Na. Innocent Kansha – Mahakama.
Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi kimeanzisha na kutekeleza programu ya
kuzitembelea taasisi za kifedha mkoani Dar es salaam kwa lengo la kubadilishana
uzoefu juu ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.
Akiongoza
ujumbe wa Kituo cha Usuluhishi kuzitembelea taasisi hizo za kifedha ikiwemo ya
Benki ya NMB na Benki ya CRDB ambao ni wadau wa nje wa Kituo hicho kwa nyakati
tofaouti hivi karibuni, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha
Usuluhishi Mhe. Zahra Maruma alisema, Kituo cha Usuluhishi kwa kutambua umuhimu
wa taasisi za kifedha katika kukuza uchumi endelevu ikiwa ni pamoja na kuyaishi
maudhui ya kauli mbiu ya wiki na siku ya sheria nchini ya mwaka 2023.
“Kituo
kinawajibu wa kusimamia na kutekeleza kauli mbiu hiyo isemayo Umuhimu wa
utatuzi wa migogoro kwa njia ya Usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu: wajibu
wa Mahakama na wadau, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa nguzo ya tatu ya Mpango
Mkakati wa Mahakama wa mwaka 2020/21 hadi 2024/25.
…ndiyo
uliopelekea kuandaliwa kwa kikao cha wadau wa nje ili kupata uzoefu wa vitu gani
vinakwamisha matumizi ya kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kutatua
migogoro inayohusisha mabenki na wateja wao kiasi ikapelekea kesi kukaa
mahakamani kwa muda mrefu na kufanya fedha zilizokopwa kutorudishwa kwa wakati
na hivyo kuathiri uchumi kwa kiasi kikubwa ”, alisisitiza Mhe. Maruma.
Jaji
Maruma alisema uzoefu wa ushughulikia migogoro ya Mabenki kwa njia ya usuluhishi
ulitolewa na kubainisha maeneo yafuatayo kuwa ndiyo chanzo cha matatizo
mathalani kutofuatwa kwa taratibu za ukopeshaji, kutopatikana kwa ridhaa ya
mwenza au mwenye umiliki katika mali inayowekwa kama dhamana na matendo ya kijinai
yanayohusika wakati wa taratibu za ukopeshaji fedha kupitia taasisi za kifedha.
Mhe.
Maruma aliendelea kuangazia maeneo mengine yenye dosari kama kutorudisha hati
baada ya mkopo kulipwa, kutoweka vizuri kumbukumbu za mikopo, kutopeana taarifa
za hatua mbalimbali zinazotakiwa kuchukuliwa katika mikopo chechefu na kutoa mkopo
wa pili kwa mtu bila uelewa na ridhaa ya mdhamini.
Jaji
Maruma aliongeza kuwa, kutoa notice kwa anuani isiyo sahihi au tofauti na
iliyotolewa wakati wa kusaini mkataba wa kukopa, kuuza mali bila kufuata hatua
za kisheria na usimamizi mbovu wa utekelezaji wa maamuzi ya benki na pia madalali
walioteuliwa kutosimamiwa ipasavyo chini ya kifungu cha 132 kifungu kidogo cha
nne(4) cha Sheria ya Ardhi.
Mhe.
Jaji Mfawidhi huyo, aliwasisitiza wadau hao wa nje juu ya faida za usuluhishi na katika kuchambua faida hizo alisema mara
nyingi zikiangaliwa asili za mahusiano ya kibenki, mikopo, muonekano wa wateja
wafikapo mahakamani ni wazi kuwa mashauri ya kibenki yana uwezekano mkubwa wa kumalizika
ndani ya muda mfupi na hivyo kuokoa pato la taifa.
Kwa upande wa Maafisa wa Benki walibainisha changamoto
wanazokutana nazo kutoka mahakamani kwamba, bado Mahakama inatoa nafasi kwa watu
ambao wameshakubaliana kumaliza kesi, kurudi tena mahakamani kufungua
mashauri tena Mahakama wakisikilizwa kwa viini au hoja zilezile.
“Hoja
za kutopatikana bei stahiki ya kuuzwa mali, taratibu kutofautiana huibuliwa
upya. Naiomba Mahakama kutoruhusu hii hali mara kwa mara tena madamu watu
wameshamaliza kesi kwenye usuluhishi maana inaporuhusiwa hujikuta mashauri
yanaenda tena mpaka Mahakama ya Rufani na kuchukua muda mrefu kutatua mgogoro”,
aliongeza Afisa wa Benki.
Afisa
huyo Benki, aliendelea kusema kuwa kesi zao nyingi sana zipo kwenye Mabaraza ya
Ardhi na Nyumba ya Wilaya ambayo huwa yanatoa Zuio (Injunctions) mara nyingi
sana. Akahoji ikiwa kama Mahakama kwa nafasi yake inaweza kuwasilisha hoja hiyo
kwa Mabaraza, kwani ni eneo ambalo wateja wengi wanalitumia vibaya ili
kukwamisha mabenki kurudisha fedha zilizokopwa kupitia dhamana zilizowekwa na
kuongeza kuwa kitendo hicho kimekuwa kikikatisha tamaa sana.
Kwa
nyakati tofauti wajumbe hao kutoka taasisi za kifedha waliongeza kuwa mkwamo
mwingine unatokana na suala la uwakilishi (Representation) mara nyingine linakwamisha
zoezi la usuluhishi kwa sababu muwakilishi huja na msimamo na hivyo juhudi zote
za msuluhishi kuonesha faida ni hafifu na badala yake kutozaa matunda,
mwakilishi utakuta bado husimama na alichotoka nacho nje ya chumba cha
usuluhishi. Kwa hivyo hupelekea mteja kuamini kuwa ana nafasi ya kushinda kesi huko
mbeleni badala ya kutumia vizuri nafasi ya usuluhishi.
Zoezi
hilo la kuzitembelea taasisi za kifedha kwa mkoa wa Dar es salaam ni endelevu
ili kujaribu kutafuta ushawishi wa kutatua migogoro baina ya wateja na mabenki
ili kukuza uchumi na kupunguza migogoro inayochukua muda mrefu kwa njia ya
kawaida mahakamani.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi Mhe. Zahra Maruma (aliyevalia ushungi) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa nje wa Taasisi ya kifedha kutoka benki ya CRDB. Wengine Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi Mhe. Angela Bahati (mwenye koti la bluu)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni