Jumatatu, 11 Desemba 2023

BONANZA LA MICHEZO: MTWARA, LINDI NA RUVUMA WAKABANA KOO

Na Richard Matasha-Mahakama, Mtwara

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe, Rose Ebrahim, akishirikiana na Kamati ya Maandalizi, hivi karibuni aliongoza Bonanza la Michezo katika Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma lililofanyika katika  viwanja vya Ilulu, huku Mahakama Kuu Kanda ya Songea ikishiriki kama waalikwa. 

Ushiriki wa Mahakama Kuu Songea uliongeza chachu katika Bonanza hilo ambalo limeweka historia ya aina yake hususani kwani Mikoa ya Kusini mwa Tanzania kwa Mahakama na wadau kujumuika pamoja katika michezo mbalimbali.

Katika Bonanza hilo, Mhe Ebrahim, ambaye alikuwa mgeni rasmi aliambata na, Majaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mtwara, Mhe. Said Ding’hoi na Mhe. Martha Mpaze, Naibu Wasajili Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara na Songea, Watendaji wa Mahakama Kuu Mtwara, Songea na Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi na viongozi wengine.

“Michezo huimarisha afya, hudumisha ushirikiano, upendo na umoja katika jamii, hasa utumishi wetu, natumaini ushirikiano huu kati ya watumishi wa Mikoa hii utaendelezwa hata kwenye masuala mengine,” Jaji Mfawidhi alisema wakati akifungua Bonanza hilo.

Bonanza hilo lilisheheni michezo kemkem, ikiwemo karata, bao, kuvuta kamba, kukimbiza kuku, riadha, kukimbia na gunia, kukimbia na yai, mpira wa pete, mpira wa miguu na mingineyo mingi, ambapo watumishi wakishirikiana na wadau wa Mahakama katika Mikoa yao walimenyana vikali katika michezo hiyo.

Katika mchezo wa mpira wa miguu wanaume, timu kutoka Lindi iliibuka kidedea kwa ushindi wa mikwaju ya penati 4-2 dhidi ya Mtwara baada ya kutoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1 ndani ya dakika 90. Mkoa wa Mtwara ulitia fora baada ya kutwaa ushindi wa kuvuta kamba kwa upande wa wanaume na wanawake kwa kuwachakaza bila huruma timu za Songea na jirani zao Lindi.

Michezo mingine iliyokuwa na msisimko mkubwa ni ule wa mpira wa pete ambapo timu ya wanawake kutoka Songea walizisambaratisha timu kutoka Mtwara na Songea kuibuka mshindi wa mchezo huo. 

Jaji Mfawidhi wa Makahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara na Mgeni rasmi, Mhe. Rose Ebrahim akitoa neno la ufinguzi wa Bonanza hilo.

Jaji Mfawidhi wa Makahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu Mtwara, Mhe. Said Ding’hoi (kulia), Mhe. Martha Mpaze (kushoto) pamoja na viongozi wengine.

Jaji Mfawidhi wa Makahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim (katikati) na Majaji wa Mahakama Kuu Mtwara, Mhe. Said Ding’hoi (kulia) na Mhe. Martha Mpaze (kushoto), watumishi na wadau wakishiriki katika jogging.

Jaji Mfawidhi wa Makahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim (katikati) na Majaji wa Mahakama Kuu Mtwara, Mhe. Said Ding’hoi (kulia) na Mhe. Martha Mpaze (kushoto), watumishi na wadau wakishiriki katika mazoezi ya viungo.

Raha iliyoje kwa watumishi wa Mahakama Mkoa wa Mtwara wakishangilia ushindi katika mchezo wa kuvuta Kamba.



Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni