Ijumaa, 24 Novemba 2023

MAJAJI WAPYA KANDA YA DAR ES SALAAM UTAWAPENDA

·Kasi umalizaji mashauri waliyopangiwainashangaza

·Wananchi wamlilia Jaji Kiongozi asiwahamishe

·Jaji Mfawidhi awamiminia sifa, awaambia wamtangulize Mungu

Na. FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Majaji watano wapya waliokuwa wanahudumu katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam kabla ya kupangiwa vituo vyao vya kazi wamefanikiwa kuondosha jumla ya mashauri 120 ndani ya mwezi mmoja kabla ya kupangiwa vituo vya kazi.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 24 Novemba, 2023 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi kwenye hafla fupi ya kuwaaga Majaji hao iliyofanyika kwenye moja ya kumbi za mikutano katika jengo la Mahakama Kuu jijini hapa.

“Nichukue nafasi hii kuwapongeza sana kwa kazi nzuri mliyowafanyia Watanzania katika kipindi hiki kifupi. Kasi mliyokuwa nayo katika kumaliza mashauri siyo ya kawaida, tunawashukuru sana kwa kuendelea kuiheshimisha Mahakama,” amesema.

Jaji Mfawidhi amefafanua kuwa hapo awali Majaji hao, Mhe. Anold Kirekiano, Mhe. Said Ding’ohi, Mhe. Griffin Mwakapeje, Mhe. Abdallah Gonzi na Mhe. Kamazima Idd, walitakiwa kupewa majalada 20 kila mmoja, lakini kutokana na wingi wa mashauri katika Kanda ya Dar es salaam wakaongezewa hadi kufikia majalada 25.

 

“Majaji hawa wamefanya maajabu kwa kweli, walimaliza mashauri yote waliyopangiwa kabla ya muda wao na hivyo kila Jaji akaongezewa tena majalada kati ya mawili na matatu na haya nayo wakamaliza

 

“Hivyo, badala ya kumaliza mashauri 100 kama ambavyo ilipangwa awaliMajaji hawa wamemaliza mashauri 120 na mashauri 12 yanasubiri hukumu. Hii ina maana kuwa wamemaliza mashauri 32 zaidi ya yale waliyokuwa wamepangiwa. Kwa, kweli wametoa msaada mkubwa katika kupunguza idadi ya mashauri kwenye Masjala ya Dar es Salaam,” amesema.

 

Mhe. Maghimbi amesema pamoja na ugumu wa kazi iliyokuwa mbele yao, Majaji hao wameshughulikia pia mashauri ya mauaji katika hatua ya usililizaji wa awali (preliminary hearing) na kutoa maamuzi ya mifano kwenye masuala ya utoaji wa adhabu.

 

Jaji Mfawidhi amewaomba Majaji hao kumtanguliza Mungu kwa kila wanachofanya kule wanakoenda ili waweze kutenda haki inayostahili kwa wananchi kwani dhamana waliyopewa ni kubwa na anaamini watatekeleza majukumu waliyopewa katika vituo vyao kwa umahiri mkubwa.

 

Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Majaji wengine wa Mahakama Kuu waliopo Dar es Salaam, akiwemo Mhe. Mohamed Gwae, Mhe. Butamo Philip, Mhe. Elizabeth Mkwizu, Mhe. Ayoub Mwenda, Mhe. Awamu Mbagwa na wengine kutoka Kanda zingine, akiwemo Mhe. David Ngunyale na Mhe. Gabriel Malata.

 

Walikuwepo pia Naibu Msajili Mwandamizi, Mhe. Sudi Fimbo na Naibu Msajili Joseph Luambano pamoja na Mtendaji Moses Mascara. Viongozi hao kwa pamoja wamewamiminia sifa Majaji hao wapya kwa kazi kubwa iliyotukuka waliyoifanya kwa kipindi kifupi.


Kadhalika, Viongozi hao wamewaasa kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa uaminifu mkubwa na kuzingatia sheria katika kufikia maamuzi ya haki kwenye mashauri yote yatakayoletwa mbele yao.

 

Kwa upande wao, Majaji hao wameushukuru Uongozi wa Mahakama katika Kanda ya Dar es Salaam na watumishi wote kwa ujumla kwa ushirikiano walioupata kwa kipindi chote cha majaribio, jambo lililowawezesha kutekeleza majukumu yao waliyopewa bila changamoto zozote. 

Baada ya hafla hiyo, baadhi ya wananchi waliokuwa katika jengo la Mahakama Kuu wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuteua Majaji wachapakazi na wanaoipenda kazi yao.

“Mtu akitekeleza kazi yake kwa ufanisi ni ishara inayoonesha jinsi gani anaipenda kazi yake. Majaji hawa wamedhihirisha kuwa Rais Samia hajakosea kuwateua, kazi ambayo wameifanya kwa muda huu mchache imeonekana. Niwaombe Majaji wetu waendelee kuchapaka kazi ili Watanzania wapate haki zao stahiki kwa wakati,” mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Abdallah K. Abdallah amesema.

Naye mwananchi anayejiita kuwa yeye ni mpenda haki amemuomba Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani kuwabakiza Majaji hao katika Kanda ya Dar es Salaam ambayo inaongoza nchini kwa kuwa na wingi wa mashauri.

“Majaji hawa wameonesha njia nzuri na kweli ni wachapa kazi, kwa nini wasibaki hapa (Dar es Salaam) ili wasaidie kusukuma mashauri mengi yaliyopo? Mimi binafsi ninaami kwa mwendo walioanza nao, wakiunganisha nguvu na hao wengine wakongwe waliopo mashauri yatamalizika kwa wakati sahihi,” amesema.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (juu na chini) akizungumza wakati wa hafla fupi ya kuwaaga Majaji watano waliokuwa wanahudumu kwa muda mahakamani hapo.



Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Butamo Philip akisisitiza jambo alipokuwa anaongea kwenye hafla hiyo.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Said Ding’ohi akieleza jambo wakati wa hafla hiyo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Griffin Mwakapeje, ambaye ni miongoni mwa Majaji wapya waliokuwa wakihudumu katika Kanda ya Dar es Salaam akitoa nano la shukrani wakati wa hafla hiyo.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Kamazima Idd, ambaye ni miongoni mwa Majaji wapya waliokuwa wakihudumu katika Kanda ya Dar es Salaam akitoa nano la shukrani wakati wa hafla hiyo.

Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Sudi Fimbo akitoa neno la shukrani kwa Majaji hao wapya.

Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania (juu na chini) wakifuatilia mambo mbalimbali yaliyokuwa yanajiri kwenye hafla hiyo.

Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wapya (juu) wakikata keki katika hafla hiyo. Picha chini, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambao ni wakongwe nao hawakuwa nyuma kukata keki iliyokuwa imeandaliwa kwa aijli ya hafla hiyo.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (kushoto) akimkabidhi Mhe. Said Ding’ohi zawadi ya kikombe kama ishara ya shukrani kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kipindi cha majaribio.

Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wapya wakiwa wameshikilia vikombe ambavyo walikabidhiwa kama zawali kwenye hafla hiyo.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Griffin Mwakapeje (kulia) akimlisha keki Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi wakati wa hafla hiyo, huku Majaji wenzake wapya wakishuhudia tukio hilo.

Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa hafla hiyo.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni