Jumatatu, 11 Desemba 2023

KILA MMOJA AWAJIBIKE KUJENGA KIZAZI CHENYE MAADILI NA UTU; WAZIRI MKUU

Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ametoa rai kwa wananchi wote nchini kutekeleza jukumu la kuhakikisha kuwa, kila mmoja anajenga kizazi chenye maadili sambamba na kuzingatia haki za binadamu. 

Mhe. Majaliwa alitoa wito huo jana tarehe 10 Desemba, 2023 kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sherehe za kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa zilizofanyika katika Viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

“Ni jukumu la kila mmoja wetu ikiwemo Viongozi wa Dini kuhakikisha kuwa kwa pamoja tunajenga kizazi chenye maadili kwakuwa jitihada za Serikali pekee hazitazaa matunda kama hakuna ushirikiano wa wananchi,” alisema Mhe. Majaliwa.

Aliongeza kuwa, katika kutekeleza jukumu hilo ni muhimu pia kutosahau mapambano dhidi ya rushwa kwakuwa bado ni janga kubwa ambalo ni adui wa vitu vingi ikiwemo haki, maendeleo ya Taifa na kadhalika na hivyo pia kuwataka wananchi ambao nao ni wadau muhimu kushirikiana kwa pamoja na Serikali kutokomeza rushwa.

“Ewe Mtanzania usikubali kutoa rushwa popote, unatakiwa kupata huduma bila kutoa rushwa kwakuwa rushwa ni adui wa haki, maendeleo na mla rushwa hafai kuwa katika jamii,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Miongoni mwa masuala kadhaa aliyoyasisitiza Mhe. Majaliwa ni pamoja na kuwa na Mkakati wa utoaji Elimu kwa Umma kuhusu Mkakati wa Awamu ya Nne wa kupambana na Rushwa, Taasisi na Ofisi mbalimbali kuwa na uwazi katika utoaji huduma.

Mengine ni Dini zote kuendelea kukalipia vitendo vya rushwa, kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia na Watoto na mengine.

Katika hafla hiyo, Waziri Mkuu alizindua kitabu cha awamu ya nne ya Mkakati wa Mapambano dhidi ya rushwa.

Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu kilienda sambamba na maadhimisho ya miaka 75 ya Tamko la Dunia kuhusu Haki za Binadamu  ambapo Tanzania ni Mshiriki mmojawapo.

Kilele cha Siku hiyo kilitanguliwa na Maonesho ya Wiki moja yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Nyerere 'Square' kuanzia tarehe 05 hadi 10 Desemba, 2023 ambapo Mahakama ya Tanzania ilishiriki pamoja na Wadau wengine ikiwemo Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na wengine ambapo walishiriki kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo maadili ya haki za binadamu.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akihutubia baadhi ya watumishi wa umma pamoja na wananchi (hawapo katika picha) katika hafla za Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa jana tarehe 10 Desemba, 2023 katika Viwanja vya Nyerere 'Square' jijini Dodoma.

Sehemu ya wananchi wakimsikiliza Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (hayupo katika picha) wakati akitoa risala yake katika hafla ya kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa jana tarehe 10 Desemba, 2023 katika Viwanja vya Nyerere 'Square' jijini Dodoma.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akizungumza jambo na Watumishi wa Mahakama ya Tanzania waliokuwa wakitoa elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali ya Mahakama ikiwepo jinsi Mahakama inavyozingatia Maadili na Haki za Binadamu.

Meza Kuu ikiongozwa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa wakiwa katika hafla za kilele cha 
Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa katika Viwanja vya Nyerere 'Square' jijini Dodoma.

Wananchi wakipata elimu ya kuhusu Mahakama kutoka kwa watumishi wa Mhimili huo. Mahakama ya Tanzania ni moja kati ya Washiriki wa Maonesho ya Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa  yaliyofanyika katika Viwanja vya Nyerere 'Square' kuanzia tarehe 05 Desemba, 2023 na kuhitimishwa jana tarehe 10 Desemba, 2023.

(Picha na Jeremia Lubango, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni