Alhamisi, 30 Novemba 2023

WANANCHI MOROGORO WAPEWA ELIMU YA USULUHISHI

Na. Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro

 

Wananchi waliofika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kilichopo mkoani hapa wamepewa elimu ya masuala ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.

 

Elimu hiyo ambayo ilitolewa jana tarehe 29 Novemba, 2023 ililenga kuwasaidia wateja hao kujua umuhimu wa kutatua migogoro kwa njia hiyo.

 

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Teresia Kaniki alisema kuwa ni vyema kukubali njia hii ya usuluhishi kuliko kuvutana katika vyombo vya mamlaka, ikiwemo Mahakama.

 

Alisema kuwa kesi inapofikishwa mahakamani na kufikia hatua ya kutolewa maamuzi (hukumu) aliyeshindwa anakuwa kakosa kila kitu wakati aliyeshinda anakuwa amepata kila kitu, wakati katika njia ya usuluhishi wote wangeondoka na kitu na pia uhusiano unaendelea kuwepo baina ya pande zote mbili.

 

Katika kipindi hicho, wananchi walipata wasaa wa kuuliza maswali na kupatiwa majibu na Mahakimu mbalimbali waliokuwepo.

 

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Livin Lyakinana alitumia nafasi hiyo kuwataka wateja hao kushiriki katika maonesho ya wiki ya sheria mara yatakapotangazwa kwa kuwa kupitia maonesho hayo elimu pana zaidi hutolewa na mwananchi hupata wasaa mzuri wa kujifunza.

 

Sanjari na hilo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor alitumia nafasi hiyo kujitambulisha kwa wateja hao na kuwasisitiza kuuliza maswali kulingana na mada iliyofundishwa. 

 

Jaji Mansoor alitangaza kuwa kuanzia sasa elimu hiyo itakuwa ikitolewa mara moja kwa wiki siku ya Jumatano. Mabadiliko hayo ni baada ya takwimu kuonesha kuwa elimu hiyo imewafikia sehemu kubwa ya wananchi wa Morogoro.



 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor akizungumza na wananchi (hawapo pichani) wakati akitoa elimu ya Sheria kwa wateja hao waliofika kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro.


 

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Livin Lyakinana akizungumza wakati wa kutoa elimu ya msingi ya sheria kwa wateja waliofika kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro kwa ajili ya masuala mbalimbali.


 


Kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Livin Lyakina na kushoto kwake ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Teresia Kaniki wakati wakijibu masuala mbalimbali ya wananchi katika kipindi cha elimu ya msingi ya sheria inayotolewa ndani ya Kituo hicho.


 


Mmoja wa wananchi akiuliza swali wakati wa kipindi cha elimu ya msingi ya Sheria kwa Wananchi.

 


Wananchi mbalimbali wakifuatilia elimu.


 

 

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni