Ijumaa, 1 Desemba 2023

MKANDARASI UJENZI WA JENGO LA 'IJC' SIMIYU AKABIDHIWA ENEO LA MRADI

  • Ujenzi kuanza tarehe Mosi Desemba, 2023

Na Naumi Shekilindi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu

Makabidhiano ya eneo kwa ajili ya kuanza kwa Mradi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Mkoa wa Simiyu yamefanyika huku yakishuhudiwa na Wawakilishi kutoka Makao Makuu ya Mahakama na Viongozi wa Mahakama mkoani Simiyu huku utekelezaji wake ukitarajiwa kuanza rasmi leo tarehe 01 Desemba, 2023.

Makabidhiano hayo yalifanyika tarehe 27 Novemba, 2023 huku yakishuhudiwa na Mhandisi Peter Mrosso, ‘QS’ Deogratius Lukansola, Mtendaji Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mhe. Martha Mahumbuga, Mhandisi Mshauri (Consultant) Bw. Humphrey Massawe, Mkandarasi, Bw. Riziki Nkona pamoja na timu yake. 

Mwenyekiti wa kikao hicho cha makabidhiano, Mhandisi Mshauri Humphrey Massawe alielezea kuwa Mradi huo ni wa muda wa miezi tisa (9) na utaanza rasmi tarehe 01 Desemba, 2023 na unatarajiwa kukamilika tarehe 31 Agosti, 2024 na kukabidhiwa mnamo tarehe 01 Septemba, 2024. 

Mhandisi Massawe aliongeza kuwa, “ikumbukwe kuwa, zile siku 14 ambazo Mkandarasi anatakiwa kupewa kabla ya kuanza ujenzi zitakua ndani ya miezi hiyo tisa (9) kutokana na muda wa Mradi kuwa mfupi.” 

Mhandisi Massawe alisisitiza mambo mbalimbali kwa Mkandarasi wa Mradi kwamba, endapo Mkandarasi atahusisha Kampuni nyingine kufanya baadhi ya kazi basi atatakiwa kuleta taarifa (profile) za Kampuni hiyo kwa ajili ya upekuzi na kujiridhisha. 

Pia alisisitiza jinsi ya kuratibu uzalishaji na utupaji taka; kwamba lazima waainishe aina ya taka wanazozalisha na wapi wanatupa ili kuepuka madhara kwa watu wanaoishi au kuzunguka eneo hilo.

Mwenyekiti wa kikao alimuelekeza Mkandarasi kujisajili Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Halmashauri- Idara ya Zimamoto kabla hawajaanza shughuli zao za ujenzi.

Mhandisi Mshauri na Mkandarasi walikubaliana kufanya kazi usiku na mchana ili kukidhi Mradi kwa muda waliopewa na Mahakama, pia wamekubaliana kuwepo kwa vikao vya kila mwezi ambavyo vitahusisha wadau  wote wa Mradi  na vikao vya ‘technical’ ambavyo vitakuwa vinafanyika mara kwa mara kwa ajili ya kuwepo ufanisi wa kazi.

Aidha, Mwenyekiti alihitimisha kwa kumuasa Mkandarasi pamoja na timu yake kuzingatia ubora (quality control) katika hatua zote za ujenzi.

Naye, Afisa Mazingira kutoka Makao Makuu ya Mahakama, Bw. Castory Kyula alisisitiza  Wakandarasi juu ya utunzaji wa mazingira na uthibiti wa kelele na vumbi katika kipindi chote cha utekelezaji wa Mradi.

Kwa upande wake, Mtendaji Mahakama Mkoa Simiyu Bw. Gasto Kanyairita aliahidi kuwapa ushirikiano wakandarasi na kufanya mawasiliano na taasisi zote zinazo husika kutoa vibali ndani ya Mkoa wa Simiyu.


Makabidhiano ya mkataba kwa ajili ya ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Simiyu kati ya Mkandarasi, Bw. Riziki Nkona na Mtendaji Mahakama Mkoa Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita. Makabidhiano ya 'site' hiyo yalifanyika tarehe 27 Novemba, 2023.
Picha ya pamoja na timu nzima inayohusika na ujenzi wa IJC wakati wa makabidhiano ya cheti baada ya kukabidhiana site.

Wajumbe wakimsikiliza Mwenyekiti wakati wa  kikao cha makabidhiano, Mhandisi Mshauri Humphrey Massawe kabla ya  makabidhiano ya eneo 'site' litakapojengwa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Simiyu.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni