Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa Tanzania mstaafu, Mhe. Barnabas Albert Samatta amesema haki ndiyo moyo wa utawala na kamwe haiwezi kutenganishwa na amani ya Nchi.
Mhe. Samatta aliyazungumza hayo katika hafla ya kuzindua kitabu chake kipya kinachoitwa, “Utawala Bora Vita Dhidi ya Udhalimu Rushwa na Elimu Duni” iliyofanyika kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
“Kila mwananchi anawajibu wa kutoa mchango wake wa kuiwezesha Nchi yake kuwa na utawala bora au kuuimarisha na kulinda kama tayari upo,” Jaji Mkuu Mstaafu alisema.
Alibainisha pia kuwa kwenye nyanja ya utoaji haki mahakamani kila mwananchi anawajibika pia kulaani vitendo vinavyoendana na maneno ambayo yanasemekana husikika sana kwenye nchi moja katika Bara la Asia yanayosema, “Kwa nini umwajiri mwanasheria kama unaweza kumnunua Jaji?”
Mhe. Samatta alisema hapa duniani hakuna maneno yaliyotamkwa au kuandikwa na binadamu kuhusu umuhimu wa kuwepo haki ambayo yana hekima yenye uzito kupita maneno ya Mfalme Mkuu Ferdinand wa Kwanza wa Himaya Takatifu ya Roma.
Alimnukuu mfalme huyo katika maneno yake alipokuwa anawaeleza wageni mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo, akiwemo Jaji Mkuu wa Tanzania, ambaye alikuwa mgeni rasmi, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma. Alisema, “Haki iwepo hata kama Dunia inaangamia.”
Jaji Mkuu mstaafu alisema kama wasomi wengi wajuavyo, utawala bora ndani yake ukiwemo utawala wa sheria ni moja ya mifumo inayohusu uendeshaji wa Nchi inayotoa michango mikubwa katika uzalishaji na ulinzi wa furaha kwa binadamu katika Nchi na kuzalisha huzuni kwa Viongozi wenye mielekeo ya udikteta.
“Ni tumaini langu kuwa kule ambako kitabu changu kitasomwa kitatoa michango pale ambapo pana upungufu wa kuzalisha au kuongeza matunda yanayozalisha furaha katika Nchi husika,” alisema.
Mhe. Samatta alieleza kuwa ili kushirikisha vya kutosha ujuzi wake wa mfumo wa utawala na demokrasia, dhana ya utawala wa sheria na Katiba bora ya Nchi aliingiza kwenye kitabu chake nukuu nyingi za Majaji, Wanafalsafa, Wataalam, Viongozi mashuhuri na wengine wengi.
Hata hivyo, hakukubaliana na nukuu kadhaa, ikiwemo ya Rais wa Uganda Iddi Amin Dada inayosomeka, “Kifo ndiyo jawabu la matatizo yote. Hakuna mtu-hakuna tatizo.”
Nukuu nyingine ambayo hakukubaliana nayo ni ya Bw. Joseph Stalin aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Nchi ya Kikomunisti ya Urusi ambayo inasema, “Mawazo yana nguvu zaidi kuliko bunduki. Hatuwezi kuwaruhusu adui zetu kuwa na bunduki. Kwa nini tunawaruhusu kuwa na mawazo?”
Hivyo, Mhe. Samatta alisema atafarijika kama baadhi ya yale ambayo ameyaandika kwenye kitabu chake yataeleweka kwa usahihi na kutoa michango kwenye juhudi za uboreshaji wa utoaji haki nchini Tanzania na kwingineko kwenye maeneo mbalimbali.
Alibainisha maeneo hayo, ikiwemo haki ya wananchi kushirikishwa kwenye maamuzi makuu kwenye uongozi wa Nchi yao; haki kwenye utawala ndani ya sekta binafsi; haki ya wananchi kuheshimiwa kwenye uongozi wa Nchi yao na haki ya wananchi kulindwa dhidi ya uonevu na uovu wa rushwa.
Maeneo mengine ni haki kwenye Ofisi za Tume za Uchaguzi na vituo vya kura; haki kwenye Mabunge na Taasisi za kutunga sheria; haki kwenye Ofisi za Serikali Kuu na Taasisi zake; haki ndani ya Serikali za Mitaa; haki ndani ya Mahakama na haki ndani ya Mabaraza ya Hukumu.
Uzinduzi wa kitabu hicho ulihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali na Mahakama, akiwemo Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu, Mhe. Joseph Sinde Warioba.
Walikuwepo pia Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama ya Rufani wastaafu, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wastaafu, Viongozi wa Dini, Vyama vya Kisiasa na Kijamii na wengine wengi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni