Jumamosi, 25 Novemba 2023

WASTAAFU WATATU MAHAKAMA YA MKOA DAR ES SALAAM-KISUTU WAFANYIWA HAFLA YA KUAGWA

  • Waitumikia Mahakama ya Tanzania kwa miaka 40
  • Waaswa kujishughulisha na kazi za kuwapatia kipato

Na Eunice Lugiana, Mahakama-Dar es Salaam

Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam iliyopo Kisutu imefanya hafla fupi ya kuwaaga wastaafu watatu waliyoitumikia Mahakama ya Tanzania kwa muda wa miaka 40. 

Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyoandaliwa na watumishi wa Mahakama hiyo na kufanyika tarehe 24 Novemba, 2023 katika viwanja vya Mahakama hiyo, Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama hiyo, Mhe. Aron Lyamuya aliwapongeza wastaafu hao kwa kumaliza salama utumishi wa umma na kuwaasa kuendelea kujishughulisha na kazi za kuwapatia kipato. 

Wastaafu hao walioagwa ni Bi.Bernadetha Rutaihwa aliyehudumu katika nafasi ya Katibu Mahsusi Ofisi ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Bi. Rosemary Mganga aliyeajiriwa kama Mchapaji na baadae kujiendeleza na kupanda cheo hadi Msaidizi wa Mtendaji na Bw. Francis Ochieng Abaja aliyeajiriwa kwa cheo cha Mlinzi.

“Mmestaafu lakini bado mna nguvu kama mtafuga kuku au kulima maghimbi leteni tutawaungisha tuwe sehemu ya maisha yenu bado tungependa kujumuika na ninyi kwa sababu na sisi muda si mrefu tunakuja huko huko mlikokuwa,” alisema Mhe. Lyamuya.

Mhe. Lyamuya aliwaeleza wastaafu hao kwamba, licha ya kuwaaga watumishi hao, Mahakama ya Kisutu bado ni nyumbani kwao, hivyo wasisite kupita ili wasalimiane na kubadilishana mawazo. 

Aliwaomba wajishughulishe na kazi zingine za mikono badala ya kukaa maana ukikaa tu mwili unachoka alitoa mfano wa chuma, kwamba chuma ni kigumu lakini kisipotumika ukikiweka tu chini kinapata kutu na hatimaye kulika na kuisha  lakini kikiwa kinatumika hakiwezi kupata kutu wala kulika.

Aliwataka wastaafu hao wajishughulishe na kujituma pamoja na kuanzisha mambo yatakayowafanya kila siku wawe na sababu ya kutoka nyumbani, hiyo itawafanya kugundua kuwa maisha mengine yapo zaidi ya Utumishi wa Umma.

Awali, akiwakaribisha wageni waalikwa pamoja na waagwa Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam-Kisutu, Bi. Athanasia Kabuyanja aliwashukuru watumishi kwa kujitoa kuwaaga wenzao  pia na kuwashukuru waagwa kwa kuitikia wito wa kufika katika hafla hiyo.

Waagwa hao walitoa shukurani zao kwa viongozi pamoja na watumishi wote kwa kuwakumbuka na kuwaandalia hafla hiyo pamoja na zawadi nzuri ambapo wamekiri kuwa hawakutegemea.

Wastaafu hao wameonesha kufurahishwa na tukio hilo na kuomba radhi kama kuna mahali walitenda kinyume na kusababisha tatizo. Pia wamewatakia kila la heri katika utumishi watumishi wote walioko kazini.

Hafla hiyo iliyoambatana na chakula cha jioni na mziki laini ilihudhuriwa na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Moses Mashaka pamoja na wawakilishi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka  na Polisi.

Wastaafu wakiwa katika picha ya pamoja. Katikati ni Francis Abaja, kulia ni Bernadetha Sahani na kushoto ni Rosemary Mganga.

Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam-Kisutu, Mhe. Aron Lyamuya akitoa nasaha kwa Wastaafu hao (hawapo katika picha) wakati wa hafla ya kuwaaga waliyofanyiwa na Watumishi wa Mahakama hiyo.

Mtendaji Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam Kisutu, Bi. Athanasia Kabuyanja akiwakaribisha wastaafu hao pamoja na wageni waalikwa kushiriki katika hafla hiyo.

Watumishi wa Mahakama hiyo wakicheza muziki wakati wa hafla hiyo.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Moses Mashaka akilishwa keki kama ishara ya Upendo kutoka kwa wastaafu hao.

Keki maalum za pongezi zilizoandaliwa na Watumishi wa Mahakama hiyo kama ishara ya Upendo kwa Wastaafu hao.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma).




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni