Ijumaa, 1 Desemba 2023

WATUMISHI MAHAKAMA MKOA WA SINGIDA WASISITIZWA UHIFADHI NA UTUNZAJI WA MAZINGIRA

Na Eva Leshange- Mahakama, Singida

 Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt Juliana Masabo amewasisitiza watumishi wa Mahakama mkoani Singida kuyatunza vema mazingira yanayowazunguka kwa faida yao na wananchi wanaopata huduma.

Mhe. Dkt. Masabo aliyasema hayo hivi karibuni katika ziara yake ya ukaguzi wa shughuli za Mahakama katika Wilaya ya Manyoni ambapo aliwaambia watumishi hao kuhakikisha wanatunza vizuri bustani na kupanda miti katika maeneo ya Mahakama.

“Nimefurahi na kuvutiwa na ubunifu wa utunzaji wa mazingira wilayani Manyoni hasa kwa kila mtumishi kupewa mti wa kuutunza ni jambo jema na la kulichukua na ndio ukawa mkakati wa Kanda kwa ujumla,” alisema Jaji Masabo.

Aidha, aliwapongeza Mahakimu pamoja na watumishi kwa kazi nzuri wanayofanya hasa katika usikilizwaji wa mashauri, amewataka kuongeza kasi zaidi na kuhakikisha hakuna kabisa mashauri ya mlundikano (Backlog Free).

Aliwapongeza pia Mahakimu kwa kutumia ya Mfumo mpya wa Kieletroniki wa usajili na usikilizaji wa mashauri Mahakamani (Advanced e-Case Management System) na kuwasihi kuwa, changamoto wanazokutana nazo zinafanyiwa kazi na zitaisha wawe na subira kwani ni kipindi cha mpito.

Katika ukaguzi huo Dkt. Masabo alitoa barua za pongezi kwa Wilaya ya Singida na Manyoni kwa kuweza kupata hati nyingi za viwanja vya Mahakama, ambapo Wilaya ya Singida katika Kata 49 wamefanikiwa kupata hati 38, Wilaya ya Manyoni katika Kata 17 wamepata hati 16.

Kufuatia hatua hiyo ya upatikanaji wa viwanja, Jaji Mfawidhi huyo alielekeza kupandwa miti katika viwanja hivyo ili kulinda mipaka.

Katika ziara yake ya siku mbili (2) Mkoani Singida, alipata pia fursa ya kutembelea Magereza ya Wilaya Singida, Iramba na Manyoni na kusikiliza kero za wafungwa na mahabusu. Aidha, aliwapongeza wadau wote wa haki jinai kwa kazi nzuri wanayofanya kwani hali ya magereza ilionekana ni nzuri hakuna msongamano na changamoto zote zilizoibuliwa walizitolea majibu.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt Juliana Masabo (aliyeketi katikati) akizungumza jambo wakati wa ziara yake ya ukaguzi aliyofanya mkoani Singida.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe.Allu Omary Nzowa akisoma taarifa ya utekelezaji  mnamo mbele ya Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt Juliana Masabo aliyeketi mbele (kushoto) pembeni yake ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Sylivia Lushasi.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Manyoni, Mhe. Alisile Mwankejela akisoma taarifa mbele ya Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo alipowasili kituoni hapo kwa ajili ya ziara ya ukaguzi mnamo tarehe 30 Novemba, 2023.

Sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida wakimsikiliza Jaji Mfawidhi (hayupo katika picha) alipofanya ziara ya ukaguzi kituoni hapo.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya Manyoni wakimsikiliza Mhe. Dkt. Masabo (hayupo katika picha) alipofanya ziara ya ukaguzi wilayani hapo.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni