Jumatano, 6 Desemba 2023

MKANDARASI AKABIDHIWA ENEO UJENZI WA KITUO JUMUISHI SONGEA

Na. Hasani Haufi- Mahakama Kuu, Songea.

Mkandarasi kutoka Kampuni ya Azhar Construction Co. Ltd Buildings and Civil Works ya jijini Dar es salaam, Mhandisi Kapinga Kapinga amekabidhiwa rasmi eneo kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Songea.

Jengo la Kituo hicho litajengwa katika eneo la Msamala, Nane Nane katika Manispaa ya Songea. Makabidhiano hayo yameshuhudiwa na wawakilishi kutoka Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Songea na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea.

Ujenzi wa Kituo hicho unafufua matumaini ya watumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Songea kuondokana na adha ya kutumia majengo ya zamani ambayo hayaendani na kasi ya miundombinu ya kisasa, hususani Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Makabidhiano hayo yameenda sambamba na kuanza kwa mradi huo baada ya Mkandarasi kupata kibali cha ujenzi ili kuendana na matakwa ya kimkataba.

Mwenyekiti wa kikao hicho cha makabidhiano, Msanifu Amri Mumba alieleza kuwa mradi huo ni wa miezi tisa na utaanza rasmi tarehe 04 Disemba, 2023, na kukamilika tarehe 03 Septemba, 2024 na kukabidhiwa mara baada ya kukamilika.

Mumba alimkumbusha Mkandarasi kuzingatia masuala yote yaliyomo kwenye mkataba ili kuepuka changamoto ambazo sio za lazima kwa kuwasiliana na Taasisi mbalimbali zinanzohusika na usalama wa jengo na watumishi kama Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Jeshi la Zima Moto na wengine.

Akihimiza kufanya kazi kama timu moja ili kufikia malengo kwa wakati kwani Mkandarasi akikwama ni sawa na kukwama Mwajiri.

Naye Mhandisi Mshauri wa Mahakama ya Tanzania Makao Makuu, Deogratius Lukansola alimkumbusha Mkandarasi kuwa mahusiano mazuri na wanaouzunguka utekelezaji wa mradi huo.

Alisema kuwa ikitokea mmoja kati ya watu wanaouzunguka mradi akitoa malalamiko ya kubughudhiwa katika mipaka au suala lingine la kimaslahi inaweza kusababisha mahusiano mabaya.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Bw. Tenganamba Epaphras aliahidi kuwapa ushirikiano na kufanya mawasiliano na Taasisi zote zinazohusika katika kufanikisha ujenzi wa mradi huo.

 

Makabadhiano ya mkataba kwa ajili ya ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Songea kati ya Mkandarasi, Mhandisi Kapinga Kapinga na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Bw. Tenganamba Epaphras.


Mkandarasi wa mradi wa ujenzi wa (IJC) Songea akioneshwa mipaka ya eneo la mradi.

Wawakilishi kutoka Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania wakikagua mipaka kabla ya kumkabidhi Mkandarasi.


Timu zima ya Mkandarasi Azhar Construction Co. Ltd Building & Civil Works ikiongozwa na Mhandisi Kapinga (watatu kutoka kulia).

Picha ya pamoja baina ya mkanadarasi Azhar Construction Co Ltd Building & Civil Works, Viongozi wa Mahakama Kanda ya Songea  na wawakilishi wa Mahakama ya Tanzania Makao Makuu.


(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni