Jumamosi, 4 Novemba 2023

MFUMO MPYA WA KIELEKTRONIKI WA KURATIBU MASHAURI MAHAKAMANI KUANZA KUTUMIKA NOVEMBA SITA

Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

Kaimu Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Sylivester Kainda amesema Mhimili huo utaanza rasmi matumizi ya Mfumo mpya wa Kielektroniki wa Kuratibu Mashauri (e-Case Management) tarehe 06 Novemba, 2023.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana tarehe 03 Novemba, 2023 na Mkuu huyo, matumizi ya Mfumo wa Menejimenti ya Mashauri unaotumika kwa sasa utazimwa kupisha matumizi ya Mfumo mpya.

“Kutokana na Maboresho ya kimfumo yanayoendelea, zoezi la kuzima Mfumo wa Menejimenti ya Mashauri (JSDS2) unaotumika kwa sasa litafanyika kuanzia tarehe 03 Novemba 2023 saa 6:00 Usiku hadi tarehe 05 Novemba 2023 saa 6 usiku ili kupisha uhamishwaji wa taarifa kwenda kwenye Mfumo mpya ulioboreshwa,” amesema Mhe. Kainda kupitia taarifa hiyo.

Amesema kuwa, katika kipindi hiki, taarifa zote zinazohusiana na Mfumo wa ‘JSDS’ hazitapatikana na baada ya Mfumo mpya kuanza kutumika kutakuwa na madawati ya kutoa msaada ambayo yapo katika Mahakama zote nchini yataendelea kuwasaidia wateja wasioweza kuutumia.

Ameongeza kuwa, endapo mtu atapatwa na changamoto kuhusu matumizi ya Mfumo huo, awasiliane na Viongozi wa Mahakama iliyo karibu naye au apige simu namba 0800750247 au 0714278389.

Mmoja kati ya Maafisa TEHAMA wa Mahakama aliyeshiriki kutengeneza Mfumo huo, Bw. Samwel Mshote amesema kuwa, Mfumo huo umeboreshwa zaidi na ni rahisi kuutumia.

Amesema kwamba, Mfumo huo una sifa lukuki ambazo baadhi yake ni pamoja na kuungana na Taasisi mbalimbali kwa ajili ya kubadilishana taarifa (e-Wakili, NIDA, BRELA, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mingine.

Kwa mujibu wa Bw. Mshote, Mfumo huo una uwezo wa kutoa namba za mashauri (automatic case numbering) sambamba na kuwapangia mashauri (case) Majaji na Mahkimu kulingana na aina ya mashauri waliyokuwa nayo.

“Mfumo huu pia una uwezo wa kutengeneza jalada la kielektroniki kupitia mienendo, vielelezo, viambatanisho na maamuzi (digital file generation),” amesema Bw. Mshote.

Ameongeza kuwa; Mfumo huo pia una dirisha la usajili wa mashauri ya Mahakama ya Rufani, mashauri ya kifamilia ya mirathi, ndoa na talaka na mengine na vilevile una uwezo wa kufanya utenganishi wa wadaawa endapo ni watu binafsi, Taasisi za Serikali au Makampuni.

Kaimu Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Sylivester Kainda.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni