Na. Innocent Kansha – Mahakama
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel amesema Mahakama ya
Tanzana imeanzisha mkakati madhubuti wenye lengo la kuimarisha utoaji haki kwa
mashauri yanayohusu miliki ubunifu.
Akizungumza katika mkutano na
waandishi wa habari leo tarehe 30 Novemba 2023 Ofisini kwake jijini Dar es
salaam Prof. Ole Gabriel amesema Miliki Ubunifu ni eneo nyeti linalogusa nyanja zote za maisha
ya kila siku ya binadamu
na ni chachu ya ukuaji
wa biashara, teknolojia, uchumi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
“Mahakama ya Tanzania kwa
kulitambua hilo na pia kwa kutambua kuwa ni
mdau mkubwa katika
kulinda miliki ubunifu imechukua hatua madhubuti
za kuhakisha inaimarisha utoaji haki kwenye eneo hilo”, amesema Mtendaji Mkuu
Prof. Ole Gabriel.
Prof. Ole Gabriel amesema, kwa kipindi
cha miaka mitano
Mahakama ya Tanzania, imepiga
hatua kubwa sana katika kuboresha utoaji haki eneo la mashauri yanayohusu miliki ubunifu kwa kushirikiana na Shirika la
Miliki Bunifu Duniani ‘World Intellectual Property Organization’ (WIPO)
Mtendaji Mkuu huyo ametaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa
ni pamoja na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na
WIPO wamekwisha andaa miongozo juu ya haki miliki(Copyright), alama za biashara
(trademarks), hataza (patent) na maumbo bunifu (Industrial design). Miongozo
hiyo inatumiwa na waheshimiwa Majaji na Mahakimu kama rejea pale wanapokuwa
wanaendesha na mashauri yanayohusu miliki ubunifu.
Prof. Ole Gabriel amesema, kuanzia
mwaka 2022 hadi 2023 Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO) lilitoa ufadhili
kwa Majaji na Mahakimu 250 kwa lengo la kusoma masomo hayo kwa njia ya masafa
‘Distance Learning Course’. Mafunzo hayo ya masafa yameongeza uelewa mkubwa kwa
washiriki hususani katika eneo la miliki ubunifu.
“Jambo hili linadhihirisha kuwa
Mahakama ya Tanzania hivi sasa ina Majaji na Mahakimu wengi waliobobea kwenye
eneo hili na wameiva katika kutoa huduma bora kwa mashauri yanayohusu miliki
ubunifu na imesaidia kutoa elimu hii kwa makundi mbalimbalimbali wakiwemo
wabunifu, wafanyabiashara, makampuni, wamiliki wa viwanda”, ameongeza Prof. Ole
Gabriel
Mtendaji Mkuu huyo akataja
mafanikio kuwa, Mahakama kwa kushirikina na WIPO wamekuwa wakifanya makongamano
ya miliki ubunifu. Mapema mwaka huu, mwezi Machi kwa kushirikiano na WIPO Mahakama ilifanikiwa kufanya
kongamono kubwa la miliki ubunifu kwa njia ya mtandao. Mkutano huo ulihudhuriwa na Majaji na
Mahakimu wa Tanzania zaidi ya 150, wataalamu kutoka WIPO na Majaji waliobobea
kwenye eneo hili la Miliki Ubunifu kutoka Berkeley Judicial Institute, Chuo
Kikuu cha London, Marekani, Ulaya, na Kenya.
Mtendaji Mkuu alisema, mafanikio mengi yaliyofikiwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na WIPO ni kuandaa muhtasari wa maamuzi mbalimbali ya Mahakama ya Tanzania kwa lengo la kuwarahisishia Majaji na Mahakimu kufanya rejea ya maamuzi ya Mahakama kwa wepesi wakati wa kufanya tafiti za kisheria zinazohusiana na mashauri ya miliki ubunifu.
Prof. Ole Gabriel ameongeza kuwa, maamuzi ya Mahakama ya Tanzania yanachapishwa kwenye mtandao mkubwa dunia WIPO Lex. Uchapishwaji wa Maamuzi hayo kwenye mtandao huo umeitambulisha kazi nzuri inayofanywa na Majaji wa Tanzania duniani na umewawezesha Majaji wa nchi mbalimbali kupata maamuzi yanayotolewa na Mahakama ya Tanzania kwenye eneo hilo.
“Majaji na Mahakimu wa Tanzania wameweza pia kupata kwa urahisi maamuzi ya Nchi zingine kupitia mtandao huo na hivi sasa Mahakama ipo mbioni kuunganisha mfumo wa WIPO Lex na tovuti ya Mahakama ili Majaji na Mahakimu waweze kupata kwa urahisi maamuzi mbalimbali ya nchi zingine kupitia mtandao huo utakaoukuwa unaonekana kwenye tovuti ya Mahakama ya Tanzania”, ameongeza Mtendaji Mkuu.
Shughuli mbalimbali zinazofanywa na
WIPO kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania hivi sasa zimeshawanufaisha
Majaji na Mahakimu takriban 815 na hii imeweka Mahakama ya Tanzania katika
nafasi nzuri ya kushughulikia vema mashauri yanayohusu hakimiliki (copyrights),
alama za Biashara (Trademarks), hataza (Patents) na maumbo bunifu (Industrial
designs).
Matendaji Mkuu huyo akatoa wito kwa wadau kuwa Mahakama ya Tanzania imeshajenga uwezo wa ndani, inapenda kutoa wito kwa wadau wa Miliki Ubunifu nchini kushirikiana na Mahakama kutoa elimu kwa umma juu ya elimu ya hakimiliki, alama za biashara, hataza na maeneo mengine yanayohusu miliki ubunifu.
“Hapa nchini tunao wabunifu, wasanii na wafanyabiashara wengi ambao kazi zao hazilindwi kisheria kutokana na uelewa mdogo wa masuala yanayohusu miliki ubunifu na namna gani ya kupata haki zao pale zinapovunjwa”, amesisitiza Prof. Ole Gabriel.
Prof. Ole Gabriel akahitimisha kwa kueleza kuwa, Mahakama ya Tanzania ina dhamira ya kuhakikisha kuwa wabunifu, wafanyabishara, makampuni na viwanda hawakutani na kikwazo chochote kwa mambo yanayohusu haki zao haswa zile ambazo Mahakama kwa namna moja au nyingine inashiriki kuzilinda. Mahakama ina dhamira kubwa ya kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji kwa ustawi wa Taifa letu.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo tarehe 30 Novemba 2023 Ofisini kwake jijini Dar es salaam akieleza mikakati ya Mahakama ya Tanzania kuimarisha mambo yanayohusu Miliki Bunifu na mafanikio ya WIPO Tanzania ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni