Alhamisi, 7 Desemba 2023

WATUMISHI WA MAHAKAMA WATAKIWA KUTEKELEZA NA KUZINGATIA MATUMIZI YA MFUMO WA ‘PEPMIS’

Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daud ametoa rai kwa Watumishi wa Mahakama kusimamia vizuri Mfumo mpya wa Kupima Utendaji Kazi wa Watumishi (PEPMIS). 

Bw. Daud aliyasema hayo jana tarehe 06 Desemba, 2023 alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania ikijumuisha Watendaji wa Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu Kanda, Divisheni Maalum, Wakuu wa Idara/Vitengo, Wakurugenzi Wasaidizi, baadhi ya Maafisa wa Mahakama ya Tanzania wakati wa kufunga Mafunzo ya siku tatu kuhusu matumizi ya Mfumo wa PEPMIS yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma.

“Serikali imekuwa ikifanya maboresho kwa nyakati tofauti na eneo la kwanza ambalo tuliona tuliangalie ni kwenye mifumo ya uendeshaji wa Serikali ikiwemo ya utendaji kazi, kwa sababu Mtumishi wa umma akifanya kazi vizuri mambo mengine yote yanakwenda,” alisema Bw. Daud.  

Alisema kuwa, rasilimali watu ni rasilimali muhimu kuliko nyingine zote na inasimamia rasilimali nyingine zote. Hivyo, ni muhimu kila mmoja atekeleze majukumu yake ipasavyo kwakuwa Serikali haitamvumilia mtumishi yoyote ambaye hataendana na kasi ya matumizi ya Mfumo huo.

Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu huyo, Mfumo huu utatumika kupima utendaji kazi wa mtumishi mmoja mmoja kuanzia ngazi ya Menejimenti mpaka Watumishi wa chini wakiwemo Waandishi Waendesha Ofisi, Madereva, Wasaidizi wa Ofisi na kadhalika.

Aliongeza kuwa, Mfumo wa PEPMIS umebuniwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kufuatia changamoto zilizobainika katika utekelezaji wa Mfumo uliokuwa ukitumika awali ujulikanao kwa jina la Mfumo wa Wazi wa Upimaji wa Utendaji Kazi maarufu kama OPRAS.

Naye Kaimu Mtendaji Mkuu - Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso aliishukuru Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kutoa mafunzo hayo kwa Watumishi wa Mahakama na kuahidi kuwa, kwa upande wa Mahakama hakuna mtumishi atakayekwamisha zoezi hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu - Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick alisema kwamba, Mafunzo yataendelea kutolewa kwa awamu kwa Watendaji na watumishi wengine wa Mahakama ili kuhakikisha kuwa, Mfumo unatumika kwa Taasisi nzima.

“Mpaka sasa Menejimenti pamoja na Maafisa kadhaa tayari wameshapatiwa mafunzo ya jinsi kuutumia mfumo huo,” alisema Bi. Beatrice.

Maelekezo yaliyotolewa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mfumo huu unapaswa kuanza kutumika ndani ya Mahakama kuanzia tarehe 30 Desemba, 2023.

Sambamba na Mfumo wa PEPMIS, Mfumo mwingine uliobuniwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ni wa PIPMIS unaopima na kutathmini utendaji kazi wa Taasisi kwa ujumla wake.


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daud akizungumza na sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania (hawapo katika picha) wakati wa kufunga Mafunzo ya jinsi ya kutumia Mfumo mpya wa Serikali wa upimaji wa utendaji kazi kwa Watumishi (PEPMIS). Hafla hiyo ilifanyika jana 06 Desemba, 2023 katika Ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma. Kushoto kwake ni Kaimu Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus M. Uisso na kulia kwake ni Mkurugenzi wa Utumishi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Felister Shuli.
 
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daud (hayupo katika picha) wakati wa mafunzo kuhusu matumizi ya Mfumo wa PEPMIS yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma.

Kaimu Mtendaji Mkuu - Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus  Uisso (aliyesimama) akizungumza jambo wakati wa hafla fupi ya kufunga mafunzo ya matumizi ya Mifumo ya PEPMIS na PIPMIS.

Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bi. Beatrice Patrick akitoa neno la utangulizi wakati wa hafla fupi ya kufunga mafunzo ya matumizi ya Mifumo ya 'PEPMIS' na 'PIPMIS'.

Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Nyasinde Mukono (kulia) pamoja na Bi. Gloria Mlaki (Mchumi) ambao ni Wawezeshaji wa Mafunzo hayo wakifuatilia kinachojiri.

Picha za watumishi wakifuatilia kwa umakini yaliyokuwa yakijiri katika hafla fupi ya kufunga mafunzo ya matumizi ya 'PEPMIS' na 'PIPMIS'.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni