Ijumaa, 1 Desemba 2023

JAJI MKUU AWAONYA MAWAKILI WANAOTUMIA LUGHA ZINAZOKIUKA MAADILI MAHAKAMANI

Na. Innocent Kansha - Mahakama.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.  Ibrahim Hamis Juma amesema kapokea malalamiko kutoka kwa majaji kuhusu mawakili wa kujitegemea wanaowasilisha hoja zao Mahakamani kwa kutumia lugha zinazokiuka maadili ndani ya Mahakama na amekitaka Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kuchukua hatua kabla ya majaji kulalamika.


Akizungumza katika sherehe ya 69 ya mahafali ya kuwakubali na kuwapokea mawakili wapya wapatao 279, idadi hiyo ikijumuisha wanawake 118 na wanaume 161 na kufanya jumla ya mawakili kufika 11,916 kutoka idadi ya awali ya mawakili 11,636 katika hafla iliyofanyika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo tarehe mosi Desemba, 2023, Jaji Mkuu Prof. Juma amesema, uwakili ni taaluma yenye heshima, vitendo, kauli sahihi na mihuli vyote vinatakiwa kuwa na heshima.


"Nimekuwa nikipokea malalamiko mengi kutoka kwa Majaji, malalamiko yanayokiuka maadili hasa pale mawakili wa kijitegemea wanapowasilisha hoja zao mahakamani kwa kiburi, jeuri na kutumia lugha zisizostahili, malalamiko mengi yanakiuka kanuni ya 92 ya kanuni ya maadili ya mawakili, ukiwa unajibizana na Jaji au Hakimu unakuwa unakiuka moja kwa moja  kanuni yenu ambayo inawaongoza, wajibu wa kuheshimu Mahakama  na kutunza lugha tunazotumia si hapo Tanzania tu, pengine sheria zetu zinanyima uhuru wa kusema tu unachotaka mahakamani, naomba jambo kama hilo likitokea sio Jaji alalamike bali mawakili wenyewe wachukue hatua " amesema Jaji Mkuu

Mhe. Prof. Juma amesema kitendo kimoja tu cha ukiukwaji wa maadili ambacho pengine kimefanywa na wakili mmoja tu Tanzania, kinaweza kuharibu taswira yote ya taaluma ya uwakili nchini.

"Eneo hili mnatakiwa muwe waangalifu, tendo lolote la wakili mmoja kukiuka maadili, linaweza kuchafua taswira ya soko la ajira la mawakili wa Tanzania kwasababu siku zote inaweza kutumika kama ndiyo mfano wa hali ya maadili kwa mawakili wa Tanzania" amesema Mhe. Prof. Juma

"Hii ni Karne ya habari, chochote kinachofanyika leo kinaweza kusambaa kwa haraka zaidi na kwa muda mfupi kwa hiyo tuwe wangalifu sana katika eneo la maadili kwasababu kinaweza kukuchafua wewe na taswira ya taaluma yote ya mawakili Tanzania" ameongeza 

Jaji Mkuu Prof. Juma amesema, kama ilivyo kwa Majaji na Mahakimu, Uwakili ni taaluma inayoheshimika sana na ni taaluma ya heshima hivyo vitendo, kauli na myenendo yeo yote iwe ya heshima kwasababu  wakiruhusu mihuri yao kutumiwa vibaya inapunguza hadhi na heshima ya uwakili.

"Saini zenu mnazosaini ni heshima, nguvu ya taaluma yetu inatokana na heshima, jamii ikikosa heshima kwetu inakuwa haina maana, siku zote tuwe na tahadhari kubwa ya kutambua kwamba mamlaka yanu ni makubwa sana" amesema Mhe. Prof. Juma 

Jaji Mkuu huyo amesema, kuna kanuni za kitaaluma zinazotakiwa kuzingatiwa zinazosaidia kusafisha taaluma ya mawakili. Kila taaluma duniani inatarajiwa kujidhibiti na kuwadhibiti wanataaluma wake kwenye masuala ya nidhamu kabla chombo chochote cha nje kuja kumsimamia nidhamu kwa kujisimamia wenyewe.

 

Mhe. Prof. Juma amesema Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kikifanya hivyo hakuna mtu atakayewaingilia kikiwa kinajichukulia hatua na kudhibiti wanachama wake katika masuala ya kinidhamu, tofauti na sasa chombo kikichukua hatua mawakili wanakusanyika kuteteana.


"Sasa Chama chenyewe kichukue hatua za kinidhamu , tumieni mamlaka mlinayo kujidhibiti wenyewe, tumieni kanuni zenu za uwakili za mwaka 2022 kujidhibiti, ni wajibu wenu kuonyesha nidhamu kwa Mahakama.


Mhe. Prof. Juma aliwataka mawakili hao kuwa na umakini wa kuchagua mawakili wa kuwa mfano wa kuigwa. Amesema wakili wa kuigwa siyo lazima awe mwandamizi tu bali wachague wale ambao watakao wahamasisha, kuwafundisha na kuwapa hamasa ya kuendelea katika fani hiyo, kuwapa miongozo na mrejesho wa kazi wanazofanya.


Pia aliwataka mawakili hao kuwa na tabia ya kujisomea kwani hakuna ukomo na kwamba wapo miongoni mwao ambao tangu walipohitimu chuo Kikuu hawajawahi kusoma kitabu hata kimoja.


“Acheni tabia za kukumbatia madesa someni kuongeza maarifa mapya ili muweze kukabiliana na ushindani wa karne ya 21, mambo mengi hivi sasa yapo hata mitandao”, ameongeza Jaji Mkuu.


Katika jambo lingine, Jaji Mkuu aliwataka mawakili hao kuwa na uwezo wa kufanya kazi kwani wamekuwa mawakili baada ya kuonesha uwezo Sekondari, Chuoni, shule ya sheria kwa vitendo, Baraza la Elimu ya Sheria na kusailiwa mbele ya Jaji Mkuu.


Jaji Mkuu amesema, kanuni za maadili ya uwakili zinataka huo uwezo muendelee kuwanao na msipojiendeleza na kukabiliana na hali ya mabadiliko itawaacha nyuma na mtakuwa mmekiuka maadili na kupoteza uwezo unaozungumzwa kwenye maadili.


Katika jambo lingine Jaji Mkuu amewasihi mawakili hao kuendana na hali ya mabadiliko ya teknolojia ambayo hayawasubiri mawakili. Amesema taaluma ya sheria na mawakili haiwezi kukwepa mapinduzi ya viwanda ambayo tayari yameshaingia mahakamani.


"Tumeanza kujifunza utaratibu mpya wa kuratibu na kumsimamia mashauri mahakamani  kwa njia ya mtandao , mfumo huu ni muhimu sana , ulikuja kuchukua nafasi mfumo uliokuwepo ambao ulizidiwa , unafaida nyingi, zipo changamoto kadhaa ambazo zinafanyiwa kazi , lakini faida zitakazopatikana ni kubwa kuliko changamoto ambazo tunazotumia kuimarisha huu mfumo" amesema Jaji Mkuu.


Kabla ya kuzungumza hayo aliwakubali na kuwatunuku vyeti mawakili hao 279.


"Kwa mamlaka niliyopewa na Sheria ya mwakili sura ya 341 Toledo la 2019, kifungu cha 8(3) nina tamka kwamba wale wote ambao majina yao yamesomwa hapa wamekubaliwa kuwa mawakili na wamerodheshwa rasmi kwenye orodha ya mawakili kuanzia leo Desemba Mosi,"amesema Jaji Mkuu. 


Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa serikali Mhe. Dkt Eliezer Mbuki Feleshi akitoa nasaha zake aliwataka mawakili hao kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali wanapotekeleza majukumu yao. 


Dkt. Feleshi amewakumbusha kwamba mawakili ni maofisa wa Mahakama hivyo wamepewa dhamana ya kuisaidia Mahakama katika utowaji haki kwa wakati na usawa kwa wote kwani ni jukumu lao kuhakikisha mahakama inatenda haki. 

Jaji Feleshi ameongeza kuwa, kanuni ya 92 ya kanuni za maadili ya amawakili inahusu myenendo ya mawakili, inakataza hujuma kwa Mahakama katika utowaji haki ikiwemo kutoa taarifa za uongo na kueleza jambo litakaloipotosha Mahakama katika kufika maamuzi ambayo yasingefikiwa kama si upotoshaji huo, usingekuwepo.

Dkt. Feleshi amesema kanuni hizo pia zinatakaza mawakili kutoa maoni ya kesi iliyo mahakamani katika mambo ambayo yanaweza kuathiri matokeo ya kesi husika.

"Mawakili mkumbuke kuwa tasinia ya uwakili ni nyeti, mnapaswa kuzingatia kanuni na miongozo mbalimbali iliyowekwa mnapotekeleza majukumu yenu hususani kanuni zote za maadili na myenendo ya kazi zenu" amesema Jaji Feleshi

…..Kumekuwa na tuhuma kwa baadhi ya mawakili wa kujitegemea kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa baadhi yetu, kuwasaliti wateja wao kwa kupokea rushwa, kutoudhuria mahakamani, kutotunza siri za mteja, kutokuwa na mawasiliano mazuri kati ya wakili na mteja, kutumia mihuri isiyo halali”, ameongeza Jaji Feleshi 

Mwanasheria Mkuu huyo amesema mabadiliko ya sheria ya mawakili ya mwaka huu imeeleza kuwa wakili atakayefanya kazi bila kuwa na sifa ya uwakili atapewa adhabu ya kutozwa faini ya shilingi milioni tano na isiyozidi milioni 20 au kifungo cha mwaka mmoja gerezani mpaka miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

"Nitumie fursa hii kuwaonya wale wote wanaofanya vitendo hivi vya kinyume na utaratibu kuacha mara moja" alisema Dokta Feleshi.

Naye, Rais wa Chama cha wanasheria Tanganyika (TLS) Wakili Msomi Harold Sungusia akuzungumza katika hafla hiyo, amesema wako katika oparesheni ya kupambana na mawakili vishoka katika maeneo yote na kuwaasa mawakili hao kuzingatia maadili na kwamba taaluma hiyo inahitaji kujitambua, kujitambua na kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa.

"Kuwa wakili msomi, siyo matangazo ya majigambo na majivuno kama upatu uvumao, bali ni haki ya mhusika kuipenda kusoma kujitafutia taarifa na Maarifa sehemu sahihi, kujielimisha, kujikosoa, kujituma na kushirikiana na mawakili wengine katika kuboresha tasnia hii" amesema Rais huyo 

Mhe. Sungusia ameongeza kuwa, wanajitahidi kusimamia vyema maadili, mihuli holela na wanahakikisha mihuli ya mawakili haughushiwi. Kama chama wameanzisha Kituo Suluhishi cha Migogoro ya ndani na nje ya nchi ili kupunguza msongamano wa kesi Mahakamani.

Aliwataka mawakili wapya kusimamia haki za wateja bila kupendelea wala kuogopa.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.  Ibrahim Hamis Juma akitoa hotuba wakati wa mahafali ya kuwakubali na kuwapokea mawakili wapya katika hafla iliyofanyika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo tarehe mosi Desemba, 2023,

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.  Ibrahim Hamis Juma (wa nne kutoka kushoto) akiwa na jopo la Majaji akipokea heshima kutoka kwa mawakili wapya aliowakubali na kuwapokea kuingia kwenye orodha ya daftari la mawakili

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa tamko rasmi kwa mamlaka niliyopewa na Sheria ya mwakili sura ya 341 Toledo la 2019, kifungu cha 8(3) nina tamka kwamba wale wote ambao majina yao yamesomwa hapa wamekubaliwa kuwa mawakili na wamerodheshwa rasmi kwenye orodha ya mawakili

Jopo la Mwasheria Mkuu wa Serikali likipokea heshima kutoka kwa mawakili wapya aliokubaliwa na kuwapokelewa kuingia kwenye orodha ya daftari la mawakili.

Jopo la Balaza la Shule ya Sheria likipokea heshima kutoka kwa mawakili wapya aliokubaliwa na kuwapokelewa kuingia kwenye orodha ya daftari la mawakili.

Sehemu ya mawakili wapya wakila kiapo cha maadili mara baada ya kukubali na kupokelewa 


Mwanasheria Mkuu wa serikali Mhe. Dkt Eliezer Mbuki Feleshi akitoa hotuba wakati wa hafla ya kuwakubali na kuwapokea mawakili wapya

Sehemu ya mawakili wapya wakitoa heshima mara baada ya kukubaliwa na kupokelewa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo pichani).


Sehemu ya mawakili wapya wakitoa heshima mara baada ya kukubaliwa na kupokelewa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo pichani).


Sehemu ya mawakili wapya wakipokea maelekezo kutoka kwa kaimu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Projustus Kahyoza mara baada ya kukubaliwa na kupokelewa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo pichani).

Sehemu ya mawakili wapya wakipokea maelekezo kutoka kwa kaimu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Projustus Kahyoza mara baada ya kukubaliwa na kupokelewa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo pichani).

Sehemu ya wazazi, walezi na wananchi waliohudhuria hafla hiyo ya kuwakubali na kuwapokea mawakili wapya


Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania waliohudhuria hafla hiyo ya kuwakubali na kuwapokea mawakili wapya.


Sehemu ya Majaji wastaafu wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania waliohudhuria hafla hiyo ya kuwakubali na kuwapokea mawakili wapya.

Mwanasheria Mkuu wa serikali Mhe. Dkt Eliezer Mbuki Feleshi (kulia) na Wakili Mkuu wa Serikali Mhe. Dkt. Boniphace Luhende (kushoto) wakifuatilia hotuba ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo pichani)

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na jopo la Majaji wakiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya mawakili walioingia rasmi kwenye orodha ya daftari la mawakili mara baada ya kuskubali na kupokelewa.

Picha na Innocent Kansha - Mahakama



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni