Jumanne, 12 Desemba 2023

JAJI KIONGOZI ATAJA SIFA ZA KIONGOZI WA MAHAKAMA

Na. Innocent Kansha - Mahakama

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Mohamed Siyani amezitaja sifa mahususi za Kiongozi wa Mahakama anazopaswa kuwa nazo zikiwemo sifa za kimuundo na za ziada, vileviele awe na wajibu wa kuwa daraja kati ya Mahakama na wadau wengine kama vile Serikali, Bunge na umma kwa ujumla.

Akifungua Mafunzo Elekezi kwa Naibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi leo tarehe 12 Desemba, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Siyani amesema Kiongozi wa Mahakama anapaswa kujipima yeye mwenyewe kabla hajapimwa na umma au viongozi wa juu yake. Ni lazima ajue kwa asili ya kazi yake atapimwa tu na kipimo chake kikubwa ni kwa umma anaouhudumia.

“Umuhimu wenu kwa Mahakama unatokana na majukumu makubwa ambayo sheria na miongozo mbalimbali imeweka kwenu. Naibu Msajili au Hakimu Mkazi Mfawidhi ana wajibu mkubwa wa kuongoza watumishi wengine wa Mahakama katika eneo lake”, amesema Mhe. Siyani.

Mhe. Siyani amesema, Kiongozi wa Mahakama anapaswa kujua wajibu wake, atambue yeye kama Naibu Msajili au Hakimu Mfawidhi ana majukumu gani. Awe na check list inayomwezesha kujipima na kujua kila siku amefanya nini. Checklist hiyo inaanzia kwenye mpango mkakati wetu.

Kiongozi wa Mahakama, anapaswa kuwa na mfano wa maadili ndani na nje ya mahakama. Kila wakati anapaswa kujitazama na kujiuliza ikiwa anachotenda kinaipa sifa nzuri mahakama au kinaichafua.

Kiongozi wa mahakama anapaswa kuwa mwenye busara, heshima, adabu, mvumilivu na mwenye lugha nzuri. Kiongozi wa mahakama hapaswi kuwa  mwenye kiburi, hasira zivukazo mpaka. Hapaswi kujivuna na kujiona yeye ni bora kuliko wengine.

“Kumbukeni miongoni mwa mambo yaliyowafikisha hapa ni maoni ya wananchi mliowahudumia. Kama mtabadilika, mkalewa sifa za ubosi, wananchi wale wale waliotoa maoni mazuri juu yenu, ndio watakaowaangusha”, amesisitiza Jaji Kiongozi.

Vilevile Mhe. Siyani akataja kwamba, Kiongozi wa Mahakama siyo tu hapaswi kula rushwa, bali hapaswi hata kuhisiwa amekula rushwa. Kiongozi wa Mahakama ni mfano wa tabia njema unaopaswa kuigwa na watumishi wenzake na kuzungumwa vizuri na umma.

Kiongozi wa Mahakama siyo kikwazo kwa walio chini yake kukua. Kiongozi wa Mahakama anapaswa kuwa mlezi anayeibua na kukuza vipaji vya walio chini yake.

Aidha, Mhe. Siyani ameongeza kuwa, Kiongozi wa Mahakama ni yule ambaye ukimpima utaona yuko juu ya viwango vya kawaida. Kiongozi wa Mahakama siyo mtu wa kulalamika, ni mtu anayetafuta majibu kwa changamoto zinazoikabili ofisi yake (problem solver).

Kiongozi wa Mahakama ni mtu anayewaunganisha watumishi wote wa mahakama. Kwa maana hiyo Kiongozi wa Mahakama si mbaguzi kwa namna yoyote. Siyo yule anayesema huyo ni Afisa Mahakama (Judicial Officer) ni mheshimu na yule siyo Afisa wa Mahakama (Non Judicial Officer) nisimuheshimu.

“Kiongozi wa Mahakama anapaswa kuheshimu watu wote na anapaswa kuwa na hofu ya Mungu kwa imani yake. Hata kama haamini uwepo wa Mungu, awe na mfano wa huruma ya Mungu. Hatuwezi kuwa na kiongozi katili ambaye hawajali watu”, amesisitiza Mhe. Siyani

Jaji Siyani amesema ni wajibu wa kila mtumishi kutambua kuwa yeye ni kiongozi na kwamba katika kufanya kazi na wenzake azingatie umuhimu wa urafiki, kuheshimiana na kushirikiana (friendliness, courtesy, mutual respect and pride in the group). Kila mmoja wenu afanye kazi kwa kutambua na kuthamini uwezo na mchango wa mwenzake, hiyo ndiyo dhana ya ushirikiano (collegiality)

Jaji Kiongozi amewakumbushe kuwa, kuwa Naibu Msajili au Hakimu Mkazi Mfawidhi haimaanishi mmepewa kibali cha kuacha kusikiliza mashauri. Kwa mfano kuna waraka zinazowataka Naibu Wasajili kusikiliza mashauri huku mkiendelea na majukumu yenu ya kiutawala. Waraka husika umeainisha hadi idadi ya chini ya mashauri mnayopaswa kumaliza kwa mwaka. Kazi yenu ya uhakimu haifi kwa kuwa wasajili. Misingi ile ile ya uhakimu inapaswa kuwaongoza mnapotekeleza majukumu yenu nayo ni kuhakikisha mnaishi viapo vyenu.

Mhe. Siyani akarejea maneno ya Jaji wa Mahakama ya Rufani Dkt. Gerald Ndika ambaye kwa nyakati tofauti amekuwa akisisitiza yafuatayo; Mosi, Kazi mnayoifanya iwe Uhakimu, Usajili au Ujaji sio ajira wala wito. Ni dhamana tuliyopewa na Watanzania chini ya Katiba yetu. Kwa sababu hiyo tunawajibika kutenda kazi yetu ya utoaji haki kwa kufuata Kanuni za Maadili na mnawajibu wa kuviishi viapo vyenu vya kutoa haki bila huba, upendeleo, hofu au chuki.

Jambo lingine Jaji Kiongozi akasema, kazi ya utoaji haki inafanywa hadharani na matokeo yake ambayo ni maamuzi tunayoyatoa yanawekwa hadharani. Hakimu au Jaji hawezi kujitetea baada ya kutoa maamuzi yake hasa pale hukumu hiyo inapokuwa na kasoro. Hivyo, yapaswa kuzingatia kuwa hukumu mtatakazozitoa ziwe na ubora na zenye kukidhi viwango ili ziweze kujieleza kwa ufasaha na zenye uwezo wa kujitetea zenyewe.

“Vilevile, kazi ya utoaji haki ni ngumu sana na pia ina lawama hasa kutoka kwa wadaawa walioshindwa. Hivyo tunatakiwa kuwa wavumilivu sana, tena sana. Tusikate tamaa tunapotupiwa lawama hasa kwenye mitandao ya kijamii. Lakini pia tukubali kukosolewa pale inapostahili”, ameongeza Jaji Kiongozi.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Mohamed Siyani akitoa hotuba ya ufunguaji wa mafunzo elekezi kwa Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mikoa leo tarehe 12 Desemba, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke.

Sehemu ya Viongozi Waandamizi wa Mahakama ya Tanzania waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa mafunzo elekezi kwa Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mikoa leo tarehe 12 Desemba, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke.

Sehemu ya Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mikoa wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa mafunzo elekezi kutoka kwa mgeni rasmi Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (hayupo pichani) 

Sehemu ya Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mikoa wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa mafunzo elekezi kutoka kwa mgeni rasmi Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (hayupo pichani) 


Sehemu ya Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mikoa wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa mafunzo elekezi kutoka kwa mgeni rasmi Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (hayupo pichani) 


Sehemu ya Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mikoa wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa mafunzo elekezi kutoka kwa mgeni rasmi Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (hayupo pichani) 

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (katikati) akiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa mafunzo elekezi kwa Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mikoa, wengine kwenye meza kuu ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Angelo Rumisha (kushoto) na kulia ni Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke Mhe. Asina Omari.


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (katikati mstari wa mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mikoa mara baada ya uzinduzi wa mafunzo elekezi yaliyoanza leo tarehe 12 Desemba, 2023.

Picha na Innocent Kansha - Mahakama  

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni