mahabusu litakuwa
endelevu na litapewa muda wa kutosha kabla ya kuanza vikao ya Mahakama Kuu ili
kuwapa wadau fursa ya kuweza kufanya mawasiliano na Mawakili wao.
“Mpango
huu unalenga kuhakikisha kuwa Mawakili wa kujitegemea wanapata fursa ya kutosha
ya kuonana na wateja wanaowawakilisha Mahakamani. Uwakilishi huu ni kwenye mashauri
mbalimbali hususani ya Jinai kama vile mashauri ya Ugaidi, Mauaji na Madawa
ya kulevya”, alisema Jaji Phillip.
Mhe.
Phillip alisema kuwa, Mpango huo utakuwa endelevu na utakuwa ukifanyika kabla
ya muda wa vikao maalum vya mashauri ya jinai (Criminal Sessions). Kanda ya
Dar-es-salaam itaanda mazingira magerezani ya kuwawezesha Mawakili usafiri wa kwenda
kwenye magereza hayo ili kuwatembelea wateja wao wanaowatetea kwa kupitia takwa
la kisheria. Hii itaweza kurahisisha mawasiliano kati ya Mawakili na Wateja wao
Pamoja na kuhakikisha haki inatendeka kwa washtakiwa kwa kupata haki ya utetezi
wa mashtaka wanayokabiliwa nayo.
“Nichukue fursa hii kuwashukuru kwa dhati Mawakili wote
waliojitokeza kutoka Chama cha Mawakili wa Kujitegemea (TLS) kwa kukubali wito
wa Mahakama na kujitokeza kwa ajili ya zoezi hili. Vile vile niwashukuru Jeshi
la Magereza kwa kukubali na kuhirikiana nasi mara baada ya kuelezwa adhima ya
Mahakama”, alisema Mhe Phillip.
Mhe.
Phillip aliwambia Mawakili walioshiriki zoezi hilo kuwa, dhumuni la safari hiyo
ya kutembelea Magereza yanayowahifadhi Mahabusu wenye Mashauri mahakamani ni
kujenga msingi wa uelewa wa pamoja kati ya Mawakili na Mahabusu ili waweze
kuzungumza nao ikiwa ni maandalizi ya vikao vya kusikiliza mashauri
wanayokabiliwa nayo. Kwa kufanya hivyo Mahakama inatekeleza na kutimiza takwa
la nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa
Ushirikishwaji wa Wadau.
Mhe.
Phillip aliwambia Mawakili hao kuwa, kwa sasa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Dar-es-salaam hivi karibuni imekwisha andaa vikao 10 ambavyo vitahusisha,
vikao vine (4) vya mashauri ya mauaji,
viako vitano (5) vya mashauri ya ugaidi, na kikao kimoja (1) cha shauri la madawa
ya kulevya.
Kwa
upande wao maafisa magereza wameshukuru jihitada za Mahakama za kufanya ukaguzi
huo, kwakuwa unapunguza sana malalamiko ya mahabusu hao wanaosubiri kusikilizwa
kwa mashauri yao. Wakaiomba Mahakama iendelee kudumisha ushirikiano huo, kwa hatua
mbalimbali zinazochukuliwa na Mahakama Kuu, Kanda ya Dar-es-salaam katika
kusukuma mashauri kwani kumepunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya mahabusu waliopo
magerezani ambapo imepungua kwa takribani asilimia 50 ya wale waliokuwepo mwaka
jana.
Zoezi
hilo limefanyika kutokana na ziara mbalimbali zaMahakama za ukaguzi wa
Magereza. Katika ziara hizo Mahakama imekuwa ikipokea malalamiko na hoja
mbalimbali kutoka kwa Mahabusu na Wafungwa waliopo magerezani.
Mhe.
Phillip alifafanua kuwa, moja kati ya changamoto iliyoanishwa na mahabusu
wanaosubiri vikao vya mashauri (Criminal Session) ilikuwa ni kutopatiwa haki
yao ya utetezi kwa ufasaha. Mahabusu hao wamekuwa wakilalamikia uwakilishwaji
wao kwenye vikao vya jinai, uwakilishi ambao hutolewa na Mahakama bila gharama.
“Mahabusu walilalamikia kutokupata fursa ya kutosha ya kuongea na mawakili wao na kuweza kujua masuala mbalimbali ya utetezi wao na hata wengine kuonana na Mawakili wa utetezi katika chumba cha Mahakama wakati shauri linaendelea hivyo kuhisi kuwa wananyimwa haki ya uwakilishi vema kwenye utetezi wao”, alisema Jaji Phillip.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni