Na Tiganya Vincent, ASTANA-Kazakhstan
Ujumbe wa Mahakama ya Tanzania ukiongozwa na Mtendaji Mkuu Prof. Elisante Ole Gabriel umetembelea Mahakama ya Kituo cha Kimataifa cha Biashara Astana na Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi kilichopo nchini Kazakhstan kwa lengo ya kubadilishana uzoefu kuhusu njia za usuluhishi katika utatuzi wa migogoro ikiwemo ya kibiashara na uwekezaji katika sekta mbalimbali.
Akizungumza jana mjini Astana mara ya baada ya kupata maelezo kutoka kwa Watendaji wa Mahakama hiyo na Kituo hicho, Prof. Ole Gabriel alisema kuwa ziara hiyo ilikuwa na lengo la kubadilishana uzoefu ambao utasaidia kuendelea kuboresha zaidi Kituo cha Usuluhishi cha Mahakama Kuu nchini Tanzania.
“Uzoefu tuliopata utasaidia kuweka mipango ambayo itakiwezesha Kituo cha Usuluhishi kutumika zaidi katika utatuzi wa migogoro mbalimbali ikiwemo ile ya kibiashara, ya sekta za ujenzi na uwekezaji kwa ajili ya kuimarisha uchumi kwa kupunguza mlolongo mrefu wa kesi unaotumia njia nyingine za Mahakama, alisema Prof. Ole Gabriel.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mahakama hiyo, Almat Igenbayev alisema Kituo cha Kimataifa ya Usuluhishi (IAC) kilianzishwa kwa lengo kutatua migogoro ya kimataifa inayohusu biashara na uwekezaji wa aina mbalimbali na imekuwa ikifanya kazi kwa saa 24.
Alisema, katika kutekeleza majukumu yake Mahakama hiyo imepata uzoefu mkubwa katika kujihusisha na usuluhishi wa migogoro katika maeneo mbalimbali ya uchumi, ikiwemo masuala ya kibenki, huduma za kifedha, viwanda na Kampuni za ujenzi, masuala ya mafuta na gesi kwa kuhusisha Kampuni ya Kazakhstan na nje ya Nchi hiyo kama vile Uingereza na Ireland ya Kaskazini, New Zealand, Jamhuri ya Korea, Uswisi, Urusi, Ukraine, China, Latvia, Uturuki, Misri, Tajikistan, Kyrgyz, Ushelisheli na nyingine.
Igenbayev alisema Mahakama ni huru haingiliwi na Serikali na hata usuluhishi unaofikiwa katika Mahakama hiyo hauwezi kuhojiwa na Mahakama yoyote.
Naye Mwanasheria kutoka Mahakama hiyo, Aidana Rassova alisema Mahakama ya Biashara na Kituo cha Kimatifa cha Usuluhishi vimekuwa vikitumia Majaji kutoka Mataifa mbalimbali katika usikilizaji na uendeshaji wa mashauri yake na kuongeza imekuwa ikipata msaada mkubwa kutoka Serikali ya Kazakhstan.
Aliongeza kuwa hadi kufikia Mwezi Aprili mwaka 2023, Mahakama hiyo ilikuwa haitozi ada yoyote kwa ajili kufungua shauri isipokuwa kwa mambo yaliyokuwa yakihusu usuluhishi ndio walitakiwa kulipa ada kwa ajili ya wasuluhishi.
Alisema baada ya Mwezi Aprili mwaka huu walianza kutoza ada ya kufungua shauri lakini ni kidogo ukilinganisha na Mahakama nyingine za nchini humo.
Ujumbe wa Mahakama ya Tanzania umemaliza ziara ya mafunzo nchini Kazakhstan baada ya kutembelea Mahakama ya Upeo (Supreme Court) na kujifunza matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari katika usimamizi wa shughuli mbalimbali, kisha kukutana na Naibu Waziri wa Sheria, Baraza la Juu linalosimamia Maadili ya Majaji na kutembelea Taasisi ya Mafunzo kwa Majaji.
Viongozi waliongozana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ni pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu na Mkuu wa Kituo cha Maboresho cha Mahakama Mhe. Dkt. Angelo Rumisha, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Omolo, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bi. Alesia Mbuya na watumishi wengine wa Mahakama ya Tanzania.
(Picha na Tiganya Vincent)
(Imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni