Na. Paul Pascal-Mahakama, Moshi
Majaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi Mhe. Safina Simfukwe na Mhe. Adrian
Kilima wamefanya kaguzi za Mahakama za chini kukagua shughuli za uendeshaji wa
Mahakama ikiwa pamoja na kuhakikisha watumishi wa Mahakama hizo wanafanya kazi
kwa kuzingatia na kuiishi salamu ya Mahakama ya Tanzania inayojengwa na maneno
ya Uadilifu,Weledi na Uwajibikaji.
Akizungumza
katika kikao na watumishi wa Mahakama za Wilaya ya Same na Mwanga kwa nyakati
tofauti katika ziara hiyo Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi Mhe.
Safina Simfukwe aliwapongeze watumishi wote wa Mahakama hizo kwa kutimiza
majukumu yao ya msingi kwa kuzingatia weledi, uadilifu na ubunifu katika
kutatua changamoto zitokanazo na majukumu yao.
“Utendaji
kazi wenu mzuri umepelekea kuondokana na mashauri ya mlundikano katika vituo
vyenu, vilevile niwatake watumishi wote muiishi dira ya Mahakama ya Tanzania
haswa kauli mbiu yetu ya uadilifu, weledi na uwajibikaji itavutia sana
watumishi wote tuiishi kwa vitendo salamu hii haswa kwa kujiepusha na vitendo
vya utovu wa maadili na kutimiza majukumu yetu kwa wakati”, aliongeza Mhe. Simfukwe.
Kwa
upande wake Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi Mhe. Adrian Kilimi
akiwa katika Wilaya za Siha na Hai aliwambia watumishi wa Mahakama hizo kuwa utendaji
kazi wao ni mzuri unaridhisha kwa kiwango kikubwa na taarifa zao za hali ya
mashauri katika Wilaya hizo inavutia kutokana na kasi ya uondoshaji wa
mashauri.
“Niwapongeze
watumishi wote kwa kuwa kazi ya kutoa haki siyo nyepese inahitaji ushirikiano wetu
sote pia niwatake watumishi wenzangu tuhakikishe tunaondokana na utamaduni usiyo
na tija wa kufanya vitendo visivyo vya kimaadili, uzembe na uvivu. Lazima kila
mmoja wetu awe mwadilifu na kuzingatia weledi kwa kuwa tumeaminiwa nakupewa
nafasi tunazozitumikia”, aliongeza Mhe. Kilimi.
Naye,
Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi Bi. Maria Itala akizungumza na watumishi
hao aliwashukuru watumishi wote katika Wilaya hizo kwa kuendelea kuimarisha
taswira chanya katika jamii wanayoihudumia.
“Hakika
mmeitekeleza kwa vitendo nguzo namba tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama tunaoendelea
kuutekeleza niwaombe ushirikiano zaidi ili zile kasoro ndogondogo zilizoonekana
zisijitokeze na tuzishughulikie kwa pamoja”, alisema Bi. Itala
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi Mhe. Safina Simfukwe (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja sehemu ya viongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi wakati wa zoezi la ukaguzi wa shughuli za Mahakama katika Kanda hiyo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi Mhe. Safina Simfukwe akisaini Kitabu cha wageni alipokuwa kwenye ziara ya ukaguzi.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi Mhe. Adrian Kilimi akisaini kitabu cha wageni alipokuwa kwenye ziara ya ukaguzi.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi Bi. Maria Itala akikabidhi nyaraka ya mtiririko wa majukumu ya ukaguzi kwa Afisa wa Mahakama ya Wilaya.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi Bi. Maria Itala akisaini kitabu cha wageni alipokuwa kwenye ziara ya ukaguzi
Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni