Alhamisi, 30 Novemba 2023

JAJI RAIS MAHAKAMA KUU ZIMBABWE AKAMILISHA ZIARA YAKE MAHAKAMA YA TANZANIA

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Jaji Rais wa Mahakama Kuu Zimbabwe, Mhe. Mary Dube leo tarehe 30 Novemba, 2023 amekamilisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu na tayari ameshaondoka nchini.

Mhe. Dube alisindikizwa na kuagwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere majira ya saa 9.00 usiku na Kaimu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Projestus Kahyoza na maafisa wengine wa Mahakama.

Maafisa wengine wa Mahakama walioshuhudia kuondoka kwa Viongozi wa Mahakama Zimbabwe ni Mtendaji wa Mahakama Philibert Matotay, Hakimu Mkazi, Mhe. Mary Kallomo na Afisa Itifaki Swalehe Mwindady.

Mhe. Dube aliwasili nchini siku ya Jumapili tarehe 26 Novemba, 2023 kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuitembelea Mahakama ya Tanzania kwa malengo mbalimbali, ikiwemo kujifunza shughuli za utoaji haki kwa wananchi.

Kiongozi huyo alipokelewa kwenye Uwanja wa Ndege na Viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe Salma Maghimbi.

Viongozi wengine wa Mahakama waliokuwepo kumlaki kiongozi huyo kutoka nchini Zimbabwe ni Kaimu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Projestus Kahyoza, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu, Mhe. Benazetha Maziku na Mtendaji wa Mahakama, Bw. Philibert Matotay.

Mhe. Dube aliambatana na Viongozi wengine akiwemo Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Walter Chikwana, Msajili wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe, Mhe. Kudzai Maronga, Mkuu wa Fedha wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Milton Shadaya na Mkuu wa Teknolojia ya Habari (IT) wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Obey Mayenga.

 

Katika siku yake ya kwanza, Jaji Rais wa Mahakama Kuu Zimbabwe alikutana na mwenyeji wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani na kufanya naye mazungumzo mafupi katika ofisi yake katika jengo la Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.

 

Baada ya mazungumzo hayo, ujumbe wa Mahakama Zimbabwe ulitembelea Kituo cha Uendeshaji wa Mitandao kwenye jengo hilo la Mahakama kabla ya kuelekea katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke.

 

Akiwa katika Kituo hicho, Jaji Rais na ujumbe wake walipata nafasi ya kutembelea jengo hilo la Mahakama na kushangwa na ukubwa wake na mpangilio uliopo unaojumusha ngazi mbalimbali za Mahakama na wadau muhimu katika mnyororo wa utoaji haki, wakiwemo Maafisa Ustawi wa Jamii.

 

Pia alipata taarifa ya maboresho na kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa maboresho ya Mahakama nchini Tanzania na kupata ufahamu kuhusu safari ya Mahakama kidijitali.

 

Katika siku ya pili, Kiongozi huyo wa Mahakama Zimbabwe alirudi katika Kituo hicho Temeke kupata ufahamu wa masuala mbalimbali ya Mahakama na uunganishaji wa mtandao kwa ngazi zote za Mahakama.

 

Baadaye mchana, Mhe Dube alimtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ofisini kwake katika jengo la Mahakama ya Rufani na kujadiliana naye masuala mbalimbali ya kimahakama.

 

Jaji Kiongozi wa Zimbabwe na ujumbe wake katika siku ya tatu ya ziara yake alitembelea Kituo cha Usuluhishi cha Mahakama Kuu ambapo alionesha kuvutiwa na namna kinavyofanya kazi.

 

Mhe. Dube siyo kiongozi wa kwanza wa Mahakama kutoka nchi mbalimbali duniani kuitembelea Mahakama ya Tanzania. Viongozi wengine ambao wameshaitembelea Mahakama ya Tanzania kwa miaka ya hivi karibuni ni Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owiny-Dollo ambaye aliwasili nchini tarehe 24 Mei 2022 kwa ziara ya siku tatu.

 

Wengine ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt.Flavian Zeija ambaye aliwasili nchini ltarehe 15 Agosti, 2023 kwa ziara ya siku tano na Naibu Jaji Mkuu na Makamu wa Rais wa Mahakama ya Upeo ya Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Yang Linping ambaye tarehe 1 Novemba, 2023.




Jaji Rais wa Mahakama Kuu Zimbabwe, Mhe. Mary Dube (kulia) akiwa na Kaimu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Projestus Kahyoza wakiwa katika chumba maalum cha wageni kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere kabla ya kuondoka nchini kuelekea Harare.



Hakimu Mkazi, Mhe. Mary Kallomo (kushoto) kwa heshima mkubwa akisalimiana na Jaji Rais wa Mahakama Kuu Zimbabwe, Mhe. Mary Dube kabla ya kuondoka nchini.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni