Na. Innocent Kansha - Mahakama
Waziri
wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dorothy
Gwajima amefungua rasmi mafunzo yanayoendeshwa kwa njia ya Mahakama ya Mfano
yenye kauli mbiu isemayo “ukatili na
ulaghai dhidi ya watoto mtandaoni” (Moot Court on Children Cyber
Bullying and Online Grooming) ikiwa ni sehemu ya kauli mbiu ya kitaifa ya kampeni
ya siku 16 ya kupinga ukatili wa kijinsia ambayo ni ‘Wekeza: Kupinga Ukatili wa
Kijinsia’.
Akifungua
Mahakama hiyo ya Mfano iliyoandaliwa na Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake
Tanzania (TAWJA) iliyoendeshwa kwenye ukumbi wa mikutano wa Nkrumah Chuo Kikuu
cha Dar es salaam leo tarehe 2 Desemba, 2023, Waziri Gwajima amesema, kauli
mbiu ya kitaifa ina lenga kuhamasisha kila Mtanzania, popote alipo na kwa
nafasi aliyokuwa nayo anatakiwa kuchukua hatua kupinga ukatili wa kijinsia.
“Niwapongeze
wanachama wa TAWJA ambao ni Majaji na Mahakimu, kwa kuchukua hatua katika
nafasi walizonazo na kuamaua kupaza sauti kwa kuandaa Mahakama ya Mfano
iliyojikita kwenye kesi ya mfano ya ukatili dhidi ya watoto mitandaoni kwani
kutokana na ukuaji wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA),
kesi za aina hii zimeanza kufikishwa Mahakamani”, amesema Waziri Gwajima.
Mhe. Gwajima amesema, takwimu zilizotolewa mwezi wa
Oktoba, 2023, na Waziri mwenye dhamana ya Habari,
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, wakati akifungua Kongamano la saba la
TEHAMA, zinaonyesha kuwa matumizi ya TEHAMA yameongezeka kutoka watumiaji
milioni 29.9 kwa mwezi Aprili 2022 hadi kufikia watu milioni 34.04 kwa mwezi
Juni 2023 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 13. Pamoja na mafanikio mengi yaliyoletwa na TEHAMA,
pamekuwepo pia changamoto ya uhalifu wa kimtandao ikiwemo uhalifu wa
unyanyasaji wa kimtandao dhidi ya wanawake na watoto.
Vilevile, Mhe. Gwajima akatoa Taarifa
ya Utafiti kuhusu Hali ya Ukatili wa Watoto Mtandaoni nchini, kwa mwaka 2022
(Disrupting Harm Report in Tanzania) inaeleza tathmini ya kina ya hali ya
ukatili wa kijinsia nchini, athari za ukatili wa kingono, mitazamo ya watoto
juu ya ukatili wa kingono mtandaoni na mwitikio wa kitaifa wa namna ya
kupambana na aina hii ya ukatili.
Matokeo
ya utafiti yanaonesha kuwa, asilimia 4 ya watumiaji wa mtandao wenye umri wa
miaka 12-17 nchini Tanzania ni manusura wa ukatili wa mtandaoni. Watoto wengi
hufanyiwa vitendo vya ukatili kupitia mitandao ya kijamii kama vile WhatsApp,
Instagram, Facebook, Tik Tok pamoja na mitando mengine ya kijamii.
Mhe.
Gwajima amebainisha athari zingine ikiwa ni wanaofanya vitendo vya ukatili ni
watu wanaofahamika na watoto wakiwemo ndugu wa karibu na marafiki na pia watoto
wanaofanyiwa ukatili hawajui namna na sehemu ya kutoa taarifa ili wapate msaada.
Aidha,
Waziri Gwajima akafafanua kuhusu hatua mbalimbali ambazo Serikali pamoja na Wizara
yake imezichukua ili kukabiliana na uwepo wa aina mpya ya Ukatili dhidi ya
Watoto Mitandaoni unaosababishwa na kukua kwa maendeleo ya Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano (TEHAMA).
Mhe.
Waziri Gwajima akatanabaisha kuwa kufuatia kuanza kwa kushamiri kwa matukio
haya ya ukatili wa kimtandao dhidi ya Watoto, Serikali imeunda kikosi kazi cha
Taifa cha Ulinzi na Usalama wa Mtoto mtandaoni chenye lengo la kuhakikisha kuwa
watoto wanalindwa dhidi ya ukatili wa mtandaoni na kuwasaidia kutumia vifaa vya
kieletroniki kwa usahihi na usalama,
Vilevile,
kuanza mchakato wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Mtoto ili iweze kuakisi
mazingira ya sasa ikiwa ni pamoja na ukatili wa watoto mtandaoni (online child
abuse) na Serikali inafanya mapitio ya Sera ya hali ya usalama katika mitandao
ili kubaini maeneo ya kuboresha, amesisitiza Mhe. Waziri Gwajima.
“Elimu itakayotolewa leo na TAWJA kupitia Mahakama ya Mfano
itasaidia sana kuelimisha wananchi kuhusu namna Mahakama zetu zinavyoshughulikia
kesi za ukatili wa kimtandao dhidi ya Watoto ambao ni Taifa la kesho, kuwapa
uafahamu wa matendo ya ukatili yanayofanyika kwenye mitandao na changamoto
zitokanazo na uhalifu wa unyanyasaji wa kimtandao hasa kwenye ukusanyaji wa ushahidi
na itasaidia pia kutahadharisha vijana wetu kuwa makini na matumizi salama na bora
ya huduma na bidhaa za TEHAMA’’, amefafanua Mhe. Gwajima.
Mhe. Waziri Gwajima amehitimisha kwa kutoa shukrani za
kipekee kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Jaji Mkuu wa Tanzania Zanzibar, Jaji Kiongozi,
Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Uongozi mzima wa Mahakama ya Tanzania Bara na
Visiwani. Nitakuwa mchoyo wa fadhila nikiwasahau Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao
wametupatia ukumbi wa kufanya Mafunzo hayo. Pia niwashukuru Chuo cha Sheria kwa
Vitendo na Chuo Kikuu cha Tumaini kwa kutoa taarifa na kuwaruhusu wanavyuo
kushirki mafunzo hayo.
Naye Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti Wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake
Tanzania (TAWJA) Mhe. Barke Sehel amesema Chama kimeandaa mkakati wa kuratibu
mafunzo ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa njia ya Mahakama ya Mfano katika
mikoa 5 ya Tanzania Bara na Zanzibar katika
mikoa ya Arusha, Dodoma, Mbeya, Mwanza na Zanzibar kwa tarehe tofauti tofauti
ili wadau wengi waweze kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo.
Mhe. Sehel amesema kuwa tayari mafunzo kama hayo wamekwisha
kutolewa katika Kanda 2 za Mahakama Kuu ambazo ni Dodoma na Arusha na yalikuwa
ya mafanikio makubwa sana kutokana na mwitikio wa wadau wanaopinga ukatili wa
kijinsia.
“Kama tunavyofahamu kuna sheria mbalimbali
zilizotungwa na serikali yetu dhidi ya uhalifu wa kimtandao, hata hivyo
maendeleo ya teknolojia yamekuwa yakikuwa na kusafiri kwa kasi ya mwanga na
hata matumizi yake yanaendelea kukua kila siku. Hii inaleta kuibuka kwa makosa mapya
ya kimtandao na hivyo kufanya baadhi ya sheria zetu kupitwa na wakati”,
amesisitiza Mhe. Sehel
Mwenyekiti huyo wa TAWJA akatoa mfano wa sheria hizo
kama sheria ya makosa ya kimtandao, unyanyasaji wa kimtandao (Cyber Bullying)
ni kosa la kijinai na adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka 3 au faini
isiyopungua shilingi milioni 5 au kutumikia kifungo na faini kutegemeana na
mazingitra ya kesi.
“Hata hivyo sheria hii ya makosa ya kimtandao aihakisi
mazingira na uhalisia, kwa sasa kumeibuka uhalifu wa kurusha moja kwa moja
picha za unyanyasaji wa kijinsia mtandaoni (Live streaming of sexual abuse)
uhalifu huu bado sheria haija itambua hivyo tunaomba Mhe. Waziri utambue hilo”,
ameongeza Mhe. Sehel
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni