- Imebainishwa wakati wa hafla ya kuuaga mwaka 2023 na kuukaribisha 2024
Na Abdallah Salum, Mahakama-Njombe
Jumla ya mashauri 21 kati ya mashauri 22 ya mauaji sawa na asilimia 85 yamesikilizwa mkoani Njombe na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha pamoja na Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Saidi Kalunde huku Majaji hao wakiwashukuru Watumishi wa Mahakama hiyo pamoja na Wadau kwa ushirikiano uliowawezesha kufanya kazi hiyo.
Hayo yalibainishwa tarehe 11 Desemba, 2023 wakati wa hafla fupi ya kuuaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka 2024 iliyofanyika katika Mahakama hiyo.
"Napenda kuwashukuru watumishi wa Mahakama hii kwa kuwezesha urahisishaji wa usikilizaji wa mashauri kwa takribani mwezi mmoja wakiwemo Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea, Jeshi la Polisi pamoja na Waandishi Waendesha Ofisi na Wasaidizi wa Ofisi," alisema Mhe. Karayemaha.
Mhe. Karayemaha aliwapongeza pia watumishi wa Mahakama Mkoa wa Njombe kwa upendo na ukarimu huku akionesha kufurahishwa kwa namna walivyompokea na kufanya kazi kwa pamoja na kwa kujitoa kwao, huku pongezi nyingi akimpa Mtendaji wa Mahakama wa Mahakama hiyo, Bw. Yusuph Msawanga jinsi anavyoishi na watumishi wake.
Pamoja na hayo, Mhe. Karayemaha aliwasisitiza pia, watumishi kuwa na tabia ya kujisomea ili kuwa na ufahamu wa vitu vingi ambavyo vitaleta tija katika kazi za kila siku.
Akizungumzia kuhusu hafla hiyo, Jaji Mfawidhi huyo aliishukuru Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe kwa kuwaalika katika hafla hiyo huku akitoa shukrani zake kwa Mahakama hiyo kwa ushirikiano waliopata kwa kipindi cha mwezi mmoja walipokuwa wakisikiliza mashauri hayo.
Aliipongeza Mahakama hiyo kwa kufanya hafla hiyo kwakuwa, muda huo unatumika pia kukaa kama familia pamoja na kuzungumza na kuwekana sawa kuhusu kazi na mambo mengine pamoja na kufurahi kwa pamoja.
Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Kalunde aliwakuwakumbusha watumishi wa Mahakama hiyo kuwa mbali na kufanya kazi ni muhimu pia kuwa na utamaduni wa kukutana na kukaa pamoja ili kufahamiana zaidi na kuwa na ukaribu.
“Wakati wa maisha yetu tusijisahau sana tuwe na utamaduni wa kukutana na kukaa kwa pamoja kama familia kwa kufurahi pamoja na kuzidi kufahamiana zaidi kwa ukaribu zaidi, kwa kuwa tumefanya kazi kuanzia Januari, 2023 hadi Desemba 2023, asubuhi mpaka jioni kwa kutoa huduma kwa wananchi muhimu kukutana kama hivi na siyo kukaa mwaka mzima bila ya kukaa pamoja kama familia kitu hicho si kizuri,” alisema Mhe. Kalunde
Hafla hiyo fupi ya kuuaga mwaka 2023 iliwashirikisha pia Mahakama Kuu ya Songea, Mahakama Kuu Iringa, Wanasheria wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea, pamoja na watumishi wa Mahakama Mkoa Njombe huku Mhe. Kalunde akisisitiza kufanya kazi kama timu moja na kwa ushirikiano.
Pia hafla hiyo fupi iliambatana na kukata keki na kulishana kwa upendo kwa ajili ya kufurahi kwa pamoja kwa kuwakutanisha watumishi wa Mahakama pamoja na wadau wa Mahakama ya Mkoa njombe.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha (kushoto) pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Saidi Kalunde wakifurahia jambo wakati wa hafla fupi ya kuuaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka 2024 iliyoandaliwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe. Majaji hao wapo mkoani humo kwenye kikao maalum cha kusikiliza mashauri ya mauaji ambapo hadi kufikia tarehe 11 Desemba, 2023.
Baadhi ya watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe wakiwa na baadhi ya Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea pamoja na Askari Polisi kama wadau wa Mahakama walioalikwa katika hafla fupi ya kuuaga mwaka 2023 na kuukaribisha 2024 iliyoandaliwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe.
Keki zilizotengenezwa maalum kwa ajili ya kuuaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka 2024.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe Mhe. Liadi Chamshama akifungua hafla fupi ya kuuaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka 2024. Kushoto ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha kushoto kwake ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Saidi Kalunde na kulia ni Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa Njombe, Bw. Yusuph Msawanga.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Iringa, Mhe. Saidi Kalunde akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe pamoja na Wadau (hawapo katika picha) wakati wa hafla fupi ya kuuaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka 2024.
Picha ya pamoja Mahakama na Wadau, Katikati ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha, wa tatu kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Saidi Kalunde, wa pili kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa Njombe, Mhe. Liadi Chamshama, wa kwanza kulia ni Mtendaji Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw. Yusuph Msawanga wa tatu kushoto ni Wakili wa Kujitegemea, Bi. Neema Msafiri, wa pili kushoto ni Wakili wa Kujitegemea, Bw. Isakwisa Mwambulukutu na wa kwanza kushoto ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Achiles Mulisa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha akizungumza jambo na akiwa na Mwendesha Mashtaka Mkoa wa Njombe wakiteta.
Katibu wa Sheria Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Jackson Banobi akimlisha keki Katibu wa Sheria Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Mhe. Lilian Haule, kushoto ni Mtendaji Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw. Yusuph Msawanga.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni