Mwinga Mpoli – Mahakama, Mbeya
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Mbeya, Mhe. Dustan Ndunguru amewakumbusha wadau juu ya makosa yanayotendeka
kimtandao na kuwa nchi ilitunga sheria mahususi juu ya makosa hayo, hivyo ni
wajibu wetu kama wadau wa haki kusimama na kukemea vitendo hivi ukatili wa
kijinsia.
Ameyasema hayo hivi karibuni akiwa mgeni rasmi katika
maadhimisho ya siku 16 za kupinga unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kwa
wanawake na watoto, ambapo chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania
(TAWJA), kiliandaa zoezi la Mahakama ya Mfano na kuendesha kesi ya unyanyasaji
na ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto ambapo kauli mbiu ilikuwa ni
“kupinga unyanyasaji na ukatili wa kijinsia mitandaoni”. Zoezi ili lilihusisha
waheshimiwa majaji, mahakimu, mawakili wa serikali, mawakili wa kujitegemea, polisi,
wakufunzi na wanafunzi wa vyuo vikuu Mzumbe na CUCoM mkoa wa Mbeya.
“Nimefurahi
kuona kuwa mmeshirikisha watu mbalimbali wakiwemo wanafunzi na naamini zoezi
ili la Mahakama ya mfano litasaidia kujua makosa ya kimitandao, mara nyingi
tunajisahau na kuhisi tunafanya utani ila ni muhimu tukumbuke kuna madhara ya
maneno yetu mitandaoni na ili suala limekuwa likituathiri na kama walengwa kwa
pamoja tusimame kupinga unyanyasi na ukatili wa kijinsia. Tuelimike lakini pia
tuielimishe jamii inayotuzunguka” alisema Mhe. Ndunguru
Pia alishukuru TAWJA, Mahakama ya Tanzania na
washiriki wengine wote kwa kuona umuhimu wa kushiriki katika maadhimisho hayo
ya kupinga unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
Aidha uongozi wa TAWJA Mbeya ulisimamia na kuendesha
zoezi ilo la Mahakama ya mfano ikiwa washiriki katika Mahakama hiyo wakiwa ni
Mahakimu, mawakili wa serikali, Mawakili wa kujitegemea, mapolisi pamoja na
wanafunzi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Dustan Ndunguru (wapili kushoto) akiwa sehemu ya washiriki wa zoezi hilo la uendeshaji kesi ya Mahakama ya Mfano na watatu kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa akifuatilia na washiriki wengine.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Dustan Ndunguru (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau walioshiriki zoezi la uendeshaji wa Mahakama ya Mfano na wa kwanza kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni