Jumatatu, 4 Desemba 2023

JAJI MKUU AZINDUA KITABU KIPYA CHA JAJI BARNABAS SAMATTA

·      Kinasisitiza utawala bora, haki

·      Awahimiza Watanzania kuishi kwa vitendo dhana za utawala bora, uadilifu

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amezindua Kitabu kipya kilichotungwa na Jaji Mkuu wa Tanzania mstaafu, Mhe. Barnabas Albert Samatta na kuhimiza Watanzania kuziishi dhana za uadilifu, utawala bora na utawala wa sheria wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.

Uzinduzi wa Kitabu hicho kinachoitwa, “Utawala Bora Vita Dhidi ya Udhalimu Rushwa na Elimu Duni” uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam ulihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali na Mahakama, akiwemo Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu, Mhe. Joseph Sinde Warioba.

Wengine ni Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama ya Rufani wastaafu, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wastaafu, Viongozi wa Dini, Vyama vya Kisiasa na Kijamii na wengine wengi.

Akizungumza kabla ya kuzindua Kitabu hicho, Mhe. Prof. Juma aliwahimiza Watanzania kununua na kukisoma ili wajiongezee maarifa yanayohusu dhana za uadilifu, utawala bora na utawala wa sheria ambazo kwa kikasi kikubwa huwa hazitekelezwi kwa vitendo.

“Naomba sana tusome, siyo mara moja hiki Kitabu ili tuweze kuelewa na kuziishi (hizi dhana za haki na utawala bora.) Ni rahisi kuzungumzia dhana, lakini kuna ugumu wa kuzitekeleza…

“…. dhana ya utawala bora, utawala wa sheria huwa tunaziongea kila wakati, lakini katika utekelezaji wake hata sisi wenyewe tunaotetea hizo dhana wakati mwingine tunajikuta hatuzitekelezi,” alisema.

Jaji Mkuu pia alihimiza vyuo mbalimbali nchini kutoa wahitimu wa aina ya Mhe. Samatta ambao ni waadilifu na wanaopenda haki kwa kila mtu. Alisema Jaji Samatta katika kipindi chote alikuwa anasisitiza uadilifu kwa Majaji na Mahakimu. 

“Kwa hiyo, anapozungumzia haki, siyo anazungumza kutoka hewani, inatokana na mapitio na tanuri alilopitia. Haya anayoyaongelea katika Kitabu chake yanatoka ndani ya makuzi na fikra zake. Naomba elimu zetu ziweze kutoa watu wenye uwezo na maadili kama ya Mhe. Samatta…

“Uelewa wake kuhusu uadilifu, utawala bora na utawala wa sheria siyo kitu ambacho unakiona juu juu, pengine ukimchanja kidogo hizi dhana zitajitokeza. Hivyo, tujaribu kuwa watu wa aina yake,” Mhe. Prof. Juma alisema

Amesema kuwa kipindi Mhe. Samatta ni Jaji Mkuu kati ya 2000 na 2007 alijiunga na kikundi huru cha hiari cha Majaji Wakuu na Majaji wengine waandamizi waliokuwa wanahimiza uadilifu wa Majaji katika utoaji haki.

“Kikundi hiki kilikuwa kinasema independence and competence of the judiciary depends on integrity. Mhe. Samatta alikuwa anapenda kusema ni afadhali uwe na uelewa mdogo wa sheria lakini uadilifu mkubwa unaweza kufanya kazi ya utoaji haki," alisema.

Aliwakumbusha wananchi wanaposoma Kitabu hicho kutokusahau hatua mbalimbali alizopitia ambazo ndizo zimemjenga kuwa Barnabas Albert Samatta ambaye wanamfahamu leo.

Jaji Mkuu alieleza kuwa utafiti wake mdogo aliofanya unaonesha Mhe. Samatta alikuwa kundi la tatu lililojiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 1963 na 1966 kusoma Shahada ya Sheria na kwenye kundi hilo walikuwa wanafunzi 32, akiwemo mzee Warioba, Jaji Damian Rubuva, Edward Mwesumo, Josephat Kanywani na Horace Kolimba.

Anaamini kuwa katika mafunzo hayo wanafunzi hao, akiwemo Mhe. Samatta walijengewa fikra ambazo nyingine ndiyo zinaibuka kwa sasa kwa sasabu yale anayoeleza leo hayakuibuka hewani, yanatokana na historia aliyopitia na makuzi yake ya imani.

“(…) pengine Mwalimu wake Mhe. Samatta anaweza kutupa picha ni tanuri la aina gani lilitumika kwa Wanafunzi hao wa wakati huo kuwajenga ili wawe na mawazo ambayo leo ameweza kuyatoa kupitia kitabu hiki,” alisema.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Kitabu kipya kilichotungwa na Jaji Mkuu wa Tanzania mstaafu, Mhe. Barnabas Albert Samatta (kushoto). Picha chini Mhe. Prof. Juma akiwaonyesha kitabu hicho wageni mbalimbali waliojitokeza kwenye uzinduzi huo.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) na mtunzi, Jaji Mkuu wa Tanzania mstaafu, Mhe. Barnabas Albert Samatta wakionyesha kitabu hicho.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) akiongea na wageni mbalimbali kwenye hafla ya uzinduzi wa  Kitabu kipya kilichotungwa na Jaji Mkuu wa Tanzania mstaafu, Mhe. Barnabas Albert Samatta.Sehemu ya wageni waalikwa (juu na chini) wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo kwenye picha) wakati wa uzinduzi wa Kitabu hicho.

 

Sehemu nyingine ya wageni (juu na chini) wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo kwenye picha).


Sehemu nyingine ya tatu ya wageni (juu na chini) wakiwa kwenye ufunguzi wa Kitabu hicho.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni