Na Tiganya Vincent, Astana-Kazakhstan
Taasisi ya Mafunzo kwa ajili ya kuwaanda Majaji ya nchini Kazakhstan imesema iko tayari kushiriana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) nchini Tanzania kwa lengo la kubadilishana uzoefu utakaosaidia kuimarisha utendaji na kuwaendeleza Maafisa hao wa Mahakama.
Hatua hiyo ilifikiwa tarehe 10 Novemba, 2023 katika Mji Mkuu wa Kazakhstan wa Astana wakati wa mkutano kati ya ujumbe wa Mahakama ya Tanzania uliongozwa na Mtendaji Mkuu Prof. Elisante Ole Gabriel pamoja na wa Taasisi ya Majaji ya Mahakama ya Upeo ya Kazakhstan.
Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Majaji ya Kazakhstan iliyopo chini ya Mahakama ya Upeo, Bi. Baimoldina Zauresh Hamitovna alisema kuwa wao wako tayari kuingia makubaliano na Chuo cha Uongozi wa Mahakama-Lushoto Tanzania kwa lengo la kubadilishana uzoefu kitaaluma na kuboresha Sekta ya utoaji haki kwa pande zote.
Alisema kwa muundo wao kabla ya mtu kuwa Jaji anatakiwa kushiriki mafunzo ya Shahada ya Uzamili (Master Degree) ya Sheria katika Taasisi hiyo na ili apate udahili anapaswa kuwa na miaka 28 na kuendelea, Stashahada (Diploma) katika fani ya Sheria na uzoefu usiopungua miaka mitano.
Zauresh aliongeza kuwa katika Nchi hiyo kuna njia mbili za kuwa Jaji ya kwanza ikiwa ni lazima mtu awe amesoma Stashahada (Diploma) ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Nchi hiyo na ya pili ni lazima mtu asome katika Taasisi ya Mafunzo kwa ajili ya kuwaanda Majaji na kufaulu mitihani yote.
Alisema mtu anayepitia katika Taasisi ya Mafunzo ya kuwaandaa Majaji anakuwa na nafasi kubwa ya kufaulu wakati wa ushindani wa kuwatafuta watu wanaostahili kuteuliwa kuwa Majaji nchini humo.
Awali, Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel aliuomba Uongozi wa Taasisi hiyo kuangalia namna ya kuingia makubaliano ya kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto nchini Tanzania katika kubadiliana uzoefu wa kuwaendeleza Maafisa Mahakama na Watumishi wengine.
Alisema kuwa, Chuo cha Uongozi wa Mahakama cha Lushoto (IJA) kimekuwa na utaratibu wa kuwapa mafunzo elekezi Majaji, Mahakimu na Watumishi wengine wasio Maafisa wa Mahakama kabla ya kuanza majukumu yao mapya jambo ambalo limesaidia kufanya kazi kwa ufanisi ndani ya Mahakama ya Tanzania.
Prof. Ole Gabriel alisema wakikubaliana wanaweza kuandaa Programu ambazo zinaweza kufundishwa katika pande mbili kama sehemu ya kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo kwa watumishi na Maafisa wa Mahakama waliopo kazini na wale walioteuliwa kuingia kazini.
Aliongeza kuwa, endapo watakubaliana Uongozi wa Mahakama ya Tanzania utahakikisha unasimamia makubaliano yaliyofikiwa kwa manufaa ya pande zote mbili.
Naye, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Angelo Rumisha alisema kwa Tanzania Majaji wanaandaliwa kutoka Vyuo Vikuu mbalimbali kwa kupata Shahada ya Sheria na kupita katika Shule ya Sheria (Law School of Tanzania) na wanapoteuliwa wanapata mafunzo elekezi katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
(Picha na Tiganya Vincent)
(Imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni