Na Tiganya Vincent-Mahakama-Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitaka Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania Bara (JMAT) kuwahimiza wanachama wao kuhakikisha wanabaki ndani ya maadili mema na kutoa huduma zilizo bora na kwa wakati.
Ametoa kauli hiyo leo tarehe 19 Desemba, 2023 wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania Bara (JMAT) jijini Dodoma.
“Wajibu wenu kama JMAT kusimamia na kuhimiza uwazi, uwajibikaji...,” alisema Jaji Mkuu na kuongeza, “Wanachama wa JMAT mnao wajibu wa kupeana nasaha, kushauriana na kuwaonya wanachama ambao wanakiuka Kanuni za Maadili kusubiri Kamati za Maadili kushughulikia.”
Mhe. Prof. Juma aliongeza kuwa Wanachama wa JMAT, endapo wataona wadau wanaoendesha mashauri (kwa mfano, Mawakili wa kujitegemea, Mawakili wa Serikali, Madalali, Wasambaza kumbukumbu) wanakiuka maadili ya Taasisi zao, ni jukumu lao kufikisha taarifa kwa vyombo vyao vya kimaadili.
Wanachama wa JMAT wahimizwa kujiendeleza kielimu
Jaji Mkuu aliwataka wanachama wa JMAT kuendeleza katika masomo yenye maudhui ambayo yatawawezesha kufanyakazi kwa kuzingatia mahitaji ya karne ya 21.
“Tusikimbilie kusoma Shahada za Uzamili au Uzamivu, zenye maudhui ya zamani. Someni yale ambayo yatawajenga kuweza kufanya kazi katika Karne ya 21. Masomo kama Legal-Tech, Project Management, Business Process Management, ADR, negotiation skills,”alisema.
“Mahakama ya Tanzania tayari kuna mfano ya Maafisa wa Mahakama ambao wamesoma na kujiunga katika maeneo mapya ya masomo akiwemo Mhe. Dkt Ubena John, sasa hivi ni “Associate Professor Information Technology Law”. Mhe. Desdery Kamugisha kujitambulisha kuwa – Mtaalam wa Court Business Process. Pia Mhe. Jaji Dkt Angelo Rumisha ni Mtaalum wa Maboresho, Project Management,” aliongeza.
Aidha, Mhe. Prof. Juma aliitaka JMAT kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama, katika kuhakikisha kuwa wanachama wote hawaachwi nyuma na mabadiliko makubwa yanayoendelea duniani yakiwemo mabadiliko makubwa katika matumizi ya kiteknolojia kwa kuhimiza mufunzo endelevu na elimu endelevu.
JMAT watakiwa kutumia mkutano wa mwaka kujitathmini, kupanga mikakati
Mhe. Prof. Juma alisema Mkutano wa JMAT ni wakati wa wanachama kutathmini na kupanga mikakati ya kukabiliana na maudhui ya mabadiliko makubwa yanayowazunguka ili wabadili namna wanavyotoa huduma za utoaji haki.
Alisema Uongozi wa Mahakama ya Tanzania unatambua kuwa vikao mbalimbali vya JMAT ni sehemu muhimu ya kuwashirikisha Majaji na Mahakimu katika masuala mbalimbali muhimu kwa JMAT na kwa Mahakama.
Mhe. Prof. Juma aliongeza kuwa JMAT ni kiungo muhimu kinachowaunganisha Majaji na Mahakimu wa Tanzania, na Majaji na Mahakimu kutoka maeneo mengine duniani, hivyo inayo nafasi kubwa ya kuandaa mikutano, semina na kongamano zenye malengo ya kujadili maeneo mapya yanayogusa kazi za kila siku za Majaji na Mahakimu.
Aliwasihi wanachama wa JMAT wanapohudhuria semina, mikutano, makongamano ya kimataifa, kujenga tabia ya kurudi na mafunzo ya kimaboresho ambayo yatawasaidia wengine katika kuboresha utoaji haki Tanzania.
Kushiriki katika maoni ya kuandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa
Jaji Mkuu amewataka wanachama wa JMAT na watumishi wa Mahakama ya Tanzania kushiriki katika kutoa maoni kuandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050 ili kuhakikisha suala la utoaji haki linaonekana vizuri.
“JMAT ni wajibu wenu kuwatayarisha wanachama wachangie mawazo hususan kuhusu nafasi ya Mahakama na mfumo wa utoaji haki katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Tanzania 2050,” alisema.
“Dira ya Maendeleo ya Taifa ni Dira kwa mihimili yote mitatu ya Dola. Mhimili wa Mahakama tusijifiche na kujitenga. Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 inayokaribia kufikia ukingoni, ilitukumbusha maudhui ya Karne ya 21,” aliongeza Jaji Mkuu.
Alisema Dira inawakumbusha kuwa endapo watakuwa washiriki hai katika maendeleo ya dunia ya Karne ya 21, lazima kama nchi, watafute mbinu za kujiimarisha katika maeneo yote ya kiushindani.
Mhe. Prof. Juma alisema Mahakama ya Tanzania kupitia wanachama wa Chama Cha Majaji na Mahakimu Tanzania wametekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 kadri walivyoweza kupitia Mpango Mkakati na Programu za Maboresho Awamu ya Kwanza na sasa Awamu ya Pili.
JMAT kushiriki kutoa mawazo kuhusu elimu ya sheria
Jaji Mkuu amewataka wanachama wa JMAT kushiriki kutoa maoni ambayo yatasaidia katika kuboresha mifumo na Sheria zinazoongoza elimu ya sheria hivi sasa, kuanzia elimu ya sheria vyuo vikuu, katika Taasisi za elimu ya juu, Shule ya Sheria kwa Vitendo, na hata Elimu ya Sheria Endelevu na Uwakili.
Alisema kuwa kazi zinazofanywa na Wanasheria zimejengwa kukidhi mahitaji ya karne zilizopita za 19 na 20.
“Elimu ya Sheria haiwezi kubaki ya kizamani wakati huu ambao Serikali imetambua mabadiliko katika Karne ya 21 kwa kutayarisha Sera ya Elimu na Mafunzo (2014) na Mitaala iliyoboreshwa 2023… Lazima wanachama wa JMAT waanze kujadili na kutoa mapendekezo ya Elimu ya Sheria itakayolingana na mahitaji ya Karne ya 21,” alisema.
Jaji Mkuu ambaye pia ni Mlezi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT), Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akishiriki kuimba wimbo wa Taifa na ule wa Afrika Mashariki kabla hajafungua Mkutano wa JMAT ambao umeanza leo tarehe 19 Desemba 2023 jijini Dodoma. Wengine katika picha ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani( wa pili kutoka kushoto), Rais wa JMAT ambaye pia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza(wa pili kutoka kulia) , Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo(kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabrriel(kulia).
Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) ambaye pia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kufungua Mkutano wa JMAT leo tarehe 19 Desemba 2023 jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni