Jumatano, 13 Desemba 2023

ZINGATIENI USHIRIKIANO, MASHAURIANO NA UWAZI KATIKA UTENDAJI KAZI; JAJI KAHYOZA

Na. Innocent Kansha - Mahakama

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza amewataka Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi kuzingatia ushirikiano, mashauriano, uwazi na kuratibu majukumu vilevile kupenda kujifunza majukumu ya Ofisi zingine zinazokuzunguka.

Akizungumza wakati wa mafunzo elekezi kwa Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi leo tarehe 13 Desemba, 2023 wakati akitoa mada ya majukumu ya Maafisa Mahakama na Watendaji wa Mahakama Mhe. Kahyoza amesema ni muhimu kujifunza kila siku kutoka kwa watumishi wengine, kupanga taratibu za uendeshaji wa shughuli zanu za kila siku za ofisi na kupenda kutoa taarifa za matukio yote muhimu yaliyoko kwenye ratiba za ofisi za Mkuu wenu wa vituo.

“Shirikiana na ofisi ya Mtendaji kila siku katika kupanga bajeti ya shughuli za kimahakama za kanda yako bila kuathiri mamlaka ya Afisa mwingine kwani Ofisi ya Naibu Msajili na Mtendaji ni ofisi moja na kiungo muhimu katika kuratibu shughuli zote za kimahakama”, ameongeza Mhe. Kahyoza  

Mhe. Kahyoza amewambia Manaibu Wasajili kuwa, watafute njia rahisi za kuwafundisha watumishi wanaoshirikiana nao mara kwa mara juu dira, miongozo, sera na taratibu mbalimbali na mabadiliko ya mara kwa mara yanayotokea kwenye taasisi.

Msajili na Mtendaji wanapaswa kufanya kazi zao za kila siku za kuratibu utendaji kazi kwa kuwashirikisha viongozi wa vituo ili kurahisisha utoaji wa maamuzi. Msitanganishe ofisi ya viongozi wenu na zile mnazozihudumu ili kuratibu mashauriano, amesema Jaji Kahyoza.

Mhe. Kahyoza amewataka wasajili kusimamia kwa ukamilifu masijala, nyaraka na vifaa vyote vya kiutendaji kama vile mihuli na mafaili, ikubukwe kuwa msajili ni mlezi mkuu wa masijala na watumishi wa masijala hizo.

Msajili unapaswa kutoa taarifa ya utendaji kazi wa mara kwa mara kwa Jaji Mfawidhi na kupanga namna bora ya uendeshaji wa mashauri kila siku. Msajili unatakiwa kuepuka kutoa amri zisizotekelezeka unapotekeleza majukumu yako ya kila siku mfano; unatakiwa kutekeleza amri hii bila kukosa kufikia kesho asubuhi la sivyo nitakufukuza kazi, ile hali unajua huna mamlaka hayo, huo ni uhalifu kama uhalifu mwingine, amesema Jaji Kahyoza.

“Zingatieni mlolongo wa amri (chain of command) na mamlaka za kimahakama bila kuathiri shughuli za watendaji wengine ndani ya eneo lako la kazi hii itawasaidia kuondoa migongano na malalmiko yasiyo ya lazima kwa watumishi na wadau wa Mahakama”, amesisitiza Jaji Kahyoza.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza akitoa mada kwa Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wakati wa mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Kuu Dodoma na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama Mhe. Angelo Rumisha (kulia) na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania anayesimamia Divisheni Bi. Mary Shirima wakifuatilia mada.

Sehemu ya Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wakifuatilia mada 

Sehemu ya Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wakifuatilia mada 

Sehemu ya Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wakifuatilia mada 

Sehemu ya Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wakifuatilia mada 

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania anayesimamia Divisheni Bi. Mary Shirima akifafanua jambo wakati wa utoaji mada ya majukumu ya Maafisa Mahakama na Watendaji wa Mahakama.

Picha na Innocent Kansha - Mahakama

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni