· Naibu Msajili, Hakimu Mahakama ya Mwanzo nao wamo
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Songea
Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Shaban Ally Lila ametunukiwa Shahada ya Umahiri ya Sheria na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika mahafali ya 42 yaliyofanyika mjini Songea, mkoani Ruvuma hivi karibuni.
Mhe. Lila alikuwa miongoni mwa wahitimu 11 waliotunukiwa shahada hiyo baada ya kufanya vizuri katika masomo yake akitokea katika Kituo cha Ilala jijini Dar es Salaam.
Mtumishi wingine wa Mahakama ya Tanzania aliyetunukiwa shahada hiyo ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Mlingoti iliyopo Wilaya ya Tunduru, Mhe. Anisa Ramadhani aliyekuwa anasoma kutokea Kituo cha Kinondoni.
“Kwa mamlaka niliyopewa ninakutunukuni Shahada ya Umahiri ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika fani husika hao wote ambao majina yao yameorodheshwa kwenye kitabu cha mahafali ya 42,” alisikika Mkuu wa Chuo na Waziri Mkuu mstaafu, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda akisema.
Katika mahafali hayo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Kifungu Mrisho Kariho alitunukiwa Stashahada ya Uzamili katika Sheria baada ya kufanya vizuri katika masomo yake akitokea katika Kituo cha Kinondoni.
Watumishi hao wa Mahakama ya Tanzania walikuwa kivutio kikubwa katika mahafali hayo baada ya kutajwa mmoja mmoja kwa majina yao kufuatia kufanya vizuri katika masomo licha ya kuwa na shughuli nyingi kwenye vituo vyao vya kazi wakiwatumikia Watanzania kwenye muktadha mzima wa utoaji haki.
Mtumishi mwingine wa Mahakama aliyehitimu katika mahafali hayo ni Afisa Habari, Bw. Faustine Kapama aliyetunukiwa Shahada ya Kwanza ya Sanaa katika Mawasiliano ya Umma baada ya kufaulu na kustahili kupata shahada hiyo akitokea katika Kituo cha Kinondoni Dar es Salaam.
Mahafali hayo yalihudhuriwa na maelfu ya wahitimu, wakiwemo 54 waliofaulu na kustahili kutunukiwa Shahada ya Uzamivu (Doctor of Philosophy) na kati yao wanaume walikuwa 45 na wanawake tisa, ambao ni sawa na asilimia 17.
Jumla ya wahitimu 516 walifaulu na kustahili kutunukiwa Shahada ya Umahiri katika fani mbalimbali, kati yao wanaume walikuwa 317 na wanawake 199 na wahitimu 95, kati yao 66 ni wanaume na 29 wanawake walifaulu na kustahili kutunukiwa Stashahada ya Uzamili.
Wanafunzi 396 katika Kitivo cha Elimu pia wamefaulu na kustahili kutunukiwa Shahada ya Kwanza katika fani mbalimbali, wanafunzi 347 katika Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii walifaulu na kustahili kutunukiwa Shahada ya Kwanza katika fani mbalimbali na wanafunzi 122 katika Kitivo cha Sheria nao wamefaulu na kutunukiwa Shahada ya Kwanza ya Sheria.
Kadhalika, wanafunzi 287 katika Kitivo cha Biashara na Uongozi wamefaulu na kustahili kutunukiwa Shahada ya Kwanza kwenye maeneo tofauti, huku wanafunzi 125 katika kitivo cha Sayansi, Teknolojia na Taaluma za Mazingira wakifuzu na kustahili kutunukiwa Shahada ya Kwanza katika fani mbalimbali.
Katika mahafali hayo, kulikuwepo pia na wahitimu 830 ambao walifaulu na kustahili kutunukiwa Stashahada (Diploma) ya chuo hicho na kati yao wanaume ni 382 na wanawake wakiwa 448. Kulikuwepo pia na wahitimu 1,206 ambao wamefuzu na kustahili kutunukiwa Astashahada (Certificate) katika maeneo mbalimbali.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo alikuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro. Akizungumza katika mahafali hayo, Mhe. Dkt. Ndumaro aliwahimiza wahitimu wote kwenda kutumia elimu waliyopata siyo kwa manufaa yao binafsi pekee bali pia kwa faida ya jamii na Watanzania kwa ujumla.
Alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuanza kufundisha kwa lazima somo la Kiswahili kwa wanafunzi wote wanaotoka nje ya Tanzania ili kutekeleza azma ya Serikali ya kukuza na kuendeleza lugha hiyo duniani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni