Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama
Waandishi wa habari wametakiwa kuzingatia weledi,
nidhamu, uadilifu na uzalendo wanapotekeleza majukumu yao ya kuhabarisha na
kuelimisha Umma kuhusu masuala yanayohusu utoaji haki hususan majukumu ya Tume
ya Utumishi wa Mahakama.
Akifungua mafunzo ya kujenga uelewa kwa Waandishi wa
habari kuhusu Muundo na majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama jijini Dodoma,
Naibu Katibu wa Tume hiyo Bi. Enziel Mtei amesema ipo haja ya kutoa elimu
kuhusu Tume ambayo moja ya majukumu yake ni kushughulikia malalamiko yanayohusu
ukiukwaji wa maadili kwa Maafisa Mahakama ili wananchi waweze kuchukua hatua
wanapokuwa na malalamiko.
Naibu Katibu huyo aliwataka Waandishi wa habari
wanaoshiriki mafunzo hayo kuisaidia Tume katika kuwaelimisha wananchi kuhusu
majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama ikiwemo uwepo wa kamati za maadili ya
Maafisa Mahakama ngazi za mikoa na wilaya ambazo hupokea malalamiko ya wananchi yanayohusu ukiukwaji
wa maadili ya Maafisa Mahakama.
”Zingatieni nidhamu, uadilifu na uzalendo kwa kutambua
kuwa ninyi ni watanzania na siku zote mtangulize Taifa letu kwanza
mnapotekeleza majukumu yenu ya kuhabarisha na kuelimisha Umma”, alisisitiza.
Alisema jukumu la Tume ya Utumishi wa Mahakama ni
kuhakikisha Waandishi wa habari wanakuwa daraja muhimu kati ya Tume na wananchi
kwa kutoa taarifa sahihi kuhusu shughuli za Tume kwani ina matarajio ya kupata
taarifa sahihi.
Bi. Mtei alisema Tume ya Utumishi wa Mahakama itaimarisha
na kuendeleza ushirikiano uliopo kati yake na Waandishi wa habari kwa kwa lengo
la kufikia hatua ya juu zaidi ya ufanisi katika uelimishaji na utoaji wa
taarifa sahihi na muhimu kwa Umma.
Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa
Mahakama (Nidhamu na Maadili) Bi. Alesia Mbuya aliwataka Waandishi wa habari
waliopata mafunzo kuhusu Tume kuwa mabalozi wa Tume kwa kuwaelimisha wananchi
kuhusu Tume hiyo hususan uwepo wa kamati zinazopokea malalamiko yanayohusu
ukiukwaji wa maadili kwa Maafisa Mahakama (Mahakimu) zilizopo kwenye ngazi za
Mikoa na Wilaya ili waweze kuwasilisha malalamiko yao na kupata haki.
Awali akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki wa Mafunzo
hayo, Afisa Habari Mwandamizi wa Idara ya Habari Maelezo Bw. Jonas Kamaleki
alisema Tume ya Utumishi wa Mahakama haina budi kuongeza kasi katika
kujitangaza ili wananchi wengi zaidi waifahamu na kuitumia kwa kuwasilisha
malalamiko yao.
Tume ya Utumishi wa Mahakama iliandaa mafunzo kwa
Waandishi wa habari yenye lengo la kuwajengea uelewa kuhusu muundo na majukumu
yake ili washirikiane na Tume katika kufikisha elimu hiyo kwa wananchi wengi
zaidi.
Waandishi wa Habari kutoka Mikoa mbalimbali nchini wakiwa kwenye Mafunzo ya kuwajengea uelewa kuhusu Muundo na Majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama yaliyofanyika jijini Dodoma.
Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Nidhamu na Maadili ) Bi. Alesia Mbuya akitoa Mada wakati wa Mafunzo ya kuwajengea uelewa Waandishi wa Habari kuhusu Tume yaliyofanyika jijini Dodoma.
Mshiriki wa Mafunzo ambaye ni Mwandishi wa Habari wa ITV Mkoani Kagera Bw. Audax Mtiganzi akichangia hoja wakati wa mafunzo.
Mshiriki wa Mafunzo ambaye ni Mwandishi wa Habari wa Azam TV Dar es salaam a Bi. Upendo Michael akichangia hoja wakati wa mafunzo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni